Vatican News
Tanzia: Askofu Evaristo Marcus Chengula amefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018. Tanzia: Askofu Evaristo Marcus Chengula amefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018.  (AFP or licensors)

TANZIA: Askofu Evaristo Marcus Chengula amefariki dunia!

Askofu Evaristo Marcus Chengula alizaliwa tarehe Mosi Januari 1941, huko Mdabulo, Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre, tarehe 15 Oktoba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Novemba 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 2 Februari 1997.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Evaristo Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya kilichotokea, Jumatano, tarehe 21 Novemba 2018 majira ya saa 3:00 asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jijini Dar es Salaam. Akizungumza na Vatican News, Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema, Marehemu Askofu Chengula aliwasili Jijini Dar es Salaam, Jumanne, tarehe 20 Novemba 2018 akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo! Akapelekwa na kulazwa kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jitihada za Madaktari kutaka kuokoa maisha yake, zikagonga mwamba na Askofu Evaristo Marcus Chengula akaaga dunia katika usingizi wa amani, akiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele!

Itakumbukwa kwamba Askofu Evaristo Marcus Chengula alizaliwa tarehe Mosi Januari 1941, huko Mdabulo, Wilaya y Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre, tarehe 15 Oktoba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Novemba 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 2 Februari 1997. Amefariki dunia akiwa amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 48 na Askofu kwa muda wa miaka 21! Apumzike katika usingizi wa amani, akiwa tayari kukutana uso kwa uso na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma na mapendo!

Maana ya Kikristo ya Kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani yake mna tumaini moja la maisha ya uzima wa milele. Kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Ubatizo, “kufanana” kamili na “sura ya Mwana”, kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mbinguni, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Kifo ni jambo linalosababisha majonzi na machungu, lakini kwa waamini wenye imani na matumaini hawana haja ya kuogopa Fumbo la Kifo katika maisha yao, kwani wanaunganishwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu, aliyeshinda dhambi na mauti! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaomnbea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2017-2018 alikazia umuhimu wa waamini kwenda kumlaki Bwana arusi, huku wakiwa na akiba ya mafuta yatakayotumika kuwashia taa; ukuaji wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku pamoja na kuwa na maandalizi makini! Wito na maisha ya Kikristo, daima ni mwaliko wa kutoka, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, na kwamba, waamini ni wasafiri hadi dakika ya mwisho!

Maandiko Matakatifu yanasema, safari hii ni mwaliko wa kwenda kukutana na Bwana arusi, Kristo Yesu aliyelipenda Kanisa lake upeo, kiasi hata cha kujisadaka, ili kuwaangazia njia wale wanaomfuasa, changamoto ni kuendelea kukua na kukomaa katika upendo wa kukutana na Bwana arusi, kilele cha maandalizi yote! Moyo uliosheheni mapendo unaweza kuwasaidia viongozi wa Kanisa kukaza macho yao kwa vile visivyoonekana; ili kuambata mambo msingi katika maisha, tayari kusikiliza sauti ya Kristo, anayekuja kuwaletea chachu ya mageuzi ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, mafuta ya akiba yaliyohifadhiwa kwenye chombo kidogo ni muhimu zaidi kuliko hata vazi la arusi na taa zenyewe, kwani Mwenyezi Mungu anaangalia yale yaliyofichika mioyoni na wala si heshima, nguvu na madaraka; utukufu na mwonekano wa nje; mambo ambayo yanapita na kutoweka kama ndoto ya mchana! Waamini wajitahidi kuboresha maisha yao ya ndani na kamwe wasipende kuonekana kwa nje. Toba na wongofu wa ndani, usaidie mchakato wa kuyatakatifuza maisha ya ndani, ili yaweze kumpendeza Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka bila ya kujibakiza katika toba na wongofu wa ndani, ili kuwa mwanga angavu unaosimikwa katika huduma, kwani falsafa ya kuishi ni huduma. Huduma makini ndio utambulisho unaomwezesha mwamini kuingia katika Karamu ya Mwanakondoo wa Mungu. Jambo la msingi kutambua ni kwa kiasi gani, kama viongozi wameweza kujisadaka bila ya kujibakiza ili kulipa gharama ya upendo wa Mungu. Upendo wa dhati ni maisha yanaosimikwa katika huduma inayopaswa kushuhudiwa na kutolewa sadaka pasi na uchoyo wala ubinafsi!

Askofu Evaristo Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya katika maisha na utume wake, kuna mambo ambayo alipenda kuyapatia kipaumbele cha kwanza: Utakatifu na ukuu wa Daraja Takatifu ya Upadre; Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika ukoloni wa kiitikadi; elimu na malezi fungamani, ili kujenga taifa la watu wanaowajibika sanjari na kuyatakatifuza malimwengu!

DARAJA TAKATIFU YA UPADRE: Dhamana kuu ya Askofu ndani ya Kanisa ni kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu ili waweze kufika mbinguni, kila mtu akijitahidi kutekeleza wito wake kadiri ya maisha aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, yote yakifanyika kwa sifa na utukufu wa Mungu. Askofu anao wajibu wa kudumisha umoja miongoni mwa kundi alilokabidhiwa na Mama Kanisa, akiendelea kukazia upendo, huruma na uvumilivu. Hayo yamebainishwa na Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya wakati wa kumwimbia  Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa maadhimisho ya miaka kumi na mbili tangu alipowekwa wakfu kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, sherehe ambazo zilikwenda sanjari na maadhimisho ya Siku ya kumi na tatu ya watawa duniani, Kanisa lilipokuwa linamkumbuka Bikira Maria na Yosefu walivyokwenda Yerusalemu kumtolea Mungu sadaka ya mwanamzaliwa wa kwanza wao.

Wito huo umetolewa na Askofu Evaristo Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Jacob Machibya, iliyofanyika Parokia ya Chunya Jimboni Humo, tarehe 16 Agosti 2018. Askofu Chengula Katika mahubiri yake Amebainisha kwamba yapo mambo mengi ambayo yanawezesha kujua kiongozi bora na muadilifu mbe za watu, lakini kipimo ambacho pia kitaimarisha zaidi nafasi yako kama padre ni pamoja na kufanya mambo sahihi na kwa wakati muafaka. “Sidhani kama litakuwa jambo la busara kwa Padre kukaa klabuni na kuanza kunywa pombe, hapana hiyo siyo tabia njema” Alisisitiza Askofu Chengula.

INJILI YA FAMILIA: Askofu Chengula amewahimiza wanafamilia kujitahidi kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Nazareti, kwa kukazia maadili na utu wema, bila kusahahu kuungana na Kristo kwa njia ya maisha ya Kisakramenti. Muungano huu uwakirimie waamini utu wema wanaoweza kuutolea ushuhuda katika maisha yao. Askofu Chengula amewaasa viongozi wa Kanisa kuendeleza katekesi kuhusu umuhimu wa siku kuu mbali mbali za Kanisa katika maisha na changamoto wanazopaswa kuzitolea ushuhuda. Askofu Evaristo Chengula amemshukuru Mungu kwa wema wote aliomkirimia kama Askofu wa Jimbo la Mbeya, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu. Wito umetolewa kwa viongozi wote wa Ibada hususani Mapadre kutambua ya kuwa, Kunywa pombe kilabuni siyo tabia za Mapadre mzuri ambaye ana Muwakilisha Kristo Yesu hapa duniani.

ELIMU NA MALEZI FUNGAMANI: “Tafuteni sababu za kufeli,na sioni kama kuna sababu za msingi endapo mtawalipa walimu mishahara yao vizuri na kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi,kuweni wema sawa lakini haki ya walimu wapeni…acheni kuwafukuza ovyo walimu kwa sababu za kisiasa wakae muda mrefu vinginevyo hata mngekuwa na majengo na mabweni mazuri ni bure.” “Mwalimu anayeshindwa somo aangaliwe na kuonywa ninashukuru kwa utaratibu mlioanza wa kutemebeleana wanafunzi na walimu kubadilishana uzoefu itasaidia kuziinua shule ambazo hazifanyi vizuri,Nnimesikia wanafunzi na walimu wa St.Francis wamekwenda kufanya semina Panda Hill, James Sangu na Igawilo endeleeni.”

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyotolewa na Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya wakati wa kupokea taarifa ya matokeo ya kidato cha pili, nne na sita kutoka katika shule zinazomilikiwa na kusimamiwa na Jimbo Katoliki la Mbeya kuwa daraja la nne halina nafasi katika mitihani inayokuja kwani alama hiyo inamnyima usingizi. Askofu Chengula ametoa onyo kwa shule zinazoendeshwa na kusimamiwa na Jimbo kuwa wakuu wa shule na walimu watakaosababisha kupata alama za daraja la nne watawajibishwa mara moja.

Anasema zamani wanafunzi waliofaulu kutoka shule za Serikali walikuwa wakipelekwa Sekondari za Tabora na Malangali na Kanisa Katoliki lilikuwa likiwapeleka wanafunzi wake Tosamaganga na Pugu na ushindani mkubwa ulikuwepo hivyo ametoa pendekezo lake kujaribu kurejesha utaratibu huo ili kuboresha kiwango cha taaluma katika Shule za Kanisa. Licha ya kuwapongeza amewataka wakuu wa shule kuweka utaratibu wa kuwalea na kuwaandaa watoto kitaaluma na katika maadili mema, tangu elimu ya chekechea hadi vyuo vikuu mintarafu mwongozo wa Kanisa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Tanzania.

Askofu Chengula
21 November 2018, 14:26