Bima ya Afya nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi zinazopaswa kuvaliwa njuga na wafau mbali mbali. Bima ya Afya nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi zinazopaswa kuvaliwa njuga na wafau mbali mbali. 

Ripoti ya afya kutoka kwa viongozi wa kidini na changamoto zake nchini Tanzania

Ripoti ya viongozi wa kidini kuhusu hifadhi ya jamii kwenye sekta ya afya inaonesha kwamba, Tanzania inaweza kuongeza au kugharimia upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote kwa kutumia fedha za mapato yake ya ndani bila kutegemea ufadhili mkubwa kutoka nje.

Na Rodrick Minja, Sarah Pelaji na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa. - Dodoma.

Serikali ya Tanzania imepokea ripoti ya Viongozi wa dini kuhusu hifadhi ya jamii kwenye sekta ya afya, tarehe 4 Oktoba 2018 katika Mkutano wa Viongozi wa dini mbalimbali uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Mt. Gaspari, Jijini Dodoma. Akiwasilisha Ripoti hiyo ya Viongozi wa dini Mtafiti katika Kamati ya Dini mbalimbali nchini Tanzania Dr. Moses Kulaba amesema kuwa, ripoti hiyo inajaribu kujibu swali la msingi ‘Je, tunawezeje kuongeza upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwenye sekta ya Afya kwa kutumia mapato au fedha ya ndani? Amesema ripoti inaonesha kwamba, Tanzania inaweza kuongeza au kugharimia upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote kwa kutumia fedha za mapato yake ya ndani bila kutegemea ufadhili mkubwa kutoka nje.

Ripoti imetazama hali ya sasa hivi ya upatikanaji wa Bima ya Afya kwa watanzania na haswa watu wa kipato cha chini. Imeangalia mafanikio na mapungufu ya kisera, ki takwimu na kibajeti na changamoto za upatikanaji wa bima ya Afya kwa watanzania wengi zaidi. Ripoti inapendekeza njia mbadala za muda mfupi na mrefu zinazoweza kusaidia Serikali kugarimia watu au kaaya masikini wapate Bima Afya na kuongeza usajili wa idadi ya watu wenye Bima ya Afya kutoka asilimia 32 mpaka Asilimia 100 ifikapo 2025. Tarifa zinaonyesha changamoto kubwa za kisera, kimfumo na kifedha kwa ajili ya upatikanaji wa Bima ya Afya.

Serikali ya Tanzania inahitaji shilingi billion 290 ili kufikia asilimia mia moja ya watanzani wote (ikiwemo na wanolipiwa na makampuni binafsi) kupata Bima ya Afya ndani ya miaka 5-6. Ili kupunguza mzigo wa kibajeti serikali inaweza kulenga kufikia kaaya asimilia 17 kila mwaka kwa miaka mitano hadi sita. Serikali inaweza kulipia  kaaya maskini (28% ya wananchi wote nchini Tanzania) kwa kutenga asilimia 19% tu kutoka kwenye vyanzo vya kodi mbali mbali.  Kiwango cha kodi kutoka kodi ya ongezeko ya thamani ni kidogo sana sawa na asilimia 0.15% kila mwaka na kufikia asilimia 0.9% ni 2025.Viwango hivi ni vidogo na vinawezekana. Serikali ianzishe utaratibu wa kutenga asilimia ya kiasi kutokana na vyanzo vya kodi mbali mbali kama tulivyopendekeza hapo juu ili kulipia garama Bima ya Afya. Serikali iwawezeshe kaaya masikini (asilimia28) kupata Bima ya afya kwa kulipia elfu 50,000 huku kaaya zikichangia elfu 10,000. Serikali itenge pesa za kutosha kuchangia kaaya asilimia 40 ambao wako kwenye sekta binafsi kama mchango wanapojiunga.

Aidha ripoti imetoa majukumu kwa serikali na viongozi wa dini huku wakiitaka Serikali kufanya Mabadiliko ya kisera, kimufumo na utaratibu wa kikodi, Upatikanaji wa huduma na malipo kwa watoa huduma. Viongozi wa dini wafanye uhamasishaji wa waamini wao,  kutoa huduma kupitia vituo vyao vya afya, kufuatilia na kufanya tathmini ya upatikanaji wa huduma, ubora ya afya nchini Tanzania.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dokta John Athony Kiangu Jingu amebainisha kuwa jukumu kubwa la serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dokta John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa msisitizo mkubwa ni kuwahudumia walio wanyonge. Hayo ameyasema hivi karibuni Jijini Dodoma alipokuwa akitoa hotuba yake kwa viongozi wa dini mbalimbali nchini Tanzania waliohudhuria uzinduzi wa ripoti kuhusu hifadhi ya jamii kwenye sekta ya afya. Amesema kuwa viongozi wa dini wamekuwa wakihubiria waamini wao juu ya huduma kwa wanyonge na maskini zaidi pamoja na kuwasaidia walio wadogo.

"Serikali yetu tangu ipate uhuru imekuwa ikisisitiza hivyo wakati iliposisitiza kupiga vita maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini ilikuwa inamaanisha hivyo" aliongeza Dokta Jingu. Hata hivyo amesema kauli ya Rais Magufuli ya kuwa yeye ni Rais wa wanyonge ina maana kuwa serikali yake ni ya wanyonge hivyo mkazo ni kuwahudumia wanyonge ndio maana serikali imeweka idara maalumu ya kuwashughulikia walio wanyonge ambayo Wizara yake ni Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.

Dokta Jingu amesema kuwa Wizara yake kupitia sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 na sera ya Afya ya Wazee ya mwaka 2003 imeweka mkazo katika kuwahudumia walio wanyonge na hususani Wazee ambao wana umri kuanzia miaka 60 na kuendelea kupatiwa matibabu bure bila ya malipo. Amesema kuwa katika kutekeleza sera na miongozo mbalimbali ambayo wamekuwa wakipata katika kuhudumia makundi hayo madogo wamekuwa na ushirikiano na tamisemi katika kuona ni namna gani ambayo wanaweza kutekeleza sera hiyo lakini pia na idara ya kuboresha afya ya ustawi wa jamii.

Amesema katika kuhakikisha hayo wamefanya zoezi la kutambua wazee katika halmashauri zote nchini na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila ya malipo ambapo hadi kkufikia septemba 2018 wamegundua uwepo wa wazee milioni moja laki nane na hamsini elfu na mia sita na ishirini na mbili huku wanaume wakiwa ni laki nane nane na arobaini na saba elfu mia tisa hamsini na tano na wanawake wakiwa ni milioni moja na elfu mbili mia sita sabini na saba wametambuliwa na kati yao laki saba hamsini na nne elfu mia sita sitini na saba wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo.

Aidha Dokta Jingu amesema kuwa serikali inaendelea kuhakikisha kuwa wazee wote ambao hawana uwezo wanapatiwa matibabu hayo lakini kumekuwapo na changamoto katika eneo hilo ambapo baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakiwanyanyapaawazee hao  na kwa kuliona hilo siku ya wazeenduniani kwa hapa nchini Tanzania ilivyoadhimishwa Kitaifa Mkoani Arusha Oktoba, 2008, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu alitoa maelekezo na maagizo kwa wale wote ambao wanawanyanyapaa wazee washughulikiwe. Amesema kuwa wao kama Viongozi wameahidi kulishughulikia suala hilo na kwamba endapo mzee yeyote atakayenyanyapailiwa katika kituo chochote kile cha afya au hospitali anapaswa kubainisha jina la mhusika wa kitendo hicho na atoe taarifa mahali husika na wizara itachukua hatua stahiki.

Dokta Jingu amebainisha kuwa wizara kupitia NHIF na CHIF wamekuwa wakijitahidi kuboresha huduma za afya kwa watu wote. "Hapa kuna changamoto kubwa ambapo kuna watu wanauwezo wa kupata huduma hizi lakini kwa njia moja ama nyingine wanakwepa ama hawajui umuhimu wa kujiunga na huduma hizo" aliongeza Dokta Jingu. Hata hivyo amewaomba viongozi wa dini waliohudhuria uzinduzi wa ripoti ya Viongozi wa dini kuhusu hifadhi ya jamii kwenye sekta ya afya kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko inayotoa huduma za matibabu. "Wakati NHIF inaanza baadhi ya watu waliona kuwa mfuko huo umelenga kuwachukulia wananchi fedha zao kumbe sio hivyo ndio maana tuliwaita watendaji na kuwaweka kitimoto lakini baada ya kupata vitambulisho hivyo na kuanza kutoa huduma faida imeonekana lakini kuna haja ya kufanya ulazima wa kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi wa serikali anajiunga na mfuko huo wa NHIF" aliongeza.

Dokta Jingu amesema kuwa kwa sasa inabidi kuwepo na kulazimisha watu kujiunga na NHIF kwani wengi wanakuwa wakipinga bila ya kujua wanachopinga na baadae wanapogundua faida zake wanajilaumu. Dokta Jingu amesema lengo la utafiti na mapendekezo yanayotoakana na utafiti sio kutoa mahitimisho isipokuwa ni kuchochea fikra ili tuzidi kufikiri zaidi na kushughulikia changamoto zilizopo.

08 October 2018, 14:37