Tafuta

Vatican News
Uongozi ni huduma inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu! Uongozi ni huduma inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu!  (ANSA)

Uongozi ni huduma inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu!

Uongozi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uongozi unapaswa kuwa ni jicho la huduma ya upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, ni sehemu ya Fumbo la Msalaba!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.

Ndugu zangu karibuni tena tutafakari pamoja neno la Mungu jumapili hii ya leo. Jumapili iliyopita tulitafakari juu ya hekima ya Mungu. Leo tunasikia habari juu ya tamaa ya madaraka. Kimsingi madaraka kwa yenyewe si dhambi. Katika Zab. 62:11 – tunasoma kuwa mamlaka ni mali yake Mungu. Kwa hakika tunafahamu kuwa Mungu ametuumba na ana lengo fulani na kila mmoja wetu. Hakuna aliyeumbwa kuzagaa zagaa tu kama daladala iliyokatika usukani!

Ni nini lakini maana ya kufaulu au kushindwa? Kwa watu wengi kama si wote na kama ionekanavyo pia kwa Yakobo na Yohani, ushindi ni kuwa juu ya kundi au mtu au watu. Ushindi ni mlinganisho wa mafanikio ya mmoja dhidi ya mwingine. Kivipi lakini? Ili kupata nini? Ili kuwa nani? Yakobo na Yohani hawakuomba kupatiwa mahali katika ufalme wa mbinguni, ila kukaa mkono wa kushoto na kulia kwake Kristo. Na katika mstari wa 38, Yesu anawaambia wazi, hamjui mliombalo. Kumbe hatuna budi kuwa makini sana katika maombi yetu kwa Mungu.

Kwa kifupi fundisho la Yesu kuhusu kufaulu latualika kutimiza mapenzi ya Mungu. Tunakuja ulimwenguni kutimiza mpango wa Mungu. Si kwamba Mungu ameshatuandalia mwisho wa kila mmoja wetu. Hapa ni uelewa potofu. Katika mpango huo wa Mungu sisi tunawekeza upande wetu. Mfano mzuri ni Mama Bikira Maria kama tuonavyo katika fundisho la Imani – Mkingiwa dhambi ya Asili. Mungu alipenda kutekeleza mpango wake wa ukombozi kwamba Maria awe Mama wa Mwanae. Akamwumba Bikira Maria, aliyeandaliwa kwa ajili ya tendo hilo. Hakuna mwingine katika mpango huo wa Mungu. Ndiyo maana Yesu anawaambia Yakobo na Yohani, kukaa mkono wangu wa kulia au wa kuume, si juu yangu, hutolewa kwa wale walioandaliwa.

Kwake Kristo, ushindi ni kutimiza na kukamilisha mapenzi yake Mungu.  Hii ina maana kuwa Mungu ana mpango nasi kwa kutuumba sisi (predestination and destination). Siyo kwamba tayari kila mmoja wetu ameshaandaliwa mwisho wake (determinism) kama wengi wanavyofiki au hata kuamini. Hapana. Ila lengo fulani la Mungu kwetu lipo, kwa kutuumba na ukamilifu wake wategemea ushirikiano wako na mapenzi yake Mungu. Mzazi humwandalia mtoto wake mazingira mazuri, pengine angependa mtoto wake awe mwalimu, nesi, padre, mtawa n.k. Ila kwa asilimia kubwa mzazi hawezi kumlazimisha mtoto wake kuwa hicho anachofikiri au kutaka. Mtoto anapewa nafasi kubwa ya kushiriki katika mpango huo wa mzazi. Hata Bikira Maria alishiriki katika upendeleo ule wa Mungu. Mungu alimpelekea malaika Gabrieli, naye akasema ndiyo.

Sote tunafahamu vizuri tamaa kubwa ya mamlaka/madaraka waliyo nayo wanadamu. Kwa yenyewe dhana ya madaraka/mamlaka si dhambi. Tunasoma katika maandiko, Mungu ni mwenye nguvu au ni nguvu na ukuu ni wake – Zab. 62:11. Nguvu hii ya Mungu inaonekana katika Agano Jipya lakini inapewa mtazamo tofauti na mawazo ya mwanadamu. Katika Agano Jipya, mahali fulani tunasoma kuwa pamoja na nguvu hizo zote, Yesu Kristo hakuona kuwa ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu – Fil. 2:7. Akageuza uwezo wake kuwa utumishi. Hapa ndipo wengi tunashindwa. Mwanadamu anapofikiria madaraka/mamlaka/kufaulu mtizamo wake unabadilika kabisa na kutaka kupata hilo hata kama ni kwa gharama ya namna gani.

Katika somo la kwanza tunasikia habari juu ya mtumishi asiye na nguvu, anayeteseka. Katika Agano Jipya tunaona aina mpya ya nguvu, nguvu ya msalaba. Mungu amewachagua wajinga kuwaaibisha wenye akili – 1Kor. 1:27. Katika sala ya Bikira Maria (magnificat), Maria anaimba, amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu – Lk. 1:52. Neno la Mungu siku ya leo lataka kutuambia nini?

Ndugu zangu, tamaa ya madaraka ni kubwa kuliko tunavyofikiri. Ipo mifano mingi pengine tunaifahamu au kuisikia na kuiona ambayo ni tishio kubwa kwa maisha yetu. Angalieni wanyama – mwenye nguvu ndiye mwenye nafasi ya kula majani mengi na mazuri, kula nyama kubwa na sehemu nzuri n.k. Magomvi kati yetu juu ya ubabe, utajiri, utawala, katika kuendesha mipango ya familia, jumuiya, serikali n.k inaathirika na aina hii ya mitizamo.

Ndugu zangu, akili zetu, mioyo yetu, utashi wetu huwa vikao vyetu, viti vyetu tunapokalia na kukalia wengine, dhidi ya wengine. Mara nyingi tungependa utashi wetu ufanye kazi kwa vyo vyote vile hata kama mara nyingi haionekani katika matendo yetu. Kutokufanya jambo fulani jema hudhihirisha jambo hilo. Migongano mikubwa hutokea pale mmoja asipokuwa tayari kuacha nafasi yake ili kingine kizuri zaidi kifanyike. Kina Yakobo na Yohani walitaka wao wapate, wengine shauri yao. Katika Injili tunaona tamaa ya madaraka na nguvu ya kutawala au kuwa juu ya wengine au kuwa na nafasi ya upendeleo inabatilishwa na uwepo wa Yesu. Anaionesha katika dhana ya utumishi. Utumishi kwa wengine na si juu ya wengine. Mamlaka huendana na madaraka ila utumishi huendana na heshima. Yesu anasema wazi alikuwa ana mamlaka ya kuagiza kundi la malaika kuangamiza adui zake – Mt. 26:53,lakini aliamua kutumia nguvu ya sala. Na kwa njia hii akaupata ushindi.

Utumishi usieleweke kama kusalimu amri ua ukimya au ujinga. Au kutenda jambo jema kama ujinga kama wengi wetu tunavyofikiri. Katika Rum. 12:21 tunasoma – usishindwe na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema. Pia mtume Paulo katika 1Kor. 4 ... anaongea kuhusu huduma ya mitume – kwamba mitume wahesabiwe na watu kama watumishi wa Kristo na watunzaji wa mafumbo ya Mungu. Na hao watumishi wajulikane kuwa waaminifu. Hii ndiyo maana halisi ya madaraka kadiri ya fundisho la Kristo. Nasi tukafanye hivyo hivyo.

Tumsifu Yesu Kristo.

18 October 2018, 17:02