Tafuta

Padre Charles Kitima: Tafiti na takwimu sahihi zisaidie kusongesha mbele maendeleo endelevu ya binadamu! Padre Charles Kitima: Tafiti na takwimu sahihi zisaidie kusongesha mbele maendeleo endelevu ya binadamu! 

Padre Kitima: Tafiti na takwimu sahihi zisaidie maboresho ya maendeleo endelevu!

Tafiti makini pamoja na takwimu sahihi, zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu katika jamii. Wito huo umetolewa hivi karibuni na Padre Charles Kitima Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kwa wadau wa tasnia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania.

Na Rodrick Minja na Julieth Muunga, Dar Es Salaam

Wadau wa tasnia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii nchini Tanzania wametakiwa kufanya utafiti wa kutosha katika habari wanazoandika kwa kutumia takwimu sahihi, ili kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu katika jamii. Wito huo umetolewa na Padre Charles Kitima Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, wakati akifungua mafunzo ya Siku kumi ya Utafiti kwa Vyombo vya Habari vya Kijamii yanayofanyika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Padre Kitima   amesema   kuwa   mwanahabari   mzuri na makini   ni   yule anayefanya   utafiti   wa   kina kabla ya kuchapisha au kutangaza jambo lolote. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwamba kwa kupitia kazi na taaluma zao kwamba, mafunzo   hayo yatawasaidia   kuimarisha uzoefu na maarifa na hivyo kusongesha mbele juhudi za kuleta maendeleo kwa Kanisa na jamii ya watanzania katika ujumla wake.

“Wanahabari wengi wa vyombo vya habari vya Kanisa wamekuwa hawajui kufanya utatifi na hawatumii takwimu sahihi wakati wanaandika habari kwenye vyombo vyao vya habari, hivyo mafunzo haya nataka yawasaidie ili muweze kuandika habari zenye utafiti na takwimu sahihi ili kulisaidia Kanisa na waamini wake” alisema. Amewataka kuhakikisha kwamba, wanatumia   vizuri   elimu wanayoipata ili waimwilishe katika mchakato mzima wa uinjilishaji   na hutoaji wa huduma katika jamii lakini zaidi wahakikishe kwamba, wanasaidia kupitia vyombo vyao vya habari kujenga umoja, amani, upendo na mshikamano wa watu wa Mungu duniani. 

Padre Kitima amesema kuwa washiriki wanapaswa kutumia fursa hiyo ya mafunzo hayo vema ili kuhabarisha vema taifa la Mungu na kuwapatia mwanga kwa vile ambavyo hawavijui. “Mwaka huu Kanisa linaadhimisha kilele cha miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, tumieni vyombo venu vya habari kuhakiksiha kuwa mnahabarisha jamii ni nini kimefanyika tokea wamisionari wa kwanza kufika hapa nchini Tanzania na ni mafanikio mangapi yamepatikana tangu wamisionari hao wafike Tanzania” aliongeza!

Alisema kuwa tangu mmisionari wa kwanza kufika Tanzania Bara na kuanza uinjilishaji wananchi wengi wamepata mafanikio katika nyanja mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, maji, kilimo, ustawi na huduma nyinginezo kwa ajili ya watu mahalia! Aidha ameongeza kuwa wakati huu kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania sambamba na uanzishwaji wa Elimu ya kishule watambue kuwa wamisionari wa kwanza walitumia vitabu   na   magazeti   ambayo   yalikuwa   yakifika   vijijini   zaidi   hivyo wahakikishe wanaandika habari za kina ili wasaidie watu kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi, maadui wakuu wa taifa la Tanzania na hatimaye kujenga uadilifu na uwajibikaji katika jamii ya watanzania.

Awali akimkaribisha Padre Kitima kufungua mafunzo hayo, Dada Meclina Kasasi, Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi Endelevu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. alisema kuwa mafunzo haya yatawasaidia washiriki kuandika habari zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuhakikisha kuwa habari zinazoandikwa zinakuwa na takwimu sahihi, kwa ajili ya kuelimisha umma. “Washiriki ni matumiani yangu kuwa mtakayofundishwa mtayafanyia kazi ili kutoa mabadiliko chanya kwenye vituo vyenu vya kazi” aliongeza Dada Kasasi. Alisema kuwa lengo la mafunzo haya ni kujua wasikilizaji wanataka nini na kwa wakati gani hivyo ni jukumu la kila kituo kutekeleza kwa vitendo mawazo ya wasikilizaji wao. Pia Dada Kisasi aliwataka waandishi wanaoshiriki kuhakikisha hawatumii takwimu ambazo ni za kutengenezwa na sio zilizokusanywa kwa weledi na utaalamu  wa kutosha.

Akichangia hoja mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Matangazo kutoka Kituo cha Radio Mbiu Jimbo Katoliki Bukoba, Padre Kagashe Katunzi amesema ameyafurahia sana mafunzo haya na anawashukuru wawezeshaji wake maana yanawasaidia kung'amua masuala mbalimbali kuhusiana na tafiti za wasikilizaji kwani watajua wasikilizaji wanataka nini kitu ambacho kitawasaidia kuboresha maudhui  ya vipindi vya Radio na Televisheni na namna ya kuviwasilisha kwa wakati husika katika jamii inayowazunguka  huku akiongeza pia ni vyema mafunzo kama haya yawe yanatolewa mara kwa mara kwa wanahabari ili yawasaidie katika kukuza na kuimarisha taaluma yao.

Mafunzo hayo ya siku kumi yanawashirikisha wanahabari wapatao 25 kutoka: Radio Mbiu Kagera, Radio Huruma Tanga, Radio Ukweli Morogoro, Radio Chemchem Sumbawanga, Radio Mwangaza Dodoma, Radio Tumaini na Televisheni Tumaini Dar es Salaam, Radio Sauti Mwanza, Radio Faraja Shinyanga, Radio Habari Njema Mbulu, na Radio Maria Tanzania, Dar es Salaam. Hivi ni vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania.

Tasnia ya mawasiliano

 

11 October 2018, 10:15