Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anapembua mchango wa Mtakatifu Paulo VI katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika! Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anapembua mchango wa Mtakatifu Paulo VI katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika!  (Vatican Media)

Mchango wa Mt. Paulo VI katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika!

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’chi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam , anasema, Mwenyezi Mungu ni mwema na wema wake unajidhihirisha kwa namna mbali mbali kwa jinsi anavyolibariki na kulitunuku Kanisa lake. Katika karne ya 20, familia ya Mungu imeshuhudia uwepo wa Mababa watakatifu makini, wakarimu, waelewa na wenye uthubutu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ya kuwatangaza watakatifu wapya saba, Jumapili tarehe 14 Oktoba 2018 alisema, Kristo Yesu anawaalika waamini kurejea tena katika kisima cha furaha, kwa kukutana naye; kwa kufanya maamuzi thabiti, kiasi hata cha kuthubutu kumfuasa bila ya kujibakiza kama walivyofanya watakatifu katika maisha na utume wao!

Ndivyo alivyofanya Mtakatifu Paulo VI kwa kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika majadiliano, huduma kwa maskini pamoja na kuwa na mwono mpana zaidi katika maisha na utume wa Kanisa hata pale ambapo hakueleweka sana. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, Mtakatifu Paulo VI ameshuhudia uzuri na furaha ya kumfuasa Kristo Yesu bila ya kujibakiza. Ni Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, aliyeonesha moyo wa uchaji wa Mungu na hivyo kujitahidi kuishi kitakatifu wito kwa watu wote.

Mtakatifu Paulo VI, alizaliwa kunako mwaka 1897 huko Concesio, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 29 Mei 1920 na hatimaye, kuteuliwa na kuwekwa wakfu kama Askofu mwaka 1954. Baba Mtakatifu Francisko, amemtangaza Paulo VI kuwa Mtakatifu, tarehe 14 Oktoba 2018 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Sinodi ni chombo kilichoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1965 kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwashirikisha watu wa Mungu katika mchakato wa kupanga, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, dhana ambayo Baba Mtakatifu anapenda kulihamasisha Kanisa kwa nyakati hizi, kuivalia njuga kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’chi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam , anasema, Mwenyezi Mungu ni mwema na wema wake unajidhihirisha kwa namna mbali mbali kwa jinsi anavyolibariki na kulitunuku Kanisa lake. Katika karne ya 20, familia ya Mungu imeshuhudia uwepo wa Mababa watakatifu makini, wakarimu, waelewa na wenye uthubutu ambao wameliongoza Kanisa katika vipindi vigumu na tete. Baadhi yao ni Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Yohane Paulo II, uwepo wao unawatia waamini nguvu na hamasa ya kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Papa Paulo VI ni Baba wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kiongozi mnyofu, mchamungu na mpenda Kanisa. Ameliongoza Kanisa katika kipindi cha misukosuko na hali tete kutokana na mabadiliko na changamoto zilizotolewa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linamshukuru na kumpongeza kwa: Imani na mafundisho yake, kielelezo makini cha utajiri wa Roho Mtakatifu kupitia Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Lakini, Kanisa Barani Afrika linamkumbuka kwa namna ya pekee kabisa, kuwa ni muasisi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, yaani SECAM, iliyoanzishwa rasmi wakati wa hija yake ya kitume nchini Uganda kunako mwaka 1969.

Mtakatifu Paulo VI alihimiza kuundwa kwa SECAM ili kiwe ni chombo cha: umoja, upendo na mshikamano wa familia ya Mungu Barani Afrika katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, sehemu muhimu sana ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Alipania kulisindikiza Kanisa Barani Afrika katika hija ya maisha na utume wake, ili liweze kujitokeza kama Kanisa linaloinjilisha na kuinjilishwa. Kumbe, familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kumuenzi Mtakatifu Paulo VI kwa kuenzi malengo mazuri na matakatifu yaliyopelekea kuundwa kwa SECAM.

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’chi anasikitika kusema kwamba, katika historia ya SECAM, kumekuwepo na hali ya kuyumba katika maisha na utume wake; kwa kushindwa kutekeleza dhamana na majukunu yake barabara. Hii inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya wadau kwa kiasi kikubwa walishindwa kutimiza pia wajibu wao. Daima inampendeza Mwenyezi Mungu, ikiwa kama familia ya Mungu itajengeka na kuimarika katika misingi ya upendo, umoja na mshikamano. Vyombo vya umoja na mshikamano wa Kanisa vinapaswa kudumishwa na kuimarishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Mtakatifu Paulo VI alijihusisha sana na mchakato wa kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha ushuhuda wa upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Alikazia imani, maadili na utu wema; kwa kuhubiri na kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Alipenda kuliona Kanisa linajikita zaidi katika katekesi makini na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Haya bado ni mafundisho makini na endelevu hata kwa Kanisa mamboleo. Ni mafundisho yaliyokabiliwa na upinzani kutoka ndani na nje ya Kanisa.

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’chi anakaza kusema, ni vyema kabla ya kupinga mafundisho ya viongozi wa Kanisa, watu wafanye tafakari ya kina, wachambue hoja kwa misingi na vigezo sahihi na hatimaye, kuyafanyia kazi kadiri inavyompendeza Mwenyezi Mungu. Mafundisho ya Mtakatifu Paulo VI ni dhahiri, sahihi na rejea makini kwa Kanisa mamboleo. Sasa ni wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza maisha, mafundisho na vipaumbele vya Mtakatifu Paulo VI ili kuweza kuvimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusoma alama za nyakati!

Papa Paulo VI na SECAM
15 October 2018, 08:36