Tafuta

Vatican News
Mtakatifu Gaspar del Bufalo alijitahidi kusikiliza na kujibu kilio cha damu kwa watu wa nyakati zake! Mtakatifu Gaspar del Bufalo alijitahidi kusikiliza na kujibu kilio cha damu kwa watu wa nyakati zake!  (Vatican Media)

Mtakatifu Gaspar del Bufalo, mfano bora wa uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha!

Mtakatifu Gaspar del Bufalo tangu mwanzo aliamua kuwa mmisionari na akashika msimamo huu hadi kuufikia utakatifu. Gaspar alifaulu kumwiga Kristo kwa kulinganisha uhodari wa kibinadamu na neema ya Mungu. Wito wake uliojitokeza tangu kuzaliwa kwake uliimarishwa na kukomazwa hadi upeo wa utakatifu kwa njia ya mazingira na watu aliokutana nayo.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Roma

Utangulizi: Mtakatifu Gaspari Del Bufalo, mwanzilishi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. (1786-1837). Ndugu mpendwa ninakukaribisha katika kipindi hiki ili kuweza kuyatambua, japo kwa kifupi, maisha na utume wa Mt. Gaspari katika kanisa na katika shirika. Kwa kawaida sikukuu za watakatifu katika Kanisa huwa tunazisherehekea au siku ya kuaga kwao dunia, yaani siku wanayozaliwa mbinguni au tarehe ya kutangazwa kwao watakatifu n amara chache siku ya kuzaliwa kwao duniani.  Hata hivyo sikukuu ya Mt. Gaspari huwa tunaisherehekea kila mwaka tarehe 21 mwezi Oktoba kila mwaka. Tarehe hii haina uhusiano wowote na siku ya kuzaliwa kwake duniani wala mbinguni maana aliaga dunia tarehe 28 Desemba 1837 na wala haina uhusiano na siku ya kutangazwa kwake Mtakatifu maana alitangazwa mtakatifu tarehe 12 mwezi Juni 1954. Tarehe hii ilipangwa baada ya makubaliano hasa kuondoa mwingiliano wa sikukuu au sherehe nyingine katika Kanisa.

Mfano tarehe 28 Desemba ni sikukuu ya kanisa ya watoto mashahidi ukiachilia mbali kwamba tarehe 6 Januari ni Sherehe ya Epifania au Tokeo la Bwana. Pia tarehe 12 Juni mara kadhaa huingiliana na sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kutokana na heshima aliyonayo Mt. Gaspari katika Kanisa la Roma, kanisa hilo kwa miaka kadhaa lilikuwa likiadhimisha sikukuu ya Mt. Gaspari tarehe 4 Januari. Kutokana na makubaliano ndani ya shirika ya kuadhimisha sikukuu ya Mt. Gaspari siku ya tarehe 21 Oktoba nalo Kanisa la Roma likakubali kwamba tarehe hiyo iwe sikukuu ya

Mt. Gaspari alizaliwa Roma tarehe 6/1/1786. Mama yake aliitwa Anunciata na Baba yake alitwa Antonio. Alikuwa na kaka yake aliyeitwa Luigi. Kutokana na ukweli kwamba alizaliwa akiwa na afya dhaifu wazazi wake waliogopa kwamba angeweza kuwa mhanga wa ugonjwa wa kifua kikuu. Kwahiyo siku iliyofuata, yaani tarehe 7 Januari alibatizwa kwa akipewa majina yote matatu ya Mamajusi toka mashariki ya mbali, yaani Gaspari, Melkior na Baltazari.

Wazazi wa Mt. Gaspari walikuwa ni wakristu wenye imani thabiti wakiishi na kuyashika vema mafundisho ya kanisa. Kila siku walihudhuria misa takatifu katika kanisa liitwalo Kanisa la Yesu lililopo karibu na mahali walipokuwa wakiishi. Katika kanisa hili kuna masalia ya mkono wa Mt. Fransisko Ksaveri ambaye alikuwa ni mmisionari maarufu aliyefanya kazi kubwa ya uinjilishaji huko India. Kutokana na afya dhaifu aliyokuwa nayo Gaspari mara nyingi aliugua. Akiwa na miezi 20 tu alishambuliwa vibaya na ugonjwa wa ndui (small pox) na alikuwa katika hatari ya kupata upofu wa macho. Madaktari walikiri kuwa hawakuwa na uwezo wa kuutibu ugonjwa kwa njia ya kisayansi.

Mama yake Gaspari alimweka mwanaye chini ya maombezi ya Mtakatifu Fransisko Xsaveri ili aweze kupona. Haikuchukua muda, mtoto Gaspari alipona. Baada ya Gaspari kupata ufahamu, mama yake alimsimulia juu ya kuponywa kwake kwa muujiza kupitia maombezi ya Mt. Francisko Xsaveri. Tangu alipotambua hilo, Gaspari akajenga upendo wa pekee na ibada kubwa kwa mtakatifu huyu kwa maisha yake yote. Kila mara alipopiga magoti na kusali mbele ya altare ya Mtakatifu huyu, alisikia mvuto wa pekee wa kuwa naye mtakatifu. Alipoanzisha shirika la wamisionari wa Damu Takatifu, Mt. Gaspari aliliweka chini ya usimamizi wake na akataka Mt. Fransis Ksaveri awe mfano wa umisionari kwa wanashirika wote.

Maisha na utakatifu wa Gaspari una msingi wake madhubuti katika malezi aliyoyapata ndani wa familiya yake. Aliwaheshimu na kuwasilikiza wazazi wake na kutoka kwao, hasa kwa mama yake, alijifunza mambo mengi yaliyojenga utu na dhamiri yake kama mwanadamu. Wazazi wake hawakulenga kumpa elimu ya kidunia tu bali hasa mafundisho yenye kuijenga imani yake ya kikristu. Mama yake ndiye alikuwa katekista mkuu. Mama huyu aliapa mbele ya Mungu kufanya analoweza ili kumlea na kumuongoza kuwa mkristu wa kweli. Alimfundisha sala na mafundisho mbalimbali ya msingi katika imani ya kikristu. Mambo yote ya imani aliyoyaishi Gaspari yalikuwa na chimbuko lake katika malezi toka kwa wazazi wake.

Tangu akiwa mtoto Mama alimpeleka Gaspari katika misa takatifu na alikuwa na tabia ya kumwongoza kwenye altare yenye Yesu Msulibiwa. Mtoto Gaspari alionekana kuingia katika tafakari ya kina juu ya jambo hilo kinyume cha umri wake. Mara kadhaa alibaki akitafakari kanisani na mama aliwajibika kumwondoa kwa nguvu. Wakati wa misa, Gaspari alikuwa na umakini wa pekee n amara nyingi alionekana kupiga magoti mbele ya Yesu Ekaristi. Siku alipoungama kwa mara yake ya kwanza, mtoto Gaspari aliweza kumshangaza muungamishaji wake kwa jinsi alivyokuwa na dhamiri ya pekee mpaka kumfanya kusikia uchungu mkubwa kutokana na dhambi alizofanya na kwa kushindwa kutimiza kile ambacho alipaswa kufanya.

Mama yake alipoziona hizi alama kwa mtoto wake, alimshukuru Mungu kwa zawadi ya mtoto huyu na bila shaka alijiuliza nafsini mwake kwamba atakuwa mtu wa namna gani atakapokuwa mtu mzima, kama jinsi ambavyo watu walijiuliza juu ya maneno na matendo aliyoyafanya Yesu akiwa mdogo. Mama yake alikubali kushiriki kikamilifu n aule mpango ambao Mungu alimpangia mwanaye.

Tangu akiwa mdogo: Gaspari tangu akiwa mdogo alisikia ndani yake sauti ikimwita kama jinsi sauti ya Mungu ilivyomwita Samweli katika hekalu. Alipompokea Yesu Ekaristi kwa mara ya kwanza, hamu hiyo iliongezeka na akaamua kujikabidhi kwa Mungu. Mjomba wake ambaye alikuwa ni padre wa shirika la msalaba mtakatifu naye alikuwa ni chachu katika kuifuata njia hiyo. Wakati ulipofika alijiunga na seminari ya jimbo na Roma akiwa na umri wa miaka 11 tu. Alikuwa na bidii kubwa katika sala, masomo na malezi yote aliyazingatia sana na alikuwa ni mfano wa kuigwa na wengine. Vazi la kanzu alilovaa kwake ilikuwa ni ishara na wajibu wa kuishi utakatifu. Alikumbwa na majaribu na magumu mengi katika safari yake ya wito ikiwa ni pamoja na matatizo ya kifamilya. Katika hayo yote alijifunza kusali, “mapenzi yako yatimizwe”.

Maisha yake kama Padre: Tarehe 12 Machi 1808, Gaspari alipata daraja la ushemasi. Hatimaye tarehe 31 Julai mwaka huohuo wa 1808, Gaspari alipewa daraja la upadre akiwa ni padre wa jimbo la Roma. Je, Gaspari alikuwa padre wa namna gani? Alikuwa na upendo mkubwa sana kwa Mungu na alipenda kusali na kutafakari mbele ya Yesu Ekaristi. Jambo hili hakulianza akiwa padre bali tangu alipokuwa mdogo. Pamoja na tafakari mbele ya Yesu Ekaristi, alitafakari sana juu ya safari nzima ya mateso ya Yesu na juu ya Damu iliyomwagika msalabani kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Tangu akiwa mdogo, tafakari juu ya mateso ya Yesu ilikuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Alisoma na kuyaiga maisha ya watakatifu mbalimbali wa Kanisa. Mbali na Mt. Fransisko Ksaveri alisoma vitabu mbalimbali juu ya maisha ya watakatifu Aloys Gonzaga, Mt. Alphonsus Maria de Ligouri, Kumuiga Kristo na alikuwa na ibada ya pekee kwa Mama Bikira Maria. Alikuwa na huruma na upendo wa pekee kwa masikini. Aliwasaidia kadiri alivyoweza. Jambo hili alilifanya tangu akiwa mdogo na kila alipolifanya alisema na kwa ajili ya kumpa heshima Bikira Maria. Mara nyingi alikubali kujinyima chakula alichopaswa kula ili awape masikini waliokuja karibu na nyumba yao. Wakati mwingine mama yake alimkaripia juu ya kujinyima huko lakini yeye alijibu akisema kwamba wale masikini wana njaa zaidi ya yeye. Hakika Gaspari alikuwa na huruma kubwa kwa masikini.

Tangu mwanzo akiwa mdogo alionesha moyo mwema na wenye ukarimu kwa wenye shida kinyume cha watoto wengi ambao huonesha tabia ya ubinafsi katika kuwagawuia wengine mambo yao. Sambamba na hilo mara nyingi aliwatembelea wagonjwa katika hospitali mbalimbali. Tangu akiwa mdogo aliguswa na shida za watu. Aliutumia muda huo pia kujifunza juu ya mahangaiko ya watu na alitafuta kila njia kuwasaidia. Katika Kanisa la Mt. Galla kulikuwa na kituo kikubwa kwa ajili ya kuwasaidia masikini na wagonjwa ambapo yeye na mapadre wengine walitoa huduma. Katika matendo hayo ya huruma, Gaspari alifanikiwa kuuishi ukristo kwa kuitikia neno la Yesu linalosema kuwa kila mlilowatendea ndugu zangu hawa wadogo mlinitendea mimi na kila msilowatendea ndugu zangu hawa wadogo hamkunitendea mimi.

Kama Padre, Gaspari alikuwa na upendo mkubwa kwa Kanisa na alibaki mwaminifu kwa Kanisa daima. Mwaka ambao alipadirishwa ndiyo mwaka ambapo Kanisa lilipata matatizo na mateso makubwa chini ya utawala wa Napoleone wa Ufaransa aliyevamia Roma na miji mingine ya Italia mwaka 1808 akitaka Kanisa na uongozi wake kutii mamlaka yake. Maaskari wa Baba Mtakatifu walitekwa na Baba Mt. Pius wa VII akatiwa gerezani. Makadinari na maaskofu wengi wakafukuzwa Roma. Watawa nao hawakusalimika, walifukuzwa toka kwenye nyumba zao na mali zao zikataifishwa. Napoleone alipunguza alipunguza idadi ya parokia na aliruhusu idadi ndogo tu ya waseminari katika seminari za majimbo. Shule ziliendeshwa kijeshi na vijana walipewa mafunzo ya kijeshi. Je, nini kilitokea baada ya hapo? Nakukaribisha katika kipindi kijacho ili kuona ni namna gani Mtakatifu alikabiliana na hali hiyo. 

Mtakatifu Gaspar

 

20 October 2018, 14:44