Tafuta

Vatican News
Katika kuelezea miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Kardinali Pengo anasisitiza juu ya  vijana kupewa elimu,lakini kwanza watambue ukuu wa Mungu Katika kuelezea miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Kardinali Pengo anasisitiza juu ya vijana kupewa elimu,lakini kwanza watambue ukuu wa Mungu 

Kard. Pengo:tuombe Mungu azidi kuteua watu wake katika uinjilishaji!

Kardinali Pengo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar Es Salaam Tanzania akizungumza na waandishi wa habari amebainisha kuwa katika kilele cha miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara, Injili ya Kristo haikuishia Bagamoyo tu bali imeenea kila kona ya Tanzania na nje ya Tanzania

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, amewataka wakristo kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili aendelee kuteua watu ambao wataendeleza shughuli za uinjilishaji kwa siku za mbeleni. Kardinali Pengo ameyasema hayo, Jumatano tarehe 17 Oktoba 2018 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Jimbo Kuu  Dar es salaam wakati akizungumzia juu ya kilele cha miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara.

Vijana wapewe elimu, lakini watambue ukuu wa Mungu kwanza

Kardinali Pengo amesema kuwa pamoja na mambo mengine kama vile vijana kupewa elimu zaidi lakini neno lake la mwisho kwao ni kile kitendo cha kutambua kuwa mwenyezi mungu ndiye mteuzi wa wahudumu ndani ya Kanisa na hii anasadiki na sio kwa Kanisa katoliki tu  au wakristo tu lakini ni mahali popote pale ambapo kiongozi wa dini wa kufaa anapatikana. Akiendelea na ufafanuzi wake amesema kuwa, katika upatikanaji wa viongozi wa kuwaongoza kondoo wa mwenyezi mungu anapopatikana tunapaswa kutambua kuwa upo mkono wa mwenyezi mungu, na wale  kwanza wanaoitwa wanapaswa kuutambua, lakini na wale wengine wawasaidie wale wanaoitwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli hiyo muhimu ya utume ndani ya Kanisa la mwenyezi mungu.

Migogoro ya Kanisa na kutafuta amani

Aidha akijibu maswali ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo, Kardinali Pengo amesema migogoro katika  Kanisa ni jambo linalosikitisha na halipaswi kuwa hivyo, na kwa maana hiyo kama watu wanatafuta Amani, hilo ni jambo la muhimu kushirikiana mpaka kufikia malengo husika. Akiendelea ameongeza kusema kuwa, wakristo wote wanaamini ya kuwa licha ya Kanisa katoliki lakini pia vyombo vyote  au makundi yote ya kidini wanatoa vitu kama wahudumu, sio watu ambao wanajipeleka bali ni watu walioteuliwa na mwenyezi mungu. Na katika kzungumza juu ya vikwazo ambavyo Kanisa Katoliki limekumbana navyo kwa kipindi cha miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara, Kardinali Pengo amesema kuwa, vikwazo vya kibinadamu ni vya kawaida na ukijaribu kuviorodhesha vyote inakuwa ni vigumu kwani vipo vingi maana, kuna hata sehemu ambazo wamisionari walipofika hawakuweza kupokelewa kwa urahisi.

Kumbukumbu ya vita vya majimaji

Akifafanua zaidi juu ya vikwazo ametoa mfano wakati ule wa  vita vya majimaji na kwamba wamisionari pamoja na kwenda kwa ajili ya kutoa huduma ya habari njema ya Injili, lakini walikutana na watu ambao hawakuelewa kusudi lao au kwa makusudi yao, kwa maana hiyo kwa makusudi mazima wapo watu wa kwanza walipeleka injili kama Askofu Kasiani Spisi aliyeuwawa huko Mikukuyumbu karibu na Liwale. Watu hao  hawakuelewa au ama kwa makusudi shughuli za kimisionari kwani suala la matukio kama hayo hayakutokea Tanzania peka yake , bali katika ulimwengu mzima.

Huduma zitolewazo katika Kanisa

Kardinali Pengo akizungumzia juu ya huduma zinazotolewa na Kanisa katoliki amesema kuwa, kwa dhati limetoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile, afya, maji, elimu  na huduma nyinginezo kwani katika kile kipindi  hicho, kuna sehemu ambazo kulikuwa na hospitali za Kanisa tu, pamoja na hayo, amebinisha kuwa,  kwa sasa Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma hizo kwa kiwango kikubwa zaidi ya hapo awali.

Uhuru kidini nchini Tanzania

Akiendelea na ufafanuzi zaidi kuhusu suala la uhuru wa  dini na kuabudu, Kardinali Pengo amesema kuwa watanzania wanao uhuru wa kuabudu na ssiyo kwamba  Kanisa katoliki libaki lenyewe katika  kuendesha ibada zake bali, ibada hizo zinafanyika kulingana na madhehebu na dini katika utofauti wake:“ Dini kama dini walau hapa mashariki na  hatugombani kama dini, wanaweza wakawepo watu wachache wewe ni mkristo, mwislamu au watu wa dini tofauti na mwelekeo tofauti na wengine lakini huwezi ukasema hii inatokana na dini fulani ndiyo inaleta wasiwasi katika maisha ya amani ya Taifa letu”. Kutokana na hili amethibitisha kuwa Injili inafanya kazi yake  na shughuli za  uinjilishaji zinaendelea katika mfumo wa kibinadamu.

Wadau wa amani ni pamoja na serikali  na madhehebu ya dini na  watanzania katika ujumla wao!

Kwa upande wa suala la amani Kardinali Pengo amesema kuwa “Injili haipo peke yake hapa katika sehemu yetu ya Tanzania Bara na sehemu nyingine na nchi jirani katika wadau wa amani, na maelewano kati ya watu”. Sababu za kutokuwa na chokochoko haiwezi kuonekana kwamba ni  kushindwa kwa uinjilishaji peke yake kwa sababu wadau wa amani ni pamoja na serikali, madhehebu ya dini, watu wa dini, kwani hakuna dini au serikali inayotaka watu wake waendelee kuteseka na kukosa amani. Akisisitiza zaidi amesema: “Kamwe hatuwezi kugombania amani tunategemea watu wapige hatua wasonge mbele kwa sababu amani ipo na inaendelea kulindwa kwa nguvu zote”.

Na katika kuhitimisha hotuba yake kwa waandishi wa habari, Kardinali Pengo amebainisha kuwa katika kipindi cha kilele cha miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara ikumbukwe kuwa Injili ya Yesu Kristo haikuishia Bagamoyo tu bali imeenea kila kona ya Tanzania na hadi kuwafikia wakristo wote  kila kona ya Tanzania na nje ya Tanzania.

KARD. PENGO
17 October 2018, 15:05