Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia. Papa Francisko anawaalika waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia.  (Vatican Media)

Familia ya Mzee Peter Msaga: Shuhuda wa Injili ya ndoa na familia

Hivi karibuni, Mzee Peter Msaga na Mama Agnes Ingram, kutoka Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, Tanzania, wameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu walipofunga ndoa kunako tarehe 26 Oktoba 1958 na kubahatika kupata watoto 11 katika maisha yao. Tukio hili lilipambwa kwa Ibada ya Misa iliyoongozwa na Askofu Gervas Nyaisonga.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Baba Mtakatifu Francisko anasema familia ni hospitali iliyoko karibu sana inayoweza kutoa huduma ya kwanza yenye mvuto na mashiko. Familia ni kiini cha upendo, umoja na ukarimu. Familia ni shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, familia ni makazi maalum ya wazee na wagonjwa. Familia ina tunu na changamoto zake. Kumbe, wazazi wanayo dhamana kubwa kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, ili kujenga na kudumisha familia ya Mungu inayowajibika.

Hivi karibuni, Mzee Peter Msaga na Mama Agnes Ingram, kutoka Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, Tanzania, wameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu walipofunga ndoa kunako tarehe 26 Oktoba 1958 na kubahatika kupata watoto 11 katika maisha yao. Tukio hili lilipambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya familia inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu na kwa namna ya pekee katika familia ya Mzee Peter Msaga. Usione ajabu tukio hili lilikwenda sanjari na maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 21- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”.

Maandalizi haya yameongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi, hata kama wataziba masikio yao, lakini watambue kwamba, kwa hakika wamehubiriwa Injili ya familia. Mzee Peter Msaga na Mama Agnes Ingram wanasema, siri ya mafanikio na udumifu katika maisha yao ya ndoa na familia hadi wakati huu ni uchaji wa Mungu na Ibada; sadaka na majitoleo kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Katika maisha yake, Mzee Peter Msaga ameshirikiana kwa karibu sana na wamisionari wa Consolata, Jimbo Katoliki Iringa, Wakapuchini, Jimbo Katoliki Dodoma na hatimaye, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Jimbo Katoliki Singida ambako ametumia muda wake mwingi kwa kazi ya useremala pamoja na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ujuzi na maarifa. Mzee Msaga ni kati ya waasisi wa Chuo cha  Ufundi RC. Manyoni, kilichoanzishwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania, ili kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na mazingira yao na hivyo kuitengeneza Kanda ya Kati kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Mama Agnes Ingram katika maisha yake kama Mama wa nyumbani, amekuwa ni mhimili mkubwa wa malezi na tunza ya familia wakati Mzee Msaga alipokuwa anachakarika usiku na mchana kuboresha maisha ya familia yake. Mama Agnes amekuwa mstari wa mbele katika utume wa Wanawake Wakatoliki, daima akisukumwa na upendo wa Mungu, unaowawajibisha. Mama huyu ana ibada ya pekee kabisa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake bila kusahau Ibada kwa Bikira Maria, shule ya upendo kwa Mungu na jirani.

Bikira Maria amekuwa ni faraja na kimbilio la familia ya Mzee Peter Msaga wakati wa raha na shida! Huu ndio ushuhuda wa Injili ya familia unaotangazwa na familia hii, wakati huu wanapomshukuru Mungu kwa kuwakirimia miaka 60 ya maisha ya ndoa na familia, wakiwa bado wameshibana, kama siku ile ya kwanza, walipofunga ndoa kwenye Parokia ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Jimbo Katoliki la Iringa kunako mwaka 1958.

Familia ya Mzee Msaga

 

 

10 October 2018, 09:34