Tafuta

Vatican News
Huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa.  (ANSA)

Mkutano mkuu wa IMBISA kuhusu huduma ya upendo!

Injili ya huduma ya upendo ni sumaku inayomuunganisha Mungu na binadamu, changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amelizawadia Kanisa Nyaraka kuu tatu ambazo kimsingi ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika mshikamano wa huruma, upendo na haki jamii. Hii ni sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa pamoja na kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Kanisa ni chombo muhimu sana cha huduma mintarafu mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili!

Injili ya huduma ya upendo ni sumaku inayomuunganisha Mungu na binadamu, changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Leo hii, maskini wanaonekana kuwa kero kwa Jumuiya ya Kimataifa, watu wasiokuwa na utu wanaochezewa kama “mpira wa danadana” na kukandamizwa chini kama “soli ya kiatu! Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, “Caritas Africa” kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi tarehe 3 Novemba 2018 wanafanya mkutano wa kimataifa unaoziunganisha nchi wanachama wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA.

Mkutano huu unaadhimishwa huko Pretoria, Afrika ya Kusini. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkutano wa Caritas Africa ulioadhimishwa kunako mwaka 2012 na kufuatiwa na mkutano wa Dakar, Senegal uliofayika mwaka 2017, ili maazimio haya sasa yaanze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya familia ya Mungu katika nchi za IMBISA. Huu ni muda muafaka wa kutafakari zaidi Mafundisho Jamii ya Kanisa na hatimaye, kuanza kuyafanyia kazi, kama sehemu ya ushuhuda wa Injili ya upendo, inayomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Nchi za IMBISA zinakabiliwa na changamoto kubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kidini na kikabila! Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaopelekea watu wengi kutumbukia katika umaskini, magonjwa na ukosefu wa fursa za ajira. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi na hasa maskini yote ni furaha, matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo. Mkutano huu unachagizwa na umaskini, hali ngumu ya maisha pamoja na changamoto zake.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa: weledi na ufanisi mkubwa unaopata chimbuko lake kutoka katika Injili ya huruma na upendo, kama Kristo Yesu alivyoguswa na mahangaiko ya watu wake, akawahudumia kwa upendo mkuu. Hii ni changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, ili kuwapaka kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini; daima ustawi, maendeleo, mafao na haki jamii zikipewa msukumo wa kwanza.

Caritas Internationalis imeweka kanuni na vigezo vya ubora wa huduma zinazotolewa na Mama Kanisa kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, vigezo hivi vinapaswa kuzingatiwa, kwani Kanisa linaitwa na kutumwa: kuhudumia, kuwasindikiza na kuwatetea maskini na wanyonge. Mashirika ya Misaada ya Kanisa yanapaswa kujizatiti katika: ukweli, uwazi na uwajibikaji na kwamba, rasilimali fedha na vitu ni kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili chini ya uongozi na usimamizi wa Askofu mahalia! Mkutano huu ni fursa ya kupembua masuala ya rasilimali fedha na changamoto zake; uzoefu na mang’amuzi katika huduma ya upendo na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa huduma ya upendo katika nchi za IMBISA.

Caritas Imbisa
29 October 2018, 09:11