Familia ya Mungu nchini Kenya kwa sasa inapambana na baa la njaa na umaskini sanjari na kukuza demokrasia shirikishi! Familia ya Mungu nchini Kenya kwa sasa inapambana na baa la njaa na umaskini sanjari na kukuza demokrasia shirikishi! 

Familia ya Mungu nchini Kenya katika mapambano ya baa la njaa na umaskini kwa kukuza demokrasia

Takwimu na shuhuda kutoka Caritas Italia zinaonesha kwamba, Kenya kwa sasa imeanza kujikita katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini na kwamba, demokrasia katika ukweli na uwazi inaanza kushika mkondo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Italia, Caritas Italia, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2018, takwimu na shuhuda zinaonesha kwamba, Kenya kwa sasa imeanza kujikita katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini na kwamba, demokrasia katika ukweli na uwazi inaanza kushika mkondo wake. Haya ni matukio yaliyojionesha katika kipindi cha mwaka 2017 pale Mahakam kuu nchini Kenya ilipofuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, uamuzi mzito uliowaacha wananchi wengi wakiwa wamepigwa butwaa kwa mshangao mkubwa, kwani hili lilikuwa ni tukio la kihistoria nchini Kenya.

Familia ya Mungu nchini Kenya, bila kuchoka, ikarejea tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na matokeo kutangazwa. Demokrasia shirikishi ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kufanyiwa kazi na nchi kadhaa Barani Afrika zikiwemo DRC, Burundi, Zimbabwe, Siera Leone, Mali, Cameroon. Wananchi wanataka kuwaona viongozi wao wa kisiasa wakiwajibika barabara katika kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani, vigezo muhimu sana katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini Barani Afrika.

Uchaguzi unaozingatia misingi ya demokrasia ya kweli ni fursa makini inayowajengea wananchi uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maamuzi ya sera na mikakati ya maendeleo endelevu inayowagusa moja kwa moja. Uchaguzi ni sauti muhimu sana ya raia katika ujenzi wa demokrasia ya kweli. Ili kufikia malengo haya, kuna haja ya kujenga utamaduni na madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kwa pamoja waweze kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini unaoendelea kudhalilisha utu, heshima na haki zao msingi.

Kumbe, mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani hauna budi kufumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana na kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na kama sehemu ya ukuaji wa demokrasia ya kweli Barani Afrika. Caritas Italia imekuwa ni mdau mkubwa wa utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani nchini Kenya kupitia katika majimbo na mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume.

Tangu mwaka 2011, baa la njaa lilipoikumba Pwani ya Pembe ya Afrika, Caritas Italia, ikakita mizizi ya huduma zake katika eneo hili, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa kuwekeza katika huduma ya maji safi na salama, kilimo endelevu na hasa vijijini pamoja na kuhakikisha kwamba, haki, amani na maridhiano yanapatikana na kudumishwa na wote. Caritas Italia, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo wanaendelea kuwekeza katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, kwa kuwajengea uwezo wafugaji wadogo wadogo, ili kuboresha hali ya mifugo yao, itakayowawezesha kuongeza kipato.

Caritas Kenya
17 October 2018, 10:10