Vatican News
Maaskofu DRC waonesha hofu ya kutofanyika uchaguzi mkuu nchini humo tarehe 23 Desemba 2018 Maaskofu DRC waonesha hofu ya kutofanyika uchaguzi mkuu nchini humo, tarehe 23 Desemba 2018  (AFP or licensors)

DRC: Maaskofu wanaonesha hofu kuhusu uchaguzi mkuu 2018!

Baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, vimefumbwa mdomo na Serikali iliyoko madarakani, hali ambayo inapania kudhohofisha nguvu ya hoja kutoka kwa wapinzani, ili kuwapatia wananchi uwepo wa kuamua hatima ya uongozi nchini mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limeonesha wasi wasi mkubwa wa kukwama tena kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 23 Desemba 2018, kutokana na kucheleweshwa kwa makusudi maandalizi muhimu ambayo yangewezesha uchaguzi huu kuwa: huru, wa haki na wenye kuaminika, tayari kuleta mageuzi makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo!

Maaskofu katika barua yao walioituma kwenye Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni, wameonesha kumekuwepo na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu na uhuru wa kujieleza hata kama tarehe 29 Septemba, 2018 vyama vya upinzani vilifanya mkutano wao mkubwa pasi na vurugu! Lakini, bado maandamano ya amani yamepigwa rufuku nchini DRC, hali ambayo inawanyima wananchi haki yao ya Kikatiba! Baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, vimefumbwa mdomo na Serikali iliyoko madarakani, hali ambayo inapania kudhohofisha nguvu ya hoja kutoka kwa wapinzani, ili kuwapatia wananchi uwepo wa kuamua hatima ya uongozi nchini mwao.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limeliomba Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuishinikiza Serikali ya DRC kuhakikisha kwamba inatoa fursa sawa kwa vyama vya kisiasa kujinadadi kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii vilivyoko nchini humo badala ya kumilikiwa na Serikali peke yake sanjari na kufyekelea mbali kizuizi cha maandamano ya amani kutoka kwa vyama vya upinzani. Maaskofu wanasema, hatari kubwa iliyoko mbele ya DRC ni kuona kwamba, Tume ya Huru ya Uchaguzi nchini humo, CENI haijafanikiwa kuorodhesha alama za vidole kutoka kwa wananchi milioni sita na kwamba, Tume inapania kutumia mashine hizi licha ya upinzani kutoka kwa wadau wanaohusika.

CENI imekuwa ikitoa mwaliko kwa watazamaji wa uchaguzi mkuu nchini humo kwa “mwendo wa kusuasua” kana kwamba, inashinikizwa! Changamoto hizi zote, zinalifanya Baraza la Maaskofu Katoliki DRC kuwa na wasi wasi mkubwa kwamba, pengine hata uchaguzi mkuu nchini humo, ukashindwa kutekelezwa na kuyeyusha ndoto ya matumaini kutoka kwa familia ya Mungu nchini DRC kama ilivyokuwa katika mwaka 2016 na matokeo yake, DRC ikajikuta ikitumbukia katika majanga na maafa makubwa ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.

Rais Joseph Kabila tayari ametangaza kwamba, hatagombea tena nafasi ya Urais nchini humo na badala yake, chama chake kimemteua Bwana Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa mambo ya ndani ya DRC kuwania uchaguzi mkuu. Maaskofu wanakaza kusema, kushindwa kufanyika kwa uchaguzi mkuu kama ilivyopangwa, kunaweza kusababisha maafa makubwa katika Eneo la Maziwa Makuu, kumbe, Jumuiya ya KImataifa inapaswa kuuangalia uchaguzi mkuu nchini DRC kama chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

 

26 October 2018, 09:57