Tafuta

Vatican News
Familia zinaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia Familia zinaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia 

Askofu Nyaisonga: Iweni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia

Familia ni kielelezo makini cha upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Familia za Kikristo zinapaswa kusimamia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; umoja, upendo, uaminifu, udumifu, msamaha na upatanisho wa dhati kutoka moyoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hivi karibuni, Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kumbu kumbu ya miaka 60 tangu Mzee Peter Msaga na Mama Agnes Ingram, kutoka Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, Tanzania, walipofunga ndoa kunako tarehe 26 Oktoba 1958 na kubahatika kupata watoto 11 katika maisha yao. Hiki ni kielelezo kwamba, Injili ya familia bado ni furaha ya walimwengu na kwamba, inajikita katika: imani, upendo, uvumilivu, huruma, msamaha na udumifu.

Katika mahubiri yake, Askofu Nyaisonga amesema, Familia ni kielelezo makini cha upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Familia za Kikristo zinapaswa kusimamia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; umoja, upendo na mshikamano, ili siku moja, kama ilivyo familia ya Mzee Peter Msaga na Mama Agnes Ingram waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa: wema, ukuu na huruma yake katika maisha yao. Zawadi ya uhai ni kielelezo cha matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Upendo wa kweli unafumbatwa katika uaminifu, uhalisia na sadaka ya maisha!

Hata katika patashika nguo kuchanika, bado wazee hawa wawili, waliweza kuvumiliana, kusameheana, daima wakiwa tayari kuanza upya safari ya maisha yao ya ndoa na familia, tarehe 26 Oktoba 2018 wanakunja jamvi la miaka 60 ya maisha ya ndoa na familia, kwa hakika si haba anasema Askofu Nyaisonga aliyefunga safari kutoka Jimbo Katoliki Mpanda, ili kuungana na familia ya Mzee Msaga, kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Injili ya familia!

Mama Agnes Ingram aliwahi kuwadokezea watoto wake kwamba, kweli yataka moyo, sadaka na uvumilivu na wala si kama watu wengi wanavyofikiri kwamba, wakati wote mambo yamekwenda shwari! Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusimulia kwamba, kuna wakati hata ndani ya familia za Kikristo, wanandoa wanarushiana sahani utadhani kwamba, ni mbayuwayu wanatafuta viota! Ni familia ambayo imeonja pia magumu ya mabadiliko ya kisiasa kwani wamefunga ndoa katika kipindi cha harakati za kupigania uhuru; wakajikuta pia, wanashuhudia madhara ya vita kati ya Tanzania na Uganda. Lakini, mwisho wa siku, wakaendelea kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kwa kuwalea, kuwatunza na kuwaendeleza watoto wao, leo hii wako mbele yao, kumtolea Mungu shukrani kwa kumbu kumbu ya Miaka 60 ya maisha ya ndoa na familia!.

Askofu Nyaisonga anakaza kusema, siri kuu ya udumifu katika maisha ya ndoa na familia za Kikristo ni: Unyenyekevu, moyo wa huruma na sadaka; utu wema na ukarimu; upole, uaminifu na uvumilivu. Mtakatifu Paulo anataja siri ya udumifu katika maisha ya ndoa na familia, katika utenzi wake wa upendo. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia kwa kujenga na kudumisha majadiliano, upendo na mshikamano katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini wajenge mawasiliano na mafungamano, kwa kupata walau muda wa kula pamoja na kuzungumza; kushirikishana hisia sanjari na kusherehekea maisha ili kudumisha umoja na upendo; kwa kuimarishana katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Majukumu ya kifamilia yatekelezwe kwa furaha, uvumilivu, huruma na upole; kwa kusaidiana na kuombeana neema na baraka katika maisha!

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, amezitaka familia kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kujituma, katika hali ya unyenyekevu sanjari na kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema, kielelezo cha imani tendaji. Wazazi watambue kwamba, wao ni walimu na makatekista wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, kumbe wanapaswa kuwa ni mifano bora ya kuigwa na watoto wao. Wajibu wa watoto ni kusikiliza kwa makini, kutazama kwa udadisi ili kuona na kuiga mema, ili kupata heri na baraka katika maisha!

Askofu Nyaisonga
25 October 2018, 10:17