Askofu Banzi anasema, tunaiharibu dunia kwa sababu hatuna mahusiano mazuri na Mungu, hatuna mahusiano mazuri katika jamii zetu, hata ndani ya familia zetu Askofu Banzi anasema, tunaiharibu dunia kwa sababu hatuna mahusiano mazuri na Mungu, hatuna mahusiano mazuri katika jamii zetu, hata ndani ya familia zetu 

Askofu Antony Banzi:kuheshimu dunia ni maadili na amri ya Mungu!

Kuiheshimu dunia ni moja ya maadili, na ni amri ya Mungu. Kuharibu mazingira ni kuabudu miungu, kwa maana hiyo, "tusiitumie dunia kwa fujo kwani atakaye athirika ni mwanadamu mwenyewe na tukiitunza nayo itatutunza”. Ndiyo wito wake katika mahubiri Askofu A. Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, Tanzania hivi karibuni

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa jina la maendeleo na ukuaji wa uchumi ni uasi sawa na kuabudu miungu, na hivyo ni wito kwa kila mwanadamu kuheshimu kazi ya uumbaji. Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Askofu Antony Banzi wakati wa Misa Takatifu ya kuwasimika viongozi wapya wa Shirika la Masista wa Mama yetu wa Usambara (COLU) iliyofanyika hivi karibuni katika Makao Makuu ya shirika hilo huko Kwamndolwa, Korogwe nchini Tanzania.

Dhamana ya mwanadamu juu ya mazingira

Wakati wa mahubiri yake katika misa hiyo, Askofu Banzi ametoa kipaumbele zaidi hasa cha kutazama kazi ya uumbajia ya Mungu,ambapo mwanadamu amepewa mamlaka juu ya mazingira na kupewa dhamana ya  kutumia zawadi hiyo kwa  akili na utashi katika kuutiisha ulimwengu na vilivyomo kwa manufaa ya leo na siku za baadaye. Askofu Banzi anabainisha kwamba, kuiheshimu dunia ni moja ya maadili na ni amri ya Mungu na kuharibu mazingira ni kuabudu miungu, na kwa maana hiyo anasema: “Tusiitumie dunia kwa fujo kwani atakaye athirika ni mwanadamu mwenyewe na tukiitunza nayo itatutunza”.

Kadhalika akiendelea na ufafanuzi zaidi,  ametaka kuwepo kwa njia rafiki katika uvuvi na ufugaji wa nyuki, huku akikemea matumizi ya mabomu na nyavu zisizofaa katika shughuli ya uvuvi, sambamba na uchomaji wa nyuki wakati wa kurina asali, akisema kuwa njia hizo zinapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira. Akiendelea na ufafunuzi huo, Askofu Banzi ameweka wazi kuwa matatizo mengi yanayotokea katika jamii husababishwa na kukosa mahusiano mazuri kati ya mwanadamu na Mungu, ambapo dawa ya uharibifu wa mazingira ni kuwa na mahusiano mazuri na Mungu pamoja na kuwa na sheria ambazo msingi wake ni Mungu.

Uhusiano mzuri na Mungu ni sambamba na mahusiano mazuri katika jamii na hasa ya wana ndoa

Akisisitiza juu ya uhusiano mwema na Mungu na binadamu amesema, “Tunaiharibu dunia kwa sababu hatuna mahusiano mazuri na Mungu, hatuna mahusiano mazuri katika jamii zetu, hata familia zetu”.  Na kwa maana hiyo ametoa wito kwa waamini wote hasa katika maisha ya ndoa na kwamba wasifikirie suala la talaka na badala yake amesema kuwa dawa  ya changamoto za ndoa, ni kujenga mahusiano mazuri na Mungu. “Talaka ni matokeo ya kukosa mahusiano mazuri na Mungu. Ukiona mtu anang’ang’ania jambo hilo daima huwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo, jambo la muhimu ni kubaki katika ndoa ama wito wa utawa” amesisitiza Askofu Banzi.

Viongozi mpya wa shirika la Mama yetu wapya kusimikwa rasmi

Katika hatua nyingin,e Askofu Banzi amewasimika rasmi viongozi wa Shirika la Masista wa Mama yetu wa Usambara (COLU) ambapo Mama Mkuu aliyechaguliwa kuongoza masista hao ni Sista Maria Gaspara Kashamba, ambaye amechaguliwa kwa awamu ya pili mara baada ya kuwa Mama Mkuu kwa miaka sita iliyopita. Wengine ni Sista Maria Focus Mjema aliyechaguliwa kuwa Mama Mkuu msaidizi, Sista Maria Regina, Sista Maria Vincent na Sista Maria Eveta. Viongozi hao wamekula kiapo mbele ya Askofu Banzi na waamini waliohudhuria misa hiyo. Askofu Banzi amesema kuwa kazi ya Mama Mkuu huyo mpya ni kumiliki, kulinda na kuendeleza utume na amali zote za shirika hilo hasa kwa kumtanguliza Mungu.

Mwanzo wa Shirika la Masista wa Mama yetu wa Usambara (COLU)

Shirika la Masista wa Mama yetu wa Usambara (COLU) lilianzishwa mwaka 1954 katika mkoa wa Tanga kwenye milima ya Usambara katika Wilaya ya Lushoto na aliyeanzisha shirika ni Monsinyo Eugeni Arthurs wa Shirika la Mapendo (Mapadri Warosmini). Monsinyo aliomba Masista wa Damu Takatifu (CPS) ili walilee shirika hili jipya, ndipo alipopewa Sista Wilibalda Giesbers akishirikiana na Sista Ambrose Mollers ambao walilea na kuliongoza shirika tangu mwaka huo wa 1954 mpka 1976 walipopokelewa na Sista Inviolata Mndeme, Mama Mkuu wa kwanza mzalendo.

Kupokea vijana wa kwanza wa kujiunga na shirika

Walezi hawa waliwapokea wasichana 12 mwaka 1954 katika shirika. Hadi leo bado wapo masista wawili waliobaki baada ya wenzao kufariki dunia, nao ni Sista Ancilla Macha na Sista Bernadetha Massawe. Shirika hili limekuwa na watawa wake wafanyakazi katika majimbo ya Tanga, Moshi, Dar es salaam, Same, Mbulu na Reggio Calabria Italia, ambapo wanatoa huduma za kufundisha dini maparokiani, kufundisha kwenye shule za chekechea, msingi, sekondari na vyuo. Pia wanawahudumia wagonjwa mahospitalini, vituo vya afya, zahanati na majumbani.

26 October 2018, 15:19