Tarehe 4 Septemba 2016 Mama Theresa wa Calcuta alitangazwa Mtakatifu Tarehe 4 Septemba 2016 Mama Theresa wa Calcuta alitangazwa Mtakatifu 

Mwaka wa pili,tangu Mama Theresa wa Calcuta kutangazwa Mtakatafu

Ninaona kiu, ni sauti ya Bwana ambayo Mama Teresa wa Calcuta alihisi rohoni mwake kabla ya kuanzisha Shirika la Upendo. Katika tukio la kutangazwa mtakatifu tarehe 4 Septemba 2016, Baba Francisk alisema, tutakuwa na shida kidogo ya kumwita Mtakatifu Theresa, kwa sababu utakatifu wake uko karibu sana na kwa maana hiyo tutaendelea kumwita Mama Theresa

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Tarehe 4 Septemba ni mwaka wa pili Tangu Mama Taresa wa Kalkota ametangazwa kuwa Mtakatifu  kuna tarehe 4 Septemba 2016. Maadhimisho yaliyofanyika katika Kiwanja cha Mtakatif Petro.

Katika tukio la kutangazwa mtakatifu tarehe 4 Septemba 2016, hata  Baba Mtakatifu alisema, tutakuwa na shida kidogo ya kumwita Mtakatifu Theresa, kwa sababu utakatifu wake uko karibu sana na sisi  kiasi cha kuona kwamba yeye  ni mwema na amekwishatoa  matunda na hivyo kwa urahsi tutendelea kusema Mama Theresa. Aidha aliongeza; mtu huyo asiyechoka katika jitihada za huruma , atusaidie kuelewa zaidi na zaidi kwamba kigezo kimoja tu cha matendo ni upendo wa bure, bila kuwa na itikadi yoyote na dhamana yoyote, kutokuwa na ubaguzi na bila utofauti wa lugha , utamaduni, rangi au dini. Na kwamba Mama Theresa alipenda kusema hata kama sizungumzi lugha yao, lakini ninaweza kutabasamu.

Mama Teresa, aliinama kwa watu walioachwa wafe katika pembezoni  mwa barabara, na mitaa kwa kutambua hadhi yao  waliyopewa na Mungu.  Mama Theresa ni mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Upendo na mwenye tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 1979.  Ni mtawa ambaye ni mfano wa pekee katika maajabu ambayo yanaweza kujikamilisha ndani ya kujitoa kwake Yesu Kristo. Tarehe 26 Oktoba 1985 akiwa katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati ule ambaye alikuwa ni   Pérez de Cuéllar alimwelezea mama Theresa kuwa ni mwanamke mwenye nguvu zaidi katika dunia. Licha ya Mtawa huyo mdogo katika mavazi yake rahisi, alipendelea kujiita kuwa yeye ni kalamu ndogo ya risasi katika mikono ya Mungu. Karamu ndogo ya risasi lakini yenye uwezo wa kuandika kurasa nyingi kuhusu huruma na ambaye kwa nguvu ya imani yake aliweza kufungua nyumba nyingi za wahitahiji hata katika maeneo yasiyoelezeka, kuanzia Quba hadi katika muungano wa nchi za Kisovietiki. Na kila mmoja aliyeuliza siri yake ni ipi alijibu  kwa urahisi kwamba anasali. Lakini Basi ebu tutazame kwa ufupi historia yake  Mama Teresa wa Calcuta

Alikuwa ni nani?

Mama Theresa wa Calcutta alizaliwa kunako tarehe 26 Agosti 1910 huko Skopje, Macedonia na wazazi wake walikuwa wanatoka Albania. Akiwa na umri wa miaka 18 akajiunga na Shirika la Watawa wa Bikira Maria wa Loreto. Kunako mwaka 1928 akatumwa kwenda Ireland na baada ya mwaka mmoja akatumwa nchini India. Kunako mwaka 1931 akaweka nadhiri zake za kwanza na kupewa jina la Sr. Maria Theresa wa Mtoto Yesu. Kwa muda wa miaka 20 akafundisha historia na jiografia huko Calcutta na huko akakutana na umaskini mkubwa miongoni mwa watu!

Wamisionari wa Upendo: Tarehe 10 Septemba 1946 akiwa njiani kuelekea mjini Darjeeling akasikia sauti ikimwambia ndani mwake,”nina kiu” na hivyo akayakumbuka maneno ya Yesu pale Msalabani! Haya ni maneno ambayo yataendelea kuandikwa kwenye nyumba zote zilizoanzishwa na Mama Theresa wa Calcutta, kama muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Upendo na huduma ya upendo ni utambulisho na karama yao!

Katika ulimwengu wa maskini kati ya maskini: Tarehe 16 Agosti 1948 akaondoka kutoka katika Shirika la Bikira Maria wa Loreto, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kunako mwaka 1949 akaungana na baadhi ya wanafunzi wake kuanzisha Shirika Jipya la kitawa kwa ajili ya kuwahudumia maskini kati ya maskini pamoja na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, huku akijitahidi kufuata na kuiga mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Tarehe 7 Oktoba 1950 Shirika lake likatambuliwa rasmi na Kanisa mahalia, wakat iwa maadhimisho ya Siku kuu ya Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili. Mama Theresa wa Calcutta akaliweka Shirika lake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu sanjari na Moyo Safi wa Maria. Licha ya nadhiri ya usafi wa moyo, ufukara na utii, watawa wa Mama Theresa wa Calcutta wanaweka pia nadhiri ya huduma kwa maskini zaidi.

Kunako mwaka 1952 Mama Theresa wa Calcutta akafungua nyumba kwa ajili ya watu waliokuwa kufani na hatimaye, huduma hii ikapanuka kwa ajili ya wagonjwa na watoto yatima. Kunako mwaka 1965 Mwenyeheri Paulo VI akalipatia Shirika la Wamissionari wa Upendo hadhi na haki za Kipapa. Mwaka 1981 tawi la tafakari likaanzishwa kwa ajili ya Mapadre wa Jimbo, huku wakiwa na Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Sifa na unyenyekevu na huduma makini ya Mama Theresa wa Calcutta ikaenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia.

Mwaka 1979 akatunukiwa Tuzo ya Amani Duniani kwa kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya umaskini na hali ngumu ya maisha. Kutokana na utume wake kwa maskini, akajenga urafiki wa karibu sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, kiasi cha kumwezesha kufungua nyumba tatu mjini Roma. Tarehe 5 Septemba 1997 Mama Theresa wa Calcutta akiwa na umri wa miaka 87 akafariki dunia. Mwezi Julai 1999 mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ukaanza rasmi kwa ridhaa ya Mtakatifu Yohane Paulo II.

Wakati huo tarehe 19 Oktoba 2003 atakatangazwa kuwa Mwenyeheri na mfano wa Msamaria mwema, aliyethubutu kumwilisha Injili katika huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa, maskini na watoto yatima; huduma iliyorutubishwa kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Tarehe 17 Desemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko akatambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mama Theresa wa Calcutta na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu.

Mama Theresa wa Calcutta ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini.

Watawa wake, wanaendelea kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka na majitoleo yao kwa maskini, kama ilivyotokea huko Yemen, kwa watawa wake walio uwawa kinyama.  Kadhalika Mama Teresa wa Calcutta, daima aliuona utume wake wa kimissionari kama changamoto na mwaliko wa wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kukumbatia neema, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Mama Teresa alijitahidi kuhakikisha kwamba, anawaonjesha upendo wa Kristo, wote waliokuwa wanamzunguka, akiongozwa na dhamiri nyofu. Ni mwanamke aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujibu kilio cha jirani zake, kwa njia ya matendo ya huruma.

04 September 2018, 16:36