Tafuta

Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi 

Askofu Mkuu Ruwa'ichi akaribishwa rasmi jimbo Kuu Dar Es Salaam

Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Tanzania limemkaribisha rasmi, Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa'ichi kwa maadhimisho ia Misa Takatifu na Maaskofu,Mapadre, watawa, na waamini wa Mungu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.

Mwishoni mwa wiki uliyopita tarehe 7  Septemba 2018, Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Tanzania, limemkaribisha rasmi, Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi ambaye ni mwandamizi wa jimbo hilo. Tarehe 21 Juni 2018 Baba  Mtakatifu Francisko alimteua Askofu mkuu Ruwaichi kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.

Askofu Mkuu Mwandamizi hakuja kupumzika bali kufanya kazi: Wakati wa sherehe za mapokezi hayo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Kardinali Pengo ameweza kugawa majukumu ya utendaji wa utume kichungaji kwa Askofu Mkuu Mwandamizi, Yuda Thadeus Ruwa’ichi ambaye amefika rasmi tarehe 7 Septemba Jijijini Dar es Salaam na kulakiwa na waumini wa jimbo hilo kuu na pia Askofu Msaidizi, Eusebius Nzigilwa.

Kardinali Pengo wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu ya kumkaribisha Askofu Mkuu Mwandamizi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, amesema kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi hakuja Dar es Salaam kupumzika bali kufanya kazi. Na kuendelea kusema kuwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi amehamishiwa Dar es Salaam baada ya Baba Mtakatifu, Francis kukubali ombi la Kardinali Pengo ili awe na msaidizi, kwa maana hiyo  uwepo wake utasaidia mgawanyo wa shughuli za kichungaji kwenda vizuri kwani jimbo hilo lina parokia zaidi ya 100 na vigango vingi.

Kuomba msaidizi wa jimbo: Kadhalika akiendelea na ufafanuzi huo alisema wakati anamwomba Papa hakupendekeza jina la askofu yeyote bali alimwachia Baba Mtakatifu atoe uamuzi mwenyewe na ndipo alipoamua kumteua Askofu Mkuu Ruwa’ichi kuwa mwandamizi wake. Kutokana na hili aliongeza kusema: “Mtuombee sisi maaskofu wenu watatu ili tuwe na imani ya kutambua Yesu ni Mwokozi wa Ulimwengu na ni Mwokozi wa wanadamu kwani yeye ni Mungu na pia ni mwanadamu,”.

Majukumu ya maaskofu watatu jimboni Dar Es Salaam: Akifafanua zaidi juu ya wajibu wao kichungaji katika jimbo hilo Kuu, alitangaza mgawanyo wa majukumu yao kusimamia idara mbalimbali akiwemo yeye mwenyewe. Kufuatana hiyo ametoa mwelekezo wa mangozi kama ya idara ifuatavyo: Kardinali Pengo atakuwa na idara ya Liturujia, Mahakama ya Kanisa, Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) na Utoto Mtakatifu; na kwa upande wa Askofu Mkuu Mwandamizi Ruwa’ichi atasimamia Idara ya Uchungaji, Utume wa Walei, Teolojia, Haki na Amani pamoja na Caritas, na wakati huo  Askofu Msaidizi, E. Nzigilwa atakuwa na jukumu la kusimamia Idara ya Miito, Katekesi, Mafundisho ya dini, Vijana Wakatoliki na Mawasiliano.

Pamoja na hayo Kardinali Pengo pia aligawa hata mipaka ya maeneo ya shughuli za kichungaji kwa kila Askofu ambapo Askofu Mkuu Mwandamizi atakuwa akitoa huduma za kichungaji katika eneo lote la upande wa kushoto mwa Barabara ya Nyerere, huku Askofu Nzigilwa akapangiwa eneo lote la upande wa kulia mwa Barabara ya Morogoro na sehemu iliyobaki  katikati ya Barabara za Morogoro na Nyerere litakuwa chini ya Kardinali Pengo.

Wakati wa huo naye Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimshukuru Mungu kwa kumpa majukumu mapya na kuomba waumini wote wamwombee ayatimize kwa uaminifu. Na alipendelea zawadi ya Sh milioni 80 aliyopewa na Jimbo Kuu la Mwanza,  kiasi cha shiliongi milioni 60 kati ya fedha hizo zirudi jimboni humo ili kufanikisha shughuli za kitume. Ilikuwa ni sherehe nzuri ambayo iliudhuriwa na wengi mapadre, watawa , waamini walei, pamoja na viongozi wa serikali kama vile wastaafu waliohudhuria Misa ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Spika mstaafu, Anne Makinda na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa.

Kabla ya uteuzi wa Askofu Mkuu Ruwaichi kuwa mwandamizi: Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Askofu mkuu Ruwaichi alizaliwa kunako tarehe 30 Desemba 1953, Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 25 Novemba 1981. Tarehe 9 Februari 1999 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu na kuwekwa wakfu tarehe 16 Mei 1999.

Tarehe 15 Januari 2005, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2005. Tarehe 10 Novemba 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza na kusimikwa rasmi tarehe 9 Januari 2011

11 September 2018, 14:21