Tafuta

Vatican News
Lipo wimbi la uhamiaji wa mapadre na watawa kutoka Afrika kwenda Ulaya Lipo wimbi la uhamiaji wa mapadre na watawa kutoka Afrika kwenda Ulaya  (Vatican Media)

Uhamiaji wa kidini kutoka Afrika kwenda Ulaya !

Ongezeko la mapadre na watawa wanaoliacha bara la Africa na kwenda Ulaya linaongezeka mara dufu. Ni huzuni lakini ni muhimu kutambua kwamba suala la uhamiaji ulaya linatazama sio tu jamii zetu za kiafrika lakini pia majimbo yetu mengi, maparokia na jumuiya za kikristu.

Frt Tito Kimario - Vatican

Wimbi la uhamiaji wa mapadre na watawa kutoka Afrika kwenda Ulaya limeelezwa kuwa hatari kwa ukuaji wa kanisa mahalia barani Afrika. “kwenda Ulaya, kuishi ulaya na kuliacha bara la Afrika imegeuka kuwa dhana potovu na hatari sana inayovunja moyo wanyonge na kuimarisha walio imara” anasema Padre Donald Zagore  wa shirika la wamisionari wa Afrika.

Ongezeko la mapadre na watawa wanaoliacha bara la Africa na kwenda Ulaya linaongezeka mara dufu. Ni huzuni lakini ni muhimu kutambua kwamba suala la uhamiaji ulaya linatazama sio tu jamii zetu za kiafrika lakini pia majimbo yetu mengi, maparokia na jumuiya za kikristu. Kuna idadi kubwa ya mapadre na watawa wanaoliacha bara la Afrika ili kuhudumia bara la ulaya na America. Uhamiaji huu kutoka Africa kwenda ng’ambo katika mtazamo wa kitawa, ni jambo linalokua kila siku katika bara letu” amesisitiza mmisionari.

Ni jambo lililokemewa vikali na baadhi ya maaskofu.

Mwanzoni mwa mwaka 2017, askofu Mercelin Yao Kouadio,  askofu wa jimbo la Daloa katika moja ya mahubiri yake aligusia baadhi ya matukio katika majimbo mawili ya Africa yaliyokumbwa na uhamiaji huu.  Mwezi wa tano mwaka huu, askofu Ignace Bessi Dogbo, ambaye pia ni rais wa baraza la maaskofu wa Ivory Coast katika ufunguzi wa mkutano wa maaskofu , alizungumzia jambo hili aliloliita “Makuhani wapotoshaji”: Mapadre waliokataa kurudi Afrika baada ya masomo au utume huko ulaya. Katika mahojiano ya Agosti 7 mwaka huu, askofu mkuu wa Rouen,  Dominique Lebrun  nae amekiri uwepo wa hii kadhia.

Akizungumza na jumuiya ya mapadre, waseminari na watawa wanaosoma mjini Roma, Askofu mkuu wa jimbo kuu la Arusha mh. Isaac Amani, tarehe 29 Juni 2018, aliliguzia suala hilo na kuwataka mapadre na watawa wanaotumwa ulaya kusoma au kwa utume kuhakikisha wanarudi katika muda muafaka ili kuwatumikia waamini waliokabidhiwa huko Afrika katika majimbo husika na kuongeza kuwa bahati waliyoipata kwenda ng’ambo kwa masomo zaidi au utume  ni tunu na ni lazima warudi ili wakazitumie kwa ajili ya manufaa ya wengine na hivi kumtukuza Mungu na sio kutafuta vijisababu vya kung’ang’ania ulaya na Amerika.

Sababu kadhaa zimekua zikiwashawishi mapadre na watawa kukimbilia ulaya. “moja ya sababu kuu inabakia utafutaji wa mali na ufahari” ameeleza Padre Donald. Wengi wao hukimbia Africa kutokana na tabu na lindi la umaskini. Zaidi ya hayo, Waafrika wengi wanadhani kuwa ni bora kuliko wengine, hasa katika Uklero, kwa sababu wanaishi, wanasoma au wanafanya kazi ulaya. Mara nyingine uteuzi au nafasi ya masomo ya juu Ulaya vinachukua sura ya “ukombozi”. Ni ajabu sana kufikiri kwamba uafrika wetu unafikia utimilifu wake kwa kuishi umaarufu na furaha za Ulaya.

Ni hatari kubwa kwa kanisa katoliki barani Africa, kanisa linalopungukiwa mapadre na watawa mbali na kuenea kwa miito isiyo ya kweli. Leo inafaa kufikiri kwamba sio lazima kuwa padre ili kuwahudumia masikini ktk Kristo, kwamba mtu anakimbizana na tamaa za mali na utukufu wa kidunia ambayo yanasababisha mgawanyiko na migogoro katika kanisa la Afrika, ameeeleza Padre Donald.

Hatua za haraka zinahitajika ili kulinusuru kanisa la Africa na uhamiaji huu wa watumishi wa Mungu. Katika majimbo yetu na jumuiya zetu za kitawa kunahitajika hatua madhubuti kuzuia uhamaji huu wa rasilimali ya watu katika ukleri.  Kwanza kabisa tunapaswa kuwa na ufahamu wa jumla wa hatari kubwa inayosababishwa na uhamiaji wa namna hii. Pili ni kwa mamlaka husika za kanisa kuchunguza kwa makini motisha zinazowasukuma vijana kuchagua maisha ya upadre na utawa na zaidi kuwa makini zaidi na teuzi wanazopewa mapadre kwenda ngambo na mwisho ni lazima kusimamia kidete, usemi huu wa askofu Mercelin Kouadio Upadre na maisha ya kitawa havipaswi kuwa nyenzo ya kulikimbia bara la Afrika eti kwa sababu ni masikini, amehitimisha Padre Zagore.

23 August 2018, 10:34