Tafuta

Vatican News
Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu inafumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Tasaufi ya Damu azizi ya Yesu inafumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.  (AFP or licensors)

Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo inafumbata Injili ya uhai!

Tasaufi ya Damu Takatifu inaweka bayana kuwa uhai wa mwanadamu ni zawadi toka kwa Mungu mwenyewe. Kama mtu binafsi au jumuiya, wanapewa jukumu la kuendeleza utamaduni wa uhai na kuitangaza na kuishuhudia Injili ya uhai. Wote wanaoongozwa na tasaufi hii wana wajibu wa kupinga mambo yote yanayotishia maisha na heshima ya mwanadamu.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu msikilizaji, ninakukaribisha tena katika mwendelezo wa tafakari yetu juu ya tasaufi ya Damu Takatifu ya Kristo. Tasaufi ya Damu Takatifu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo ni msingi wa ukombozi wetu na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote. Pia tasaufi hii ina msingi wake katika na Neno la Mungu na katika Ekaristi Takatifu ambayo ndiyo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. (Rej Kifungu namba 1324 cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki). Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani yetu na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. (Rejea kifungu namba 1327 cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki).

Katika tafakari yetu iliyopita tuliangalia jinsi ambavyo tasaufi ya Damu Takatifu inavyoweza kutuongoza na kutujenga katika kuishi tunu mbalimbali za imani yetu kadiri ya mafundisho ya Injili. Tuliona na jinsi gani tasaufi hii inatusaidia kutambua ukuu wa huruma ya Mungu kwa wanadamu na jinsi gani twaweza kuitikia mwaliko wa Yesu wa kututaka tuwe wenye huruma kama jinsi Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma.

Pia tuliona kuwa tasaufi hii inatupa changamoto ya kuwa na upendo usiobagua kama jinsi Mungu anavyowapenda wote bila ubaguzi na kama jinsi ambavyo Yesu mwenyewe alivyouishi upendo huo hapa duniani. Hatimaye tuliona kwamba tasaufi hii inatusaidia kumuiga Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa na mshikamano na wale wenye shida kama namna mojawapo ya kuliishi fumbo la umwilisho tukimuiga Yesu mwenyewe aliyekubali kujinyenyekeza akawa mwanadamu na akatutumikia.

Kutokana na upana na utajiri wa tasaufi hii, si rahisi kuziongelea tunu zote. Kila mmoja wetu anaalikwa kuendelea kutafakari zaidi juu ya Damu Takatifu ya Yesu ili kugundua tunu nyingine za kikristo zitokanazo na tasaufi hii. Leo, tungependa kwa kifupi kuona ni jinsi gani tasaufi ya Damu Takatifu inavyotusaidia na kutujenga katika mitazamo sahihi kuhusu Mungu, maisha, wenzetu, na ulimwengu kwa jumla.

Mosi, Tasaufi ya Damu Takatifu inatusisitizia juu ya thamani kubwa ya uhai wa mwanadamu na heshima aliyonayo:

Sisi sote katika maisha ya kawaida tunatambua umuhimu ya damu katika mwiili wa mwanadamu. Damu ina kazi nyingi; huvipa viungo vyote uhai na kuupa mwili kinga dhidi ya magonjwa. Damu hubeba na kupeleka hewa ya oksijeni na chakula kwa kila kiungo na huondoa kutoka kila kiungo kitu chochote chenye madhara kwa mwili. Damu hurekebisha joto la mwili na hurekebisha mifumo mingine katika mwili. Kwa kifupi damu ina thamani kubwa kwa maisha na uhai wa mwanadamu, bila damu mtu hawezi kuishi.

Katika Agano la Kale damu ilikuwa na nafasi kubwa sana katika imani na katika shughuli za kiibada. Kwa Waisraeli damu haikuwa tu ishara ya uhai bali waliihesabu kwa ndiyo uhai wenyewe. Walitambua kuwa ni Mungu pekee ndiye chanzo cha uhai na uhai ni mali yake. (Rejea Walawi 17:14.) Walitambua kuwa bila damu, maisha ya mwanadamu au ya mnyama hayawezekani. Kwa sababu ndani ya damu kuna uhai, Waisraeli hawakuruhusiwa kula nyama yeyote mpaka walipohakikisha kuwa damu yote imeondolewa. (Rejea Walawi 17: 10, 12; Mwanzo 9:1, 3-4; Walawi 17:13-14; Hesabu 12: 16, 23.).

Kwakuwa damu na uhai ni mali ya Mungu, Waisraeli walitambua kuwa Mungu pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuitoa damu toka kwa mwanadamu au toka kwa mnyama. Kumwaga damu ya mtu lilikuwa ni kosa dhidi ya Mungu mwenyewe. Maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu yalihesabiwa kuwa ni ya thamani kubwa. Damu ya mtu yeyote iliyomwagwa ilikuwa ni chukizo kubwa kwa Mungu. (Rejea 1Sam 19: 5). Ndiyo maana Mungu hakupenda Mfalme Daudi amjengee nyumba kutokana na damu nyingi aliyokuwa ameimwaga siku za nyuma. (Rejea 1Kumb 22:8; 28:3).

Agano Jipya nalo linaongelea damu kama msingi wa maisha lakini linaweka msisitizo mkubwa katika Damu ya Kristo kama msingi wa uhai na uzima wa milele. Yesu anapoelezea juu ya lengo lake la kuja hapa duniani anasema kwamba alikuja ili watu wawe na uhai tena wawe na uhai tele (Rejea Yoh 10:10). Damu ya Kristo iliyomwagika msalabani haikututakasa na kutuondolea dhambi tu bali pia ilituunganisha katika maisha ya Kristo, maisha ya kimungu na maisha ya neema. Yesu mwenyewe anasema, “aulaye mwili wangu na kuinywa Damu yangu, hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake.” (Yohana 6: 56).

Kama jinsi ambavyo damu ni muhimu kwa uhai wa mwili wa mwanadamu, Damu ya Kristo ndiyo msingi wa uhai wa maisha ya kiroho ya kila Mkristo. Yesu mwenyewe anasema, “aulaye mwili wangu na kuinywa Damu yangu ataishi milele.” (Yohana 6: 54). Moja kati ya miongozo ya mtu anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu au yule aishiye ibada kwa Damu Takatifu ya Yes uni jukumu la kupokea sacramenti za Kitubio na Ekaristi Takatifu mara kwa mara. Basi kumbe tasaufi hii katika maisha ya kawaida ya Mkristo inamuongoza katika kuifuata njia ya utakatifu.

Kutokana na thamani ya uhai wa mwanadamu, tasaufi ya Damu Takatifu inasisitiza kuwa uhai wa kila mwanadamu lazima uthaminiwe na utunzwe. Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika barua yake ya kipapa, Evangelium vitae, anasisitiza juu ya jambo hili akisema kuwa ujumbe mkuu na wa msingi wa Injili ya Yesu ni ni kuhusu uhai au maisha. (Rejea Evangelium Vitae # 1). Kwa sababu hiyo kila mwanadamu anaalikwa katika ukamilifu wa maisha kuanzia maisha yake ya kimwili hapa duniani na katika kushiriki maisha ya kimungu. (Rejea Evangelium Vitae # 2). Sambamba na mafundisho hayo ya Mtakatifu Yohane Paulo II, tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu inasisitiza kuwa mwanadamu lazima alindwe na kupewa haki yake ya kuishi tangu akiwa bado tumboni mwa mama na hatimaye katika safari nzima ya maisha yake kama mtoto, kijana, mtu mzima na hata akiwa mzee sana, akiwa mgonjwa au akiwa na upungufu fulani katika maumbile yake.

Tasaufi ya Damu Takatifu inaweka bayana kuwa uhai wa mwanadamu ni zawadi toka kwa Mungu mwenyewe, zawadi yenye thamani kubwa na hivyo wanadamu, kama mtu binafsi au jumuiya, wanapewa jukumu la kuendeleza utamaduni wa uhai na kuitangaza Injili ya uhai kwa watu wote, waliowaamini na wasiowaamini.  Wote wanaoongozwa na tasaufi hii wana wajibu wa kupinga mambo yote yanayotishia maisha na heshima ya mwanadamu.

Wanaalikwa kupinga vitendo vyote vyenye kutishia na kuharibu maisha ya mwanadamu, kwa mfano mfano; utoaji mimba, ukatili dhidi ya watu, vita, magonjwa, njaa, uchafuaji wa mazingira ambao hatimaye husababisha magonjwa na vifo. Wanaoongozwa na tasaufi hii wanaalikwa kupinga mambo yote yanayo mdhalilisha na kumvunjia heshima na kumnyima haki zake za msingi, mfano; aina mbali mbali za utumwa, unyonyaji, rushwa na mambo mengine kama hayo.

Wanaoongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu ya Yesu wanapewa changamoto ya kuwa mstari wa mbele kimatendo kutetea maisha na kupinga utamaduni wa kifo na vitendo vyote vya uvunjifu wa haki. Kwa mfano, daktari anayeongozwa na tasaufi hii kamwe hatataka rushwa kama sharti la kumtibu mgonjwa. Kadhalika daktari huyo hawezi kuingia katika mgomo wa kuwatibu wagonjwa kama sharti la kuongezewa mshahara. Kinyume chake ataangalia kwanza kuokoa maisha na kisha kudai haki yake kwa namna nyingine. Inasikitisha kuona kuwa wagonjwa wengi wamepoteza maisha kutokana na migomo katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania. Tasaufi ya Damu Takatifu inatia mkazo kwamba maisha ya mwanadamu ni muhimu zaidi kuliko fedha ambayo ulimwengu wa sasa unajaribu kuiweka mbele na kumtoa Mungu na mwanadamu katika nafasi zao.

Kumbe basi, tasaufi ya Damu Takatifu ni msaada wa kutuongoza na kutukumbusha juu ya mitazamo yetu sahihi kama wakristu na juu ya wajibu wetu kwa wenzetu na kwa kwa dunia nzima. Ninakualika basi ili nawe uweze kuchota kutoka tasaufi hii nguvu ya kumtumikia Mungu na kuwatumikia wengine kwa kutoa ushuhuda wa imani kwa maneno na kwa matendo.

Unaweza kusikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

04 August 2018, 09:38