Tafuta

Kutaniko la Mungu na Binadamu Kutaniko la Mungu na Binadamu 

Neno la Mungu linasimama, hata kama yote yatapita!

Tunajikuta mara nyingi tunapoteza imani au kuwa na udhaifu kiimani pale mambo yamekwama. Badala ya kumweka Mungu katika nafasi ya kwanza yaani kuwa chanzo, mratibu na mwisho wa yote tuyafanyayo, tunamweka Yeye kama pambo la kuthibitisha kile tunachokifikiria. Neno lake lapaswa kusimama daima hata kama linapingana na matakwa au mawazo yetu.

Padre Joseph Peter Mosha - Vatican.

Hekima ya mwanadamu inatengeneza mazingira yake na kujitahidi kumleta mwenyezi Mungu aenee katika mazingira hayo. Haya huonekana pale tunaposhindwa kumwelewa Mungu katika changamoto fulani fulani za maisha. Tunajikuta mara nyingi tunapoteza imani au kuwa na udhaifu kiimani pale mambo yamekwama. Badala ya kumweka Mungu katika nafasi ya kwanza yaani kuwa chanzo, mratibu na mwisho wa yote tuyafanyayo, tunamweka Yeye kama pambo la kuthibitisha kile tunachokifikiria. Katika muktadha wa kiimani tunapaswa kumtanguliza Mungu mbele. Neno lake lapaswa kupewa kiapo mbele. Neno lake lapaswa kusimama daima hata kama linapingana na matakwa au mawazo yetu.

Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”. Maneno haya Kristo ni ya msingi na yanakuja baada ya kuona mwitikio wa watu juu ya fundisho lake kuhusu chakula cha uzima. Tangu mstari wa 26 wa sura ya sita ya Injili ya Yohane Kristo alinuia kuwaondoa wafuasi wake kutoka katika fikara za kimwili ili kuupokea ujumbe wa kiroho aliotuletea wanadamu. Mara nyingi tunafungwa na fikara na matamanio ya kimwili na kujidanganya tunaifuata vyema imani yetu. Mara nyingi tunahusisha mambo ya kidunia na misingi ya kiimani na kujikuta tunayaweka mambo ya kiimani katika nafasi ya pili, au kuyachukulia kama kitu kinachothibitisha tu mambo ya kimwili.

Kristo anasema: “mwili haufai kitu”. Hii haimaanishi kuudharau mwili. Mwili unabaki katika umuhimu wake na ulazima wa kumwelezea mwanadamu. Msisitizo ni kuwa muunganiko wetu na Mungu katika hali ya kiroho. Roho ndiyo inayotuunganisha na Mungu na hivyo kutupatia uzima. Hatuunganiki na Mungu kwa kumwelewa katika ustadi wa akili zetu za kimwili bali katika unganiko la ndani la kiroho. Unganiko hilo ndilo mazingira mahsusi ya kumfanya mmoja kuweza kuuelewa ujumbe wa ukombozi uletwao na Kristo. Ujumbe huo ni ujumbe wa kiroho, ujumbe ambao ukipokelewa katika namna sahihi unakuwa na tija kubwa katika maisha ya mwanadamu ndani ya jamii. Ujumbe huo unapopokelewa vyema utamjenga mtu katika ukomavu wa kiutu.

“Bwana! Twende kwa nani?

Wewe unayo maneno ya uzima wa milele”. Pale tunapokosa kuona maana ya maisha, kuona mwanga mbele tunapaswa kupata ujasiri huo wa kujikabidhisha kwa Kristo kwa kuona hakuna namna nyingine ya kutustawisha kiroho na kimwili bali kubaki katika Yeye. Kutaniko letu na Kristo ni kutaniko la kiroho na hivyo ujasiri huo hauji bure kama tusipompokea Kristo kiroho. Ni wajibu kwetu kuona namna tunavyomtafuta Kristo. Tunapokumbana na ugumu wa kumpokea tunapaswa kujiuliza kama kweli tumempokea katika namna ya kiroho. Tunaweza kutumia akili na ujuzi wetu kumwelewa Kristo na kumwelezea kwa maandiko mbalimbali lakini bado asiingie mioyoni mwetu.

Hili linaweza kujithibitisha kwa namna tunavyotenda katika maisha.

Changamoto nyingi za kimaisha ambazo mwanadamu anakutana nazo zinashawishi kurudi nyuma na kumwacha Kristo. Wapo wengine wanaotamani hata kutumia nguvu za giza. Namna hizi ni kishawishi cha kutaka kurudi nyuma na kumwacha Kristo. Kristo anamuuliza kila mmoja moyoni: “Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Namna hii pia inajitokeza katika jamii ya Waisraeli wakati wakiwa mbele za Mungu huko Shekemu. Yoshua aliwaandaa katika namna ya kiroho ili kufanya maamuzi ya maisha. Aliwakumbusha historia yao na juu ya mkono wa Mungu wenye nguvu uliowakomboa kisha akawapa uchaguzi: “Nanyi kama mkiona vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia… lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana”.

Leo hii tunachagua kumtumikia nani? Je, amfundisho ya imani yanakuwa magumu sana kwetu? Tunavutwa na miungu ya fedha, madaraka, umaarufu na utajiri ambayo tuliitumikia zamani. Lakini tunakumbushwa namna miungu hiyo ilivyotuingiza katika majanga. Tumepoteza ndugu zetu na marafiki sababu ya kiburi na ubinafsi wetu, tumeua dhamiri za watu, tumenyang’anya haki za watu. Tulitawaliwa sana na maelekeo ya mwili ambao haufai kitu. Maisha yetu kiroho yalikuwa mfu. Kwa ujumla utumishi wetu kwa miungu hiyo umetuingiza katika maangamizi ya utu wetu. Lakini tunashukuru tumeletewa neno la uzima kwa njia ya Kristo, neno ambalo linatupatia uzima a milele na kuturudisha katika hadhi yetu iliyochakachuliwa na dhambi. Hivyo uchaguzi ni wako: kumtumikia Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo na kupata uzima wa milele au kurudi kwenye miungu ya zamani na kuingia katika kifo.

Swali la Kristo kwa Mitume wake linatufundisha pia uimara unaohitajika katika mafundisho ya Kanisa. Si kwa sababu watu fulani wameondoka au wameshindwa kuelewa fundisho letu ndipo tulegeze ukweli wa mafundisho yetu. Neno la Mungu linapaswa kusimama milele. Ni onyo la kuepuka kuineza imani kwa kutafuta kuongeza idadi ya wafuasi tu bila kuangalia kiwango na ubora wa imani katika kundi. Namna hii itafananishwa na makundi ya ushabiki wa kidini ambayo huangalia tu kuongezeka idadi ya waamini bila kujali ustawi wa malengo msingi ya kiimani yaani makuzi ya kiroho na kutunza amani, ukweli, haki na huruma. Leo hii kwa namna fulani, tunaona kuingiliwa kwa misingi ya kiimani na mambo ya kidunia. Watu ulimwengu huu wanatamani misingi ya kiimani iwe kama bendera inayofuta upepo wa mwendo wa dunia. Tuliombee Kanisa kusudi libaki aminifu katika kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na kuongozwa nayo.

Moja ya maeneo ambayo yanapotoshwa na upepo wa kidunia na kuharibu maana yake ya kiroho ni maisha ya ndoa. Ujumbe anaoutoa Mtakatifu Paulo katika Somo la pili juu ya utii na upendo kama misingi katika maisha ya familia huwa unageuzwa mara nyingi ili kutoa auheni za kidunia hata kama huaribu makusudio ya kiroho. Tunashuhudia leo hii jinsi ambavyo dhana ya upendo na utii inavyochakachuliwa. Watu wengi wanatafuta kuhalalisha madai ya uhuru na usawa si kadiri ya namna ya kiroho bali katika mivuto na vionjo vya kibinadamu. Matokeo yake ni kuvunjika kwa ndoa nyingi. Sasa tujiulize, nini maana ya uhuru au usawa katika namna ya kiroho? Je, utii katika namna ya kiroho humfanya mmoja kuwa mtwana na mwingine mtumwa? Je, dhana ya upendo inaeandana vipi na usawa wa kweli?

Neno la Mungu limeweka wazi kwamba yote yafanyike katika namna ya “kunyenyekeana katika Kristo”. Fumbo la Msalaba linatufundisha maana hiyo ya kuonesha utii na upendo katika namna ya uhuru kamili. Hii ni namna ya kuifuata njia ya Kristo, yaani kusikiliza sauti yake katika maisha ya familia. Utii na upendo ndani ya familia unapaswa kupata msingi wake katika Kristo. Katika maisha ya familia ya mwanadamu, iliyo kitovu cha maisha ya undugu, tunapaswa kumfuata Kristo. Maarifa na ujuzi wa kiulimwengu hutulazimisha kuamisha mawazo yetu kutoka huko na matokeo yake huwa ni kuharibu familia. Jamii ya leo imekuwa mwalimu na muelekezaji wa familia ya mwanadamu lakini imempeleka katika maangamizi. Mwaliko wa Yoshua katika somo la kwanza pia unapata nafasi hapa. Familia ya mwanadamu inaulizwa njia ya kufuata: je! Ni kusikiliza sauti ya Dunia na kuendelea kuiharibu familia aua kuisikiliza sauti ya Kristo inayotupeleka katika maisha ya uzima wa milele?

Tuyapokee maelekezo ya Mungu katika namna ya kiroho ili kuupata uzima wa milele. Tutatumbue daima kuwa Neno la Mungu litasimama na yote yanapaswa kujielekeza katika matakwa ya neno hilo. Tutalielewa neno hilo la uzima pale tutakapoungana na Mungu katika namna ya kiroho kwani “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu.”

 

24 August 2018, 16:28