Vatican News
Sr. Maria Veronica Alfonce Mwanandenga, aweka nadhiri za daima, mwanzo wa mapambazuko mapya ya maisha ya kitawa. Sr. Maria Veronica Alfonce Mwanandenga, aweka nadhiri za daima, mwanzo wa mapambazuko mapya ya maisha ya kitawa.  (2018 Getty Images)

Sr. Maria Veronica Alfonce Mwanandenga aweka nadhiri za daima

Sr. Maria Veronica Mwanandenga kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania, tarehe 2 Agosti 2018 kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu, ameweka nadhiri zake za daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 22 Agosti 1822, huko Lione, nchini Ufaransa, yaani miaka 196 iliyopita, Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu lilipoanzishwa rasmi na kuanza hija ya kujichotea neema na baraka ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa. Watawa wa Shirika hili wanapania kuwashirikisha watu wa Mungu, upendo na huruma inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Wanapolala kifudifudi kwa ajili ya kuabudu, wanaamka wakiwa wamisionari tayari kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Huu ni wito ambao unafumbatwa katika maisha ya sala, upendo kwa Mungu na jirani; tafakari ya kina na majitoleo ya dhati kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha!

Baada ya tafakari ya kina hatimaye, Sr. Maria Veronica Mwanandenga kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania, tarehe 2 Agosti 2018 kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliweka nadhiri zake za daima. Ibada imeongozwa na Padre Mario Laurenti, Paroko wa Parokia ya “Divin Maestro” Jimbo kuu la Roma. Sr. Caterina Micali, mjumbe wa kitume, amepokea nadhiri za Sr. Selela Mwanandenga kama anavyofahamika na wengi Jimboni Mbeya. Sr. Maria Veronica, mwanzoni mwa Ibada ya Misa ameonesha nia yake ya kutaka kujisadaka kwa kuweka nadhiri za daima katika Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwani kwa njia ya neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu amegundua ndani ya Shirika hili furaha ya Injili na umuhimu wa kujisada maisha yote kwa ajili ya Mungu. Ndiyo maana anaomba kuweka nadhiri za daima katika Shirika hili, kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma kwa Kanisa.

Padre Mario katika mahubiri yake, amekazia kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu kama dira na mwongozo wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kila wanalofikiri na kutenda lipate asili na hitimisho lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini, kwa bahati mbaya katika ulimwengu mamboleo watu wanataka kufikiri na kutenda bila kumhusisha Mwenyezi Mungu, kwa kudhani kwamba, wanajitosheleza na wala hakuna kile wanachopungukiwa. Amewataka waamini kujivika fadhila ya unyenyekevu, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwainua na hivyo kuonesha utukufu wake hata katika mambo ambayo kwa macho ya kibinadamu yanaonekana kuwa ni dhaifu sana!

Utukufu wa Mungu unajionesha kwa namna ya pekee kabisa, katika udhaifu wa mwanadamu. Ni kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, hata Mitume waliokuwa wavuvi, wadhambi na watu wa kawaida kabisa, lakini, waliweza kutenda makubwa na leo hii Habari Njema ya Wokovu imeenea sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa kwa asili ni takatifu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa lina asili ya kibinadamu kwa sababu linaongozwa na kusimamiwa na binadamu ambao wana karama na mapungufu yao; ni watenda dhambi wanaohitaji toba na wongofu wa ndani.

Hata katika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, anasema Padre Mario, utukufu wa Mungu utajionesha katika maisha na utume wa Sr. Maria Veronica Mwanandenga. Jambo la kuzingatia ni kutambua kwamba, utakatifu ni mchakato endelevu ulioanzishwa kwa Sakramenti ya Ubatizo na sasa unaendelea kuimarishwa kwa njia ya nadhiri za daima. Sr. Veronica atambue udhaifu wake na kwamba, ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni chombo cha huruma na upendo kwa watu wake, ili aweze kushiriki katika kuandika na kupamba kurasa za ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Kwa mikate mitano na samaki wawili, Yesu aliweza kuwalisha watu zaidi ya elfu tano. Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda miujiza kwa kutumia: karama na mapaji; uhuru na sadaka ya maisha inayogeuka kuwa ni sehemu ya ushiriki wa kazi kubwa ya ukombozi. Kwa kutambua yote haya, Sr. Veronica ataweza kutambua: Ukuu, utakatifu, wema, huruma na upendo na hivyo kumsaidia katika mchakato wa ukamilifu na utakatifu wa maisha.

Sr. Maria Veronica Mwanandenga baada ya kusikiliza wosia huu, akaweka nadhiri zake za daima yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili, mintarafu Katiba ya Shirika la Masista Waabuduo Moyo Mtakatifu wa Yesu, na kwamba, sasa anataka kujisadaka maisha yake yote kwa ajili ya Mungu na jirani. Akapewa alama za Shirika: Msalaba kama kielelezo cha agano na uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Biblia Takatifu, dira na mwongozo wa maisha; Mshumaa, mwanga wa Kristo Mfufuka.

Baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Mwishoni mwa Ibada ya Nadhiri za Daima, Padre Mario Laurenti alitoa baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Sr. Maria Veronica kwa kuweka nadhiri za daima. Amemwombea neema ili aendelee kutekeleza wito wake kwa moyo wa ukarimu na furaha ya ndani; kwa kujisadaka kwa Mungu na Kanisa. Sr. Maria Veronica Mwanandenga, a.k.a. Sr. Selela amewashukuru wote waliofika kumtia shime katika Ibada ya kuweka Nadhiri za daima.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

03 August 2018, 16:09