Tafuta

Papa Francisko alipokutana na vijana wa Italia, 12 Agosti 2018 Papa Francisko alipokutana na vijana wa Italia, 12 Agosti 2018 

Vijana ni matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake!

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema, Ibada ya Misa Takatifu ni kilele cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha lakini zaidi kwa ujana wao! Amewashukuru na kuwapongeza vijana kwa ari, ujasiri na moyo mkuu hadi kufika kwenye Mlima wa Bwana, kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baada ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa Siku ya Vijana Italia, kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” ulioko Roma, amedadavua kuhusu: changamoto ya kuunda utambulisho wa mtu binafsi na utekelezaji wa ndoto za maisha ya ujana katika uhalisia wake! Pili ni kuhusiana na mang’amuzi ya maisha, dhana ya sadaka na uwajibikaji katika ulimwengu wa vijana. Tatu, vijana wamegusia kuhusu imani na maana ya maisha! Ametoa shukrani kwa ushuhuda wa imani;akajikita katika umuhimu wa kutoka kwa haraka ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu; Ushuhuda wa imani ili kwa kuona waweze kuamini na kwamba, vijana wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, tarehe 12 Agosti 2018, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Italia, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na bahari ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia na kuwakumbusha kwamba, vijana wanapothubutu kukutana na Kikristo Yesu anawapatia siri ya maisha mapya. Ibada hii ya Misa Takatifu ni kilele cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha lakini zaidi kwa ujana wao! Amewashukuru na kuwapongeza kwa ari, ujasiri na moyo mkuu hadi kufika kwenye Mlima wa Bwana, kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya.

Hija ya maisha ya mwanadamu imesheheni: furaha, matatizo na changamoto za maisha, ambazo zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya umoja na mshikamano kama ulivyoneshwa na vijana wakati wa hija yao kuelekea mjini Roma. Vijana wasiwe na wasi wasi kwani Mwenyezi Mungu atawatumia Malaika wake mlinzi ili aweze kuwaongoza katika safari ya maisha, ikiwa kama watamtumainia. Vijana wengi hawana fursa za ajira, baadhi yao wanatoka kwenye familia zenye kinzani na migogoro; shida na changamoto zinazoendelea kuikumba Italia kwa wakati huu; mambo ambayo pengine yanaweza kuwafanya kujisikia kana kwamba, si mali kitu, kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya aliyetaka “kubwaga manyanga” na kutokomea kusikojulikana!

Kardinali Bassetti anasema, hata leo hii kuna watu wanakimbia nchi zao kutokana na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, kinzani, dhuluma na nyanyaso, hata katika magumu ya maisha kama haya, Mwenyezi Mungu bado anaonesha huruma na upendo kwa waja wake. Duniani kumejaa rasilimali na utajiri mkubwa ambao ungeweza kutosheleza mahitaji msingi ya binadamu, lakini kutokana na ubinafsi na uchoyo, kuna baadhi ya watu wanateseka. Changamoto kwa vijana ni kujenga utamaduni wa ukarimu wa upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Pale vijana wanapojisikia kukata tamaa na kuishiwa nguvu kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya, wakimbilie katika huruma na upendo wa Mungu, kwani atawakirimia nguvu na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Vijana wajitahidi kumtafuta Mungu katika maisha yao, kwani anawafahamu fika, Yesu awe ni lengo na mwandani mwa maisha yao! Vijana warutubishe maisha kwa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na sala ili waweze kuwa na ujana uliotukuka na unaong’ara kama nyota ya asubuhi, chachu ya matumaini kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

12 August 2018, 15:00