Tafuta

Vatican News
Uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM. Uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM. 

SECAM: Jubilei ya Miaka 50: Umoja, upendo na mshikamano

Waamini watambue kwamba, Msalaba wa Kristo ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na udugu unaoshuhudiwa katika maisha ya kijumuiya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Gabrieli Mbilingi, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, Jumapili, tarehe 29 Julai 2018 amezindua mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1969. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”.

Kilele chake kitakuwa ni mwezi Julai 2019. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika utangulizi uliotolewa na Askofu mkuu John Baptist Odama, Rais wa Baraza amesema, Uganda ina nafasi ya pekee kabisa katika historia na maisha ya Kanisa Barani Afrika! Hapa ni chemchemi ya mashuhuda wa imani, waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hapa ni mahali ambapo Mwenyeheri Paulo VI aliasisi SECAM. Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM iwe ni fursa ya kuimarisha maisha na utume wa SECAM, kama chombo cha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu Barani Afrika.

Kwa upande wake, Askofu Emmanuel Badejo, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, CEPAS, akifafanua kuhusu Neno la Jubilei, anasema, SECAM, imekazia zaidi: umoja wa familia ya Mungu Barani Afrika unaopaswa kujengwa na kushuhudiwa kwa njia ya utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; upendo na mshikamano; mambo msingi yanayowatambulisha waafrika, sehemu mbali mbali za dunia. Licha ya tofauti zao msingi, familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kushikamana katika imani, matumaini na mapendo.

Waamini watambue kwamba, Msalaba wa Kristo ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na udugu unaoshuhudiwa katika maisha ya kijumuiya. Waamini walioko ndani na nje ya Bara la Afrika wanawakilishwa barabara na kwamba, kila mwamini anapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa na familia ya Mungu Barani Afrika, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni fursa kwa waamini kujikita katika nchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar wamepewa sala ambayo waamini wataitumia katika kipindi cha mwaka mzima: kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya wamisionari wa kwanza waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni sala ya toba na wongofu wa ndani, ili kuomba huruma na msamaha wa Mungu kutokana na dhambi na mapungufu ya kibinadamu yaliyojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kutokana na utawala mbaya, rushwa na ufisadi, vita na mipasuko pamoja na kushindwa kutumia vyema vipaji na rasilimali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni sala ya kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia ari, nguvu na moyo wa kutubu na kumwongokea Mungu; ili kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika, ili kweli waamini waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Kristo na Kanisa lake. Bikira Maria Malkia wa Afrika, Watakatifu wote wa Afrika na Mashahidi wa Uganda, waiombee familia ya Mungu Barani Afrika.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

02 August 2018, 14:27