Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, Maaskofu mahalia wanawajibu wa kimaadili kuwalinda watu wao Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, Maaskofu mahalia wana wajibu wa kimaadili kuwalinda watu wao.  (AFP or licensors)

Maaskofu mahalia wanawajibu wa kimaadili kuwalinda watu wao

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, viongozi wa Kanisa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kimaadili ni kosa kubwa, dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Makosa ya nyanyaso za kijinsia hayana budi kushughulikiwa mara moja kadiri ya sheria kanuni na taratibu zilizowekwa na kamwe kusiwepo na matumizi mabaya ya madaraka

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani ametoa tamko linaloonesha hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na Kanisa pale ambapo itabainika kwamba, Askofu mahalia ameshindwa kuwajibika kimaadili kuwalinda watu wa Mungu dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Hii inatokana na ukweli kwamba, nyanyaso za kijinsia zinasababisha uchungu, hasira na aibu kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kumbe, Maaskofu mahalia wanapaswa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, wanachukua hatua madhubuti kuwalinda watu wa Mungu katika maeneo yao dhidi ya nyanyaso za kijinsia, kwani madhara yake kwa sasa ni makubwa licha ya kwamba, pengine matukio kama yalitendwa miaka kadhaa iliyopita! Kardinali DiNardo ametoa tamko hili kufuatia hatua iliyochukuliwa na Askofu mkuu mstaafu Theodore McCarrick za kujivua heshima ya Ukardinali kutokana na tuhuma za nyanyaso za kijinsia dhidi yake.

Viongozi wa Kanisa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kimaadili ni kosa kubwa, dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Makosa ya nyanyaso za kijinsia hayana budi kushughulikiwa mara moja kadiri ya sheria kanuni na taratibu zilizowekwa na kamwe kusiwepo na matumizi mabaya ya madaraka. Askofu mkuu mstaafu McCarrick atashughulikiwa kadiri ya Sheria kanuni na taratibu za Kanisa na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaendelea kupembua kwa kina na mapana hatua ambazo zinastahili kuchukuliwa dhidi ya kiongozi wa Kanisa anayeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kimaadili.

Kardinali Daniel N. DiNardo, kwa sasa anapenda kukazia mambo makuu yafuatayo: Maaskofu mahalia wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanatenda kwa huruma, busara na haki, kwa wakleri watakaoshutumiwa kujihusisha au kuhusishwa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia, pamoja na kuwasindika katika kipindi hiki kigumu. Anawaalika wale wote waliotendewa nyanyaso za kijinsia kujitokeza mara moja na kwa vile matukio kama haya ni kesi za jinai, kumbe, vyombo vya sheria vinapaswa kushirikishwa kikamilifu. Tatu, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limepania kutafuta ukweli kuhusu shutuma za nyanyaso za kijinsia zinazomkabili Askofu mstaafu McCarrick. Nne, toba na wongofu wa ndani ni muhimu sana, ili kuweza kurejesha tena uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu. Kanisa nchini Marekani linateseka sana kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Makosa yaliyopita, yawe ni fundisho kubwa kwa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

01 August 2018, 14:14