Tafuta

Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba anatufundisha juu ya Sayansi ya Msalaba. Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba anatufundisha juu ya Sayansi ya Msalaba. 

Mt. Theresa Bernadetha: Sayansi ya Msalaba

Sayansi ya Msalaba inatuonesha njia ya kufikia uzima wa milele kwa kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kristo alikubali kufa Msalabani kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu na kujifunua kwetu kama njia ya kutufikisha kwenye uzima wa milele. Ametuachia Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi kama chakula na kinywaji cha maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Joseph Peter Mosha. – Vatican.

Mpendwa, “Kristo alijivika katika nafsi yake nira ya sheria yote (haya ni mapenzi ya Mungu), akiifuata na kuitimiza kikamilifu, hadi kufa kwa ajili ya sheria na kuwa mhanga wa sheria”. (Edith Stein Werke, I, Freiburg in Br. 1983, 15 – 16). Nukuu hii kutoka maandishi ya Mtakatifu Theresa Benadetha wa Msalaba (Edith Stein) yanatufunulia sayansi ya msalaba wa Kristo ambayo inafungwa na tendo moja: “kuyatimiza mapenzi ya Mungu”. Wafuasi wa Kristo hushiriki kifo chake kwa ubatizo (Rum 6:3) na kuyarandanisha maisha yao na msalaba wa Kristo kwa kuifia dunia, yaani kuachana na mambo mafu na kuwa hai katika Mungu. Tarehe 9 Agosti 2018, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba.

Sayansi ya Msalaba inatuonesha njia ya kufikia uzima wa milele. Njia hiyo ni kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kristo alikubali kufa Msalabani kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Kristo amejifunua kwetu kama njia ya kutufikisha katika uzima wa milele. Kisha akatuachia Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi kama chakula cha kiroho kwa ajili ya kuupata uzima wa milele. Kristo anatuambia kuwa uzima wa milele ni “kumwamini Yeye aliyetumwa na Yeye” (Yoh 6:29). Huku ndiko kujiweka katika mafundisho ya Kristo na kuyaamini. Namna hiyo ndiyo inatupatia uzima wa milele. Kristo amehitimisha mafundisho yake hayo kwa sadaka ya kifo chake Msalabani, sadaka ambayo tunaiadhimisha kila tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu. Hivyo Ekaristi Takatifu inatufunulia kwetu sayansi ya Msalaba wa Kristo na kuwa kwetu chachu na nguvu ya kila siku kwa ajili ya kuyatafuta mafundisho yake na kywashika.

Ni njia ambayo inatupatia uhuru wa kweli. Uhuru wa kweli unapatikana pale mmoja anapokuwa tayari kujivua kongwa la utumwa wa ulimwengu huu na kuwa huru kweli kweli katika Kristo. Uhuru anaotuletea Kristo ni uhuru wa wana wa Mungu. Hadhi hii ya kuwa wana inatuonesha kuwa uwepo wetu hapa duniani si jambo la kujiamulia binafsi. Hakuna anayeweza kuwa mwana bila kuzaliwa. Hivyo kwa kuwa wana ina maanisha tumeoka mahali fulani na wapo walitutangulia; zipo taratibu na kanuni amabazo zimeufanya uwepo wangu. Uhuru wangu kama mwana unajizingirisha katika kanuni na taratibu hizo na kamwe hautoki katika maamuzi binafsi. Dhambi imefanya juhudi ya kumwondoa mwanadamu katika mrengo huo na matokeo yake ameingia katika utumwa wa visanamu vya ulimwengu wa leo. Sayansi ya Msalaba inatuondoa katika visanamu hivyo na kutuvika utu wetu halisi wa kuwa huru katika Kristo.

Kifo cha Msalaba kinatuelekeza katika kukubali kuonekana umekufa katika ulimwengu huu lakini kuwa hali katika Mungu. Utii wetu kwa matakwa ya Injili, ambayo inajumuisha maisha yote ya Kristo katika kujivika na kuishika sheria ya Mungu kikamilifu, huonekana mara nyingi ni kituko mbele ya macho ya ulimwengu. Ni kweli tunaonekana tuepitwa na wakati na wakati mwingine tunavutwa kufuata matakwa ya dunia. Sayansi ya Msalaba inatupatia ujasiri wa kuufanya ulimwengu uitii sauti ya Mungu. Ni nguvu kwetu kupitika katika maswahibu yote ya kuchekwa, kudharauliwa na kuonekana kituko katika jamii lakini tunatumaini kwa utii wetu kufika katika uzima wa milele.

Fumbo la Kanisa linaendelea kuifanya sadaka ya Kristo kuwa hai siku zote. Kwa njia ya fumbo hili matakatifu huadhimishwa na Neno la Mungu hutangazwa kama nyenzo za kutukumbusha kuunganika na mapenzi ya Mungu. Jamii hii ya waamini ni Sakramenti ya wokovu na kwa njia yake wengi huvutwa na kukombolewa katika Kristo. Chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu Kanisa limeendelea kuangazwa na kuongozwa katika kweli na hivyo kuwa chombo maalum mahsusi katika jamii ya mwanadamu leo hii cha kutuferejishia uzima wa milele. Muunganiko wetu na jamii hii ya kimbingu hapa duniani unatudai kuitambua nafasi yetu kama wana wa Mungu, kutuimarisha katika umoja wa kindugu katika Kristo, kutuweka tayari kuisikiliza sauti ya Kristo na mwisho kuzaa matunda yanayoleta uzima wa milele. Sayansi ya Msalaba inaendelezwa na maadhimisho mbalimbali ndani ya Kanisa na kuimarishwa na umoja wa wana Kanisa.

Sayansi ya Msalaba ni mwarobaini kwa changamoto mabalimbali za kiulimwengu. Katika ujumla wake sayansi hii inatuunganisha na Mungu na kutupatia uhuru wa wa kweli wa wana wa Mungu. Changamoto nyingi za kiulimwengu ni zao la kumweka Mungu pembeni mwa maisha. Mwanadamu anajiweka kana kwamba yeye ndiye chanzo cha yote na anaweza kutumia yote kadiri anavyojisikia yeye. Uhuru huu bandia hutia ndimu hamu ya kutaka kutimiza hisia binafsi za mtu hata kama zinapingana na ukweli ambao ni sheria ya Mungu.

Leo hii tunashuhudia upotoshwaji mkubwa wa mahusiano ya kijinsia. Mwanadamu anajiendeshea mambo haya kama anavyojisikia mwenyewe. Jamii ya mwanadamu inahalalisha mahusiano kinyume na matakwa ya Mungu na wakati mwingi inalielekeza Kanisa, jamii ambayo inaukumbatia msalaba kuendana na mambo hayo. Familia ya mwanadamu ianapata athari kubwa na matokeo yake ni uharibifu wa tunu ya utu. Tunu hii hupata mbolea na virutubisho ndani ya familia. Sasa tutawezaje kuona ustawi wake katika jamii inayoitupilia mbali tunu hii?

Katika ulimwengu wa kiuchumi mwanadamu amekamatwa na tamaa ya utajiri. Kila mmoja anatafuta kujilimbikizia mali na fedha. Thamani ya utu wa mwanadamu haionekani tena katika utu bali katika mali. Umoja wa kindugu unafafanuliwa na matabaka ya matajiri na maskini. Mmoja anakuwa Mwananchi kweli kweli pale anapokubaliana na taratibu za kiuchumi na kutokuigusa misingi yake hata kama inapingana na sheria ya Mungu. Matokeo yake ni ubinafsi uliopitiliza na kujenga matabaka ya wachache walio nacho na wengi wasio nacho. Pia tunaingia katika utamaduni wa kifo na kutupa vitu hivyo bila kujali uthamani wake kwa wengine wasio nacho.

Sayansi ya Msalaba inatufunulia upendo wa Mungu ambao msingi wake umejikita katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Upendo huu unapopotea huingia matamanio ya mwanadamu. Hivyo matokeo yake huwa ni chuki, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu pamoja na kuwatumbukiza wengine katika utumwa mamboleo, kwa ajili ya kupata mafanikio chapuchapu, uchu wa mali na madaraka, mambo yanayokinzana na umoja, upendo na udugu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

09 August 2018, 15:28