Kanisa Katoliki linaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agostino wa Hippo kila ifikapo tarehe 28 Agosti Kanisa Katoliki linaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agostino wa Hippo kila ifikapo tarehe 28 Agosti 

Mtakatifu Agostino:Usadiki ili uelewe,halafu uelewe ili usadiki!

Tarehe 28 ya kila mwaka Kanisa linamkubuka Mtakatifu Agostino wa Hippo , Padre, Askofu na mwalimu wa Kanisa ambaye katika maisha yake amefanya mengi. Anakumbukwa sana katika uongofu wake, na urithi wa barua nyingi zenye ushuhuda wa upendo kwa Bwana.Yeye anathibitisha, si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mdhambi.

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Tarehe 28 Agosti Kanisa linaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Agostino,  Mwalimu wa Kanisa. Mtakatifu Agostino wa Hippo alizaliwa huko Thagaste, leo mji huo unaitwa Souk Ahras nchini Algeria, kunako tarehe 13 Novemba mwaka 354  na mauti yakamfikia kunako tarehe  28 Agosti, 430. Yeye alikuwa mtawa, mwanataalimungu, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Ujana wake: Wakati wote wa ujana alifuata anasa na uzushi, bila kujali machozi ya mama yake. Alipata elimu yake nzuri ya lugha na ya ufasaha wa kuhubiri huko Thagaste, Madaura na hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis) ingawa hakuwa daima mwanafunzi mzuri, mbali ya kuwa na akili ya pekee. Alimudu kikamilifu Kilatini, lakini si sana Kigiriki. Akiwa huko Karthago, mwaka 373 alisoma kitabu cha maadili cha Sisero ambacho kilibadilisha hisia zake hivi kwa maana hiyo anasema,“matumaini yote ya bure yakawa hayana maana kwangu, nikatamani hekima isiyokufa kwa ari isiyosemeka moyoni mwangu”. Lakini kwa kuamini ukweli haupatikani pasipo Yesu, ambaye hatajwi katika kitabu hicho, alianza kusoma Biblia, ila hakupenda tafsiri ya Kilatini wala yaliyomo, akiyaona tofauti na mtindo wa falsafa inayotafuta ukweli. Hivyo alisogea mbali na dini iliyoonekana kutotia maanani hoja za akili ambayo pamoja na imani ndizo “nguvu mbili zinazotuongoza kwenye ujuzi”. Ndivyo alivyoandika baadaye, akitoa pia kauli mbili za msingi kuhusu kulenga ukweli: “Usadiki ili uelewe”, halafu “uelewe ili usadiki”.

Hapo, kusudi asiishi bila Mungu, alijitafutia dini ya kuridhisha hamu yake ya kujua ukweli na ya kuwa karibu na Yesu, akajiunga kwa karibu miaka 10 na Umani. Dini hiyo ilidai kufuata akili na kufafanua sababu ya mabaya kuwepo duniani kutokana na chanzo cha pili cha ulimwengu kilicho kinyume cha Mungu, ikikataa Agano la Kale ili kufuata Ukristo wa kiroho. Augustino alipenda pia maadili ya dini hiyo kwa sababu yalikuwa yanawadai sana baadhi ya waumini tu, yakiwaacha wengine wote wasijali zaidi. Hatimaye Wamani walikuwa wanasaidiana kupanda chati katika jamii. Lakini alipokutana na askofu wao Fausto, alikosa imani nao kwa kuona alivyoshindwa kujibu maswali yake.

Wongofu na ubatizo: Uongofu wake ulitimia kunako tarehe 15 Agosti 386, akiwa na umri wa miaka 32, aliacha kufundisha na hata kuishi na mama mtoto, akaenda kwa muda Cassiciaco karibu na ziwa la Como nchini Italia , akiwa na Monika, Adeodatus na marafiki wachache, akarudi Milano alipobatizwa na Ambrosi pamoja na mwanae na rafiki yake Alipio usiku wa Pasaka ya mwaka 387. Baada ya kubatizwa hatimaye na kunuia akaishi kitawa Thagaste, alirudi Afrika; lakini akiwa njiani, huko Ostia, bandari ya Roma, mama yake Monika akafa. Ndoto yake ilikuwa kujitosa katika maisha ya sala na masomo pamoja na marafiki wake. Lakini hiyo ilidumu miaka mitatu tu.

Padri na askofu : Mwaka 391 bila kutarajia alipewa daraja ya upadri huko Hippo, alipoanzisha monasteri, akigawa muda wake kati ya sala, masomo na mahubiri, halafu mwaka 395 akachaguliwa kuwa askofu msaidizi wa mji huo na mwaka 397 akawa askofu wa jimbo hilo. Ilimbidi akubali matakwa ya Mungu kwake, kwamba ajitoe kwa wengine na kuwashirikisha ujuzi wake ili kuishi kweli kwa ajili ya Kristo. “Kuhubiri mfululizo, kujadili, kusisitiza, kujenga, kuwa tayari kwa yeyote ni jukumu kubwa sana, ni mzigo mzito, ni juhudi ya ajabu”. Ilikuwa kama wongofu wake wa pili. Hapo alitegemeza maskini na mayatima, alisimamia malezi ya wakleri, akiwadai waishi pamoja, akaeneza monasteri za kiume na za kike. Alifanya adhimisho la ekaristi kuwa kiini cha maisha ya jumuia zake. Mahubiri yake mengi yanaonyesha alivyojua kujadiliana na umati akitumia maneno rahisi na ya kawaida na hata ucheshi katika kulinganisha Neno la Mungu na mazingira yao. Kwa tabia yake karimu na pendevu, hisia zake, uvumilivu na utayari wa kusamehe alifanya hata maadui kadhaa kuwa marafiki. Maisha yake ya Kiroho yaliyoongoza uandishi wa kanuni yake kwa watawa yamefuatwa na mashirika mengi ya kiume na ya kike hadi leo.

Kwa miaka 35 mpaka kifo chake, mbali na kutimiza majukumu yake mengi, aliendelea kueleza na kutetea imani sahihi ya Kikristo kwa mahubiri, maandishi na vitabu vingi sana (hata vya mitindo mipya) dhidi ya aina zote za uzushi za wakati ule: Wamani, Wadonati, Wapelaji na Waario. Hivyo tangu alipokuwa hai, hakuongoza Kanisa la Afrika Kaskazini tu, bali alitegemeza imani kila mahali. Kwa njia hiyo amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo, hasa wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na katika Uprotestanti uliotokea katika Kanisa hilo. Kwa mfano Martin Luther alimtaja kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mtume Paulo). Augustino alijilisha tunu za Kikristo na kutokeza utajiri wake wa dhati, akibuni mawazo na mifumo ya kulisha vizazi vijavyo. Hata nakala za vitabu vyake ni nyingi sana, zikithibitisha vilivyopendwa na kuenea. Hivyo aliathiri sana ustaarabu wa Magharibi unaozidi kuenea leo duniani kote. Mawazo yote yaliyomtangulia yanakutana katika maandishi yake na kuwa chemchemi ya mafundisho kwa nyakati zilizofuata.

Miaka ya mwisho: Tarehe 26 Septemba 426 alikusanya waamini ili kuwatambulisha padri Eraklio aliyemchagua kama mwandamizi wake naye aweze kutumia miaka yake ya mwisho katika kusoma kwa dhati zaidi Maandiko matakatifu. Watu walimkubalia kwa shangwe. Miaka minne iliyofuata Augustino alifanya kazi kubwa kwa kumaliza vitabu mbalimbali na kuanza kuandika vingine. Kati ya vile vya wakati huo kuna “Retractationes” (yaani “Kupitia Upya” vile vilivyotangulia), ambamo tunaona unyofu wake kwa kuwa tayari kurekebisha baadhi ya mafundisho aliyowahi kuyatoa. Hivyo mpaka mwisho alionyesha alivyolenga ukweli kuliko yote.Pia miaka hiyo alijadiliana na wazushi hadharani na kurudisha amani iliyohatarishwa na makabila ya kusini yakifaidika na matatizo kati ya Kaisari na jemadari wake Bonifasi. Alimuandikia mpatanishi: “Ni utukufu mkubwa zaidi kuzuia vita vyenyewe kwa neno moja, kuliko kuangamiza watu kwa upanga, na vilevile kusababisha au kudumisha amani kwa amani kuliko kwa vita. Kwa sababu wanaopigana, ikiwa ni watu wema, bila shaka wanalenga amani, ila kupitia damu. Kumbe kazi yako ni kuzuia umwagaji damu”.

Hata hivyo, tumaini lilitoweka Bonifasi alipoalika kwa hasira washenzi wa Kijerumani walioitwa Wavandali kutoka Hispania wavamie Afrika. Agostino aliaga dunia akiwa Hippo tarehe 28 Agosti 430, wakati Wavandali walipokaribia kuteka mji wake baada ya kuuzingira miezi mitatu, huku wakibomoa makanisa na nyumba za vijijini na kuua au kukimbiza wakazi, wakiwemo watawa. Baadhi waliteswa na kuchinjwa, wengine walibakwa au kufanywa watumwa. Mbele ya maovu hayo yaliyokomesha ustaarabu wa Kirumi, Augustino alizidi kutafakari fumbo la Maongozi ya Mungu ili kujifariji na kuwatuliza wengine kama alivyofanya miaka 20 ya nyuma, Roma ilipotekwa kwa mara ya kwanza na Wagoti. Aliona ustaarabu huo ulikuwa umechakaa, kumbe Kristo tu hazeeki kamwe na ni wa kutegemewa. Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5. Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake bora, tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa. Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Anakumbukwa sana katika suala la Dhambi na neema: Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao. Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi. Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa. Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho. Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu. Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki. Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki.

Sala zake zimekuwa ni mwanga mkuu kwa kila mmoja mwenye kujikita katika hija ya Bwana kwa: Wewe Bwana ni mkuu na unastahili kabisa sifa. Uweza wake ni mkuu na hekima yako haina mipaka. Mtu anataka kukusifu, yeye aliye sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, yeye anayetembea akielekea kifo, ushahidi wa dhambi yake, wa kwamba wewe unapinga wenye kiburi. Hata hivyo mtu, sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, anataka kukusifu. Wewe unamchochea aonje furaha ya kukusifu, kwa kuwa umetuumba kwa ajili yako, na moyo wetu hautulii mpaka ustarehe ndani mwako. Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto! Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia. Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako. Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.

Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka: Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako. Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako. Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako.

Historia yake na maandiko yake ni ya kusisimua sana  na kuvutia kuendelea kumtafuta Bwana kila wakati, kwa utambuzi wa kuwa sisi sote ni wadhambi, na kukumbuka ushuhuda wake kwamba hatutaweza kabisa kutulia , hadi tunapumzika ndani mwake Yeye...!

28 August 2018, 12:40