Tafuta

Kardinali Polycarp Pengo amewataka Mashemasi wapya wa C.PP.S. kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kardinali Polycarp Pengo amewataka Mashemasi wapya wa C.PP.S. kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. 

Kardinali Pengo awataka Mashemasi wapya kujisadaka kwa Kristo!

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania ametoa Daraja ya Ushemasi kwa Wamisionari watano wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Katika wosia wake, amewatia shime Mashemasi kumtumikia Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza.

Na Padre Stephano Furaha Karabyo, C.PP.S., Rodrick Minja na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu Ushemasi anasema, Mashemasi ni watumishi na mitume wa Kristo wanaotumwa kumtangaza na kumshuhudia Yesu kwa njia ya huduma ya mapendo katika: Neno, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Daraja yao, lakini zaidi katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kristo Yesu amejifunua kama Neno wa Baba wa milele ambaye amekuja kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, akawa ni chemchemi ya furaha na huduma kwa wote, yaani akawa Shemasi.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa kwa watangazaji na wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu kuhakikisha kwamba, wanafuata kikamilifu maagizo ya Kristo Yesu. Ikumbukwe daima kwamba, dhamana ya uinjilishaji ni kwa Wakristo wote na huduma ya upendo ni njia muafaka ya kumwilisha utume wa kumfuasa Yesu, kielelezo cha ushuhuda wa maisha yanayojikita katika huduma. Maisha ya huduma yanapaliliwa kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na kufunga kama njia ya kurekebisha vilema na mapungufu katika maisha!

Ili kuwa kweli ni watumishi wema na waaminifu, kuna haja ya kujikita katika dhana ya uwepo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya zawadi ya huduma kutoka kwa Mungu inayotolewa kama sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawataka Mashemasi kuwa wazi na tayari daima kutoa huduma inayobubujika kutoka katika fadhila ya unyenyekevu wa moyo, huku wakiendelea kushangazwa na Mungu katika maisha ya kila siku. Mtumishi mwema na mwaminifu anafahamu na kutambua dhamana, wajibu na nafasi yake, tayari kuhudumia hata wale wanaokuja kuomba msaada nje kabisa ya muda uliokubalika, kielelezo cha sadaka katika maisha. Kwa njia ya maisha ya kuwajibika, huduma ya Mashemasi itaweza kuzaa matunda ya Kiinjili.

Tarehe 8 Agosti 2018 katika Kanisa la Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Jimbo kuu la Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Dominico Guzman, mtumishi mwaminifu wa Kristo na Kanisa lake, mfano bora wa kuigwa katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo kati ya watu wa Mataifa, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania ametoa Daraja ya Ushemasi kwa Wamisionari watano wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Katika wosia wake, amewatia shime mashemasi kumtumikia Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza, kwani kamwe hataweza kuteseka zaidi kuliko alivyoteseka Kristo Yesu na hatimaye, kufa Msalabani.

Kardinali Pengo amewataka Mashemasi kuhakikisha kwamba, matizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazowajia mbele yao, zinakuwa ni chachu ya kumwambata na kumfuasa zaidi Kristo Yesu katika maisha na utume wa Kikuhani. Kanisa Katoliki Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo. Lakini, kabla ya Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu kufika na kutua nanga ya matumaini ya Habari Njema ya Wokovu mjini Bagamoyo, kulikuwepo na Waarabu na dini yao ya Kiislam. Lakini kadiri ya mpango wa Mungu, kutoka Bagamoyo, Mlango wa imani, Ukristo ukaenea sehemu mbali mbali za Afrika Mashariki na Kati. Kumbe, Mashemasi wapya ni matunda ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, changamoto ni kuwa kweli vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania kitakuwa ni hapo tarehe 4 Novemba 2018 mjini Bagamoyo.

Mashemasi wapya ni: Bonaventura Mushi, Faustin Maganga, Godfrey Boge, Hillary Ngowi na Severin Hyera. Kabla ya kupewa Daraja Takatifu ya Ushemasi, Jumanne, tarehe 7 Agosti 2018 Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania aliwapokea rasmi Shirikani. Amemshukuru Mungu kwa zawadi ya wito kwa wanashirika hawa wapya na kuwataka waendelee kubaki waaminifu, wadumifu na wachapakazi ndani ya Shirika na Kanisa katika ujumla wake.

Wamisionari wapya wamekabidhiwa nyenzo za kazi: Katiba ya Shirika ili watambue dhamana na wajibu wao ndani ya Shirika pamoja na Msalaba, changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha damu katika maeneo yao ya kazi na utume. Mashemasi wapya waendelee kuchakarika katika kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha, kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya! Kwa hakika, Ndoto ya Mtakatifu Gaspar inaendelea!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

09 August 2018, 16:13