Tafuta

Ekaristi Takatifu ni masurufu ya njiani kuelekea uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni masurufu ya njiani kuelekea uzima wa milele. 

Nguvu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu

Naye alaye chakula cha mwili wa Kristo Yesu, kifo cha kimwili hakitakuwa kwake upotevu au hakitakuwa kuingia katika mateso ya Jehanum, bali kwake kifo cha kimwili kitakuwa ni mlango wa kuingia katika furaha ya uzima wa milele. Na hivi hatakufa bali ataishi milele.

Padre William Bahitwa. – Vatican.

UTANGULIZI: Kristo anasema “Mimi ndimi chakula lilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki ataishi milele” Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni dominika ya 19 ya mwaka B wa Kanisa. Tunaendelea kumtafakari Kristo mkate wa uzima na chakula kilichoshuka toka mbinguni kwa ajili yetu; kwa ajili ya kutupa nguvu katika safari ya maisha yetu hapa duniani na pia kuwa kwetu amana ya uzima wa milele.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (1 Waf. 19:4-8) Nabii Eliya baada ya kumdhihirisha Mungu wa kweli dhidi ya miungu Baali katika mlima Karmeli anatishiwa kuuwawa. Anakimbia kwenda kujificha jangwani, mahala pa ukiwa na upweke na kibiblia mahala ambapo mtu anakwenda kutafuta mang’amuzi mapya. Katika kipindi hicho Eliya anaona ameshindwa kutimiza matazamio ya utume wake wa kinabii. Anaona amefeli na amemwangusha Mungu. Hivyo anaomba afe tu. Eliya alikuwa ni mtumishi hodari na ni kati ya manabii waliokuwa na imani kubwa sana kwa Mungu na waliofanya vyema kazi yao ya unabii. Ni hapa tunaona maneno yale ya mtume Paulo “hata dhahabu hujaribiwa kwa moto”. Hata waaminifu wa Mungu hupatwa na majaribu na hupatwa na nyakati ngumu maishani. Hukata tamaa na hupata hisia za kushindwa. Lakini somo hili pia linatuonesha kuwa Mungu hawaachi milele waaminifu wake hao. Kwa njia ya malaika, Mungu anamletea Eliya msaada. Anamletea chakula kinachompa nguvu na kwa nguvu ya chakula hicho Eliya anaendelea kwa siku arobaini, yaani anapata nguvu ya kuendelea katika kipindi chote cha utume wake.

Somo la pili (Ef. 4:30-5:2) mtume Paulo anaendelea kuwapa mausia mbalimbali ya mwenendo mwema wakristo wa jumuiya ya Efeso, jumuiya ambayo ilikuwa na mwingiliano mkubwa wa watu kwa sababu za kibiashara. Paulo anatambua changamoto kubwa inayowakabili wao kama wakristo wapya wanaozungukwa na watu wengine wasio wakristo na walio na mwenendo tofauti nao. Na hii ni changamoto ya kushawishika kuacha mwenendo wao wa maisha na kuiga namna watu wa mataifa wanavyoenenda. Katika somo hili ambalo ni sehemu ya mausia hayo Mtume Paulo anawakumbusha kuwa wao kama wakristo wanaye ndani yao Roho Mtakatifu. Na Roho huyu wamempata kwa sababu ya upendo wa Kristo kwao.

Kristo amewapenda akajitoa kwa ajili yao kama sadaka na dhabihu ili kuwafanya wawe wana wapendwa wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyewajalia. Kwa jinsi hii, wakikengeuka na kuiga mitindo ya watu wa mataifa watakuwa wameusaliti uana wa Mungu na zaidi watakuwa wanamhuzunisha Roho Mtakatifu aliye ndani yao. Anasema mtume Paulo “wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”. Na kutoka hapa ndipo anawahimiza wazidi kuwa watu wa fadhili, wenye huruma na wanaosameheana kama vile Kristo naye alivyowasamehe.

Somo hili linaonesha hadhi ya juu aliyonayo mkristo dhidi ya yule asiye mkristo. Baba Mtakatifu Francisko huhimiza kutambua kuwa mtu aliyebatizwa si sawa na yule ambaye hajabatizwa. Kuna tofauti kubwa mno. Na tofauti hii ndiyo inayomfanya mbatizwa aoneshe hali ya juu ya mwenendo mwema katika maisha yake kulingana na hadhi yake ilivyo ya juu.

Injili (Yn. 6: 41-51) Yesu anaendelea kuwafundisha wayahudi kuwa yeye ndiye chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni kuwashibisha waisraeli jangwani katika safari yao kuelekea nchi ya ahadi Kanaani. Kusikia hivyo, Wayahudi wananung’unika. Katika lugha ya kibiblia kunung’unika si maana yake kusikitika au kuonewa bali kunung’unika ni neno linalotumiwa kuonesha hali ya kuwa na ugumu wa imani, kutokuamini. Kwa kiswahili cha siku hizi tungesema waliposikia hivyo “wakaguna mmmmh”. Akazidi Yesu kujipambanua kuwa Yeye ni chakula chenye uzima, sio kama kile walichokula baba zao wakafa, mtu akila chakula hicho ambacho ni Yeye mwenyewe, hatakufa bali atakuwa na uzima wa milele. Kristo anaonesha kuwa kama vile mwili usivyoweza kuishi bila chakula, ndivyo na roho ya amwaniye haiwezi kuishi bila Yeye. Naye alaye chakula cha mwili wake, kifo cha kimwili hakitakuwa kwake upotevu au hakitakuwa kuingia katika mateso ya Jehanum bali kwake kifo cha kimwili kitakuwa ni mlango wa kuingia katika furaha za milele. Na hivi hatakufa bali ataishi milele.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tukio la Nabii Eliya kama tulivyoliona katika somo la kwanza, ni tukio ambalo tunaweza kusema linatoa muhtasari wa yale ambayo karibu kila mwanadamu anayapitia maishani. Kila mwanadamu anapitia nyakati ngumu za maisha: nyakati za uchungu, kukosa mwelekeo, kuona mambo hayaendi, kutokueleweka, kufeli na wakati mwingine hata kukata tamaa kabisa. Katika nyakati hizo, kama mtu asipopata msaada au asipoweza kujinasua mwenyewe vizuri anaweza akapoteza mojamoja mwelekeo wa maisha au hata ndio ukawa mwisho wa maisha yake.

Kama kwa Eliya Mungu alivyomtuma malaika kumpatia chakula na nguvu ya chakula hicho akaweza kusimama na kuendelea na safari yake ya utume ndivyo hata leo Mungu anaweka mbele yetu kwa njia ya Kristo chakula cha uzima ambacho ni Kristo huyo huyo mwenyewe katika sakramenti zake na hasa sakramenti ya Ekaristi Takatifu ili tupate nguvu ya kusimama na kusonga mbele. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatufundisha kuwa katika Ekaristi Kristo anakuwa chakula cha wasafiri “viaticum” ambacho kinakuwa ni nguvu kwa waliochoka, waliopoteza mwelekeo na waliokata tamaa. Katika sakramenti hiyo ya altare, Bwana anakutana na mwanadamu, anaambatana naye njiani katika safari ya maisha na anakuwa kweli chakula kwa mwanadamu aliye na njaa ya kupata ukweli na aliye na njaa ya kuwa na uhuru (Rej. Encyclical Sacramentum Caritatis).

Tazama ni nguvu kubwa kiasi gani iliyomo katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwa si tu kwa mafaa ya roho bali ya utu wetu mzima kabisa! Na ni kwa nguvu hii ya Ekaristi tunaelewa vizuri kabisa alichowahi kusema Mtakatifu Maria Yohana Vianney kwamba “iache parokia kwa miaka 20 bila Padre  na watu wataishia kuabudu wanyama”. Miaka 20 bila Padre maana yake ni miaka 20 bila Ekaristi, miaka 20 bila nguvu ya kimungu na miaka 20 ya njaa ya kupata ukweli na uhuru wa wana wa Mungu. Kwa nini watu wasiabudu wanyama na hatimaye wao wenyewe kugeuka kuwa wanyama?

Mafundisho haya yatusaidie kujenga ndani yetu hamu ya kupokea Ekaristi mara kwa mara. Tuone kabisa kuwa tunapungukiwa kitu muhimu kama tusipopokea Ekaristi na mbaya zaidi kama hatupokei kwa muda mrefu na kwa makusudi au kwa kutokujali. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika barua yake “Sakramenti ya Upendo” anaongeza kuwa mkristo anapaswa kujitahidi kishiriki mara nyingi awezavyo ili uovu wa dunia usimzunguke na kumshinda. Tena aishiriki mara nyingi awezavyo ili apate nguvu ya kumbadili yeye mwenyewe na kumwelekeza kuelekea mema. Ni katika kupokea Ekaristi mkristo anafikia tendo kuu kabisa la sala. Sala kama muungano na Mungu huakisiwa kama kilele chake na tendo la kukomunika, tendo linaoonesha muungano wa mwamini na kanisa, na muungano wake na Mungu.

Yapo mazingira ya kusikitisha ambapo mwamini anajifungia kupokea Ekaristi kwa sababu mbalimbali za kichungaji zinazomwingiza katika vikwazo. Katika hali hii anashindwa kuudhihirisha muungano wake wa kikomunio na kanisa na muungano wake wa kikomunio na Mungu. ni tendo la kusikitisha kwa sababu pia linaliumiza kanisa kama mama wa wanawe wote na ndiyo maana kanisa haliachi kila wakati kujishughulisha na wanawe walio katika vikwazo ili warudi. Ni mwaliko pia kwa kila mwamini anayeishi katika vikwazo kutumia nafasi mbalimbali na milango ya kanisa iliyo wazi daima kumsindikiza polepole na hatua kwa hatua kuirudia komunyo Takatifu. Na huu pia unakuwa ni mwaliko kwa mwamini aliye ndani ya komunyo Takatifu kujilinda dhidi ya kuteleza na kuanguka kama anavyotukumbusha mtume Paulo  kuwa “yeye anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

11 August 2018, 09:55