Cerca

Vatican News
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani na amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani na amana ya uzima wa milele. 

Ekaristi Takatifu ni amana ya uzima wa milele!

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la imani na muhtasari wa fumbo la wokovuwa mwanadamu! Hii ni Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo mwamini anapata amana ya uzima wa milele.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Wapendwa taifa la Mungu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibuni tena katika siku hii ya Bwana tushiriki tena upendo wake pamoja. Leo tunaadhimisha Jumapili ya 20 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Jumapili iliyopita – tuliona na kusikia habari juu ya wasiwasi wa watu, baada ya kupata mwaliko wa kula Mwili na kunywa damu yake Bwana. Wanakosa imani. Wanaona kuwa haiwezekani. Wanakosa utayari wa kuona upande wa pili. Leo tena tunasikia Yesu anaendelea na nia yake – anaendelea kufafanua na kutoa mwaliko – kushiriki MKATE WA UZIMA. Katika somo la kwanza tunaona kuwa wito unatolewa kuvuka hali ya ujinga na kuingia na kuongozwa na hekima ya Mungu

Katika Somo la pili jumapili iliyopita tulisikia mwaliko wa Mt. Paolo kuishi fadhila. Katika somo la leo Mt. Paolo anatualika tufanye tafakari na kusoma alama za nyakati ili kuuona mpango wa Mungu, ili kuzaliwa upya. Anatukumbusha juu ya uwezekano wa kuona pia zawadi za Mungu na upendo wake, uzima wake na kuweza kushukuru na kumsherehekea huyo Mungu wa uzima. Zaidi sana anatualika kuwa ufahamu huu uhusishe jumuiya nzima na huu ndio ufahamu mpya kama anavyouita Paolo, ambayo ni hekima ya kweli katika Kristo.

Katika Injili ya leo tunaona kwamba Yesu anaandaa karamu – anatoa mwaliko – akisema wazi Mwili wangu na Damu yangu ni chakula cha kweli na kinywaji cha kweli. katika sura yote ya 6 ya Injili ya Yohane tunaona Yesu anasema wazi – mimi ndimi mkate wa uzima ulioshuka toka mbinguni -  na anatualika tuule na kumwamini yeye. Kwa hilo tunapata uzima wa milele. Halafu katika Yoh.6:51, Yesu anasema – mkate niwapao kwa ajili ya uzima wa ulimwengu ni mwili wangu. Halafu wanauliza – awezaje kutupa sisi mwili wake kama chakula? Je waliuliza hivi ili kumpa Yesu nafasi ya kutoa maelezo? Bila shaka walitegemea hilo ila Yesu alitegemea kusema jambo lingine. Aidha katika maandiko  matakatifu kula mwili wa mtu ilionekana kama alama ya uadui mkubwa (Zab.27:2; Zakaria 11:9) na kunywa damu ya mtu kama alama ya chuki kubwa na jambo lililokatazwa na sheria ya Mungu (Mwa.9:4, Walawi 3:17; Kumb.12:23).

Tunasoma kuwa neno ‘utakuwa unachokula’ halikuwa kwenye kamusi ya Kiingereza mpaka kwenye miaka ya 1920 na 1930, wakati mwanalishe maarufu Victor Lindlahr, aliyeamini kabisa kuwa chakula hutawala afya alipoanza kuongea juu ya nafasi ya chakula katika  mwili wa mwanadamu. Mwaka 1942, Lindlahr aliandika kitabu "You Are What You Eat: How to Win and Keep Health With Diet." – utakuwa unachokula: namna ya kupata na kutunza afya kwa njia ya chakula. Jambo hili likagusa sana dhamiri za watu.

Milo yetu – inagusa miili yetu – ukila nyama ya ng’ombe unatoa harufu ya ng’ombe, samaki hali kadhalika n.k, na vinywaji pia - mtu hucheua kile alacho au anywacho.   Katika ukweli wa maisha – chakula ni zaidi ya ule mkusanyiko tu wa vitu vinavyounda hicho tulacho. Chakula kikishaandaliwa huwa ni alama ya upendo na alama ya umoja kwa ndugu, jamaa na marafiki. Wengine husema meza ya chakula na kinywaji huunganisha, hukutanisha. Hata waliogombana, wakipatana huhitimisha maelewano yao  kwa mlo na kinywaji. Makabila yote hufanya hivyo. Yesu aliagana na wanafunzi wake kwa karamu ya Bwana.

Pia namna tunavyokula na vitu tunavyokula na kunywa huelezea urithi wetu – ukiona vyakula na jinsi watu wanavyokula waweza kuelezea pia asili yao, kabila lao, taifa lao, utamaduni wao n.k. angalia matangazo mbalimbali ya biashara – safari – urithi wetu n.k. Kwa kawaida mwili hulishwa na chakula na kinywaji tunachokula na ROHO huburudishwa na matokeo ya ulaji na unywaji huo. Baada ya kula chakula kizuri, safi na salama – tunafurahi, tunachangamka, tunawashukuru waliokiandaa na tunamshukuru Mungu kwa kutujalia hayo.

Leo tunaye Yesu Kristo ambaye anatupatia chakula cha mbinguni – tunaalikwa tule na tunywe ili tuupate uzima wa milele. Hakika katika karamu ya mwisho tunaona tendo kuu la upendo. Hivyo uzima mpya wa Kikristo unapatikana hapa. Kwa tendo hili la upendo – MUNGU ANAHUSIANA NA MWANADAMU yaani  MUNGU ANABAKI KWETU NASI PIA KWAKE. Katika EKARISTI, tunaadhimisha UMWILISHO WA KRISTO na kwa hiyo tunaadhimisha maisha mapya ya kimungu yaliyoletwa kwetu kwa njia ya Kristo. Ekaristi inatupatia uzima wa milele. Amina.

Tumsifu Yesu Kristo.

 

15 August 2018, 07:47