Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linajadili kuhusu mapinduzi ya kilimo na mawasiliano ndani ya Kanisa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linajadili kuhusu mapinduzi ya kilimo na mawasiliano ndani ya Kanisa  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini: Kilimo na Mawasiliano

Askofu mkuu Steven Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini katika hotuba yake elekezi, amekazia umuhimu wa Kanisa kuwa ni chombo cha huruma na mapendo kwa watu wa Mungu sanjari na kuisaidia familia ya Mungu Afrika ya Kusini kuchuchumilia na hatimaye, kuambata utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, SACBS, katika mkutano wake mkuu wa Mwaka 2018, linapembua kwa kina na mapana mapinduzi ya kilimo yaliyotangazwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika ya Kusini, pamoja na mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa Katoliki nchini humo. Askofu mkuu Steven Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini katika hotuba yake elekezi, amekazia umuhimu wa Kanisa kuwa ni chombo cha huruma na mapendo kwa watu wa Mungu sanjari na kuisaidia familia ya Mungu Afrika ya Kusini kuchuchumilia na hatimaye, kuambata utakatifu wa maisha, changamoto inayotolewa na Mama Kanisa, kama mwaliko na wito kwa kila mwamini na kukaziwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Brislin alisema, hivi karibuni, Jimbo kuu la Johanesburg limeadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu lilipoanzishwa na imekuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake, uliowawezesha watu wa Mungu kutangaziwa na kushuhudiwa Habari Njema ya Wokovu. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani ili kuomba huruma na neema ya Mungu kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Imekuwa ni nafasi ya kutafakari umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa nchini Afrika ya Kusini.

Vyombo hivi vinapaswa kuwa ni sauti ya kinabii kwa Kanisa nchini Afrika ya Kusini kwa kuhakikisha kwamba, taarifa za Baraza la Maaskofu na Kanisa katika ujumla wake, zinawasilishwa kikamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Afrika ya Kusini. Kwanza kabisa, Baraza la Maaskofu linapaswa kuimarisha mawasiliano kati yao wenyewe pamoja na kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Kanisa unaofumbatwa katika ukweli na uwazi unawafikia kwa usahihi watu wa Mungu.

Kanisa katika maisha na utume wake, halihitaji upendeleo, bali linapania nafasi ya kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu na wala halina sababu ya kufanya malumbano na makundi ya watu kana kwamba, linahitaji kupata “ujiko” au upendeleo maalum kutoka Serikalini. Majimbo yejenge utamaduni wa kushirikishana historia, matukio na changamoto katika maisha na utume wa Makanisa mahalia na kuangalia jinsi ambavyo matukio kama haya yanavyoweza kuboresha mchakato wa utakatifu miongoni mwa familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini.

Si kila wakati, Kanisa Afrika ya Kusini lazima litoe tamko kwa matukio mbali mbali ya kisiasa na kijamii. Kama likifanya hivi, kwanza kabisa, tafakari ya kina lazima ifanyike, ili kupanga mawazo na kuwakilisha msimamo wa Kanisa katika masuala hasa zaidi ya imani na maadili, ili kusaidia mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Brislin anasema hakuna sababu ya msingi ya kufanya mashindano ya kutoa matamko kana kwamba, Kanisa linashinikizwa kufanya hivyo. Mawasiliano yalenge zaidi kutoa msimamo wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kuhusu masuala ya imani, maadili na utu wema na kwamba, mambo haya yanaweza kufafanuliwa vyema zaidi kwa kuwatumia Maaskofu, wanataalimungu au watu waliobobea katika fani hizi.

Umefika wakati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kuhakikisha kwamba, linatumia vyema maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuwa na sera na mbinu mkakati zitakaloliwezesha Kanisa kufikisha ujumbe wake, kama linavyokusudiwa! Vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Afrika ya Kusini, havina budi kuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Kanisa unawafikia watu wengi zaidi katika ukweli na uaminifu kwa Mafundisho ya Mama Kanisa na wala si kwa ajili ya kuwafurahisha watu.

Utu, heshima, ustawi, haki msingi za binadamu ni kati ya mambo ambayo Kanisa linataka kuyasimamia kwa ajili ya mafao ya wengi. Mawasiliano ndani ya Kanisa yalenge kuhabarisha, kuelimisha, kufunda na kuwaendeleza watu: kiroho na kimwili, kama njia ya kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zinazojitokeza katika mwanga wa Injili. Mawasiliano ya Kanisa yanajikita zaidi katika kulinda, kutetea na kudumisha: maisha, utu na heshima ya binadamu; usawa, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kanisa linapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa, ili kuamsha tena miongoni mwa watu, upendo na mshikamano wa dhati, mambo msingi yanayotiliwa mkazo katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Lengo la mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kusaidia mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano. Kiini cha ujumbe wa Kanisa ni Injili ya Kristo! Kwa sasa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linataka kuunda upya mfumo wa mawasiliano unaojikita katika taaluma, tafiti makini na uwajibikaji utakaogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kumbe, kuna haja kwa Baraza kutenga rasilimali fedha na watu, ili kuweza kufanikisha malengo haya na kuanza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Afrika ya Kusini, mwaka 2019.

Askofu mkuu Steven Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini katika hotuba yake elekezi amepembua kwa kina na mapana kuhusu hali ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini chini ya uongozi wa Rais Cyril Ramaphosa, anayeshutumiwa kwa kusababisha mpasuko katika chama tawala; msimamo wake kuhusu mapambano ya rushwa na ufisadi kwa kukazia: ukweli, uaminifu, uwajibikaji na utawala bora pamoja na kuvutia wawekezaji Afrika ya Kusini.

Lakini hata hivyo, ubaguzi wa rangi na vitendo vya uvunjifu wa haki na amani vinaendelea kushamiri nchini Afrika ya Kusini, jambo ambalo kamwe haliwezi kufumbiwa macho na wapenda haki na amani. Hali hii inajionesha pia katika hatua ya kutaifisha ardhi ya watu bila kuwalipa fidia. Makundi ya uhalifu kitaifa na kimataifa yanazidi kushamiri sana nchini Afrika ya Kusini, kiasi kwamba, utakatishaji wa fedha haramu limekuwa ni jambo la kawaida. Kuna nyanyaso za kijinsia na mauaji ya kisiasa yanayoendelea chini kwa chini kama kwamba, hakuna vyombo vya ulinzi na usalama.

Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga ili kweli: haki, amani na mshikamano viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu Afrika ya Kusini na watu wanaomba hifadhi ya kisiasa waweze kupatiwa makazi. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha”. Kambi ya wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa inayotarajiwa kujengwa Kaskazini wa Afrika ya Kusini, si mahali muafaka kutokana na kuwa mbali na maeneo ya mjini ambako watu wanaweza kupata huduma kwa urahisi. Kuna haja ya kufuata ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwani hawa ni rasilimali na utajiri mkubwa, ikiwa kama kutakuwepo na sera na mikakati makini.

Mwishoni, Askofu mkuu Steven Brislin amegusia umuhimu wa Kanisa kuwa na mfuko wa hifadhi za kijamii kwa ajili ya ustawi, ulinzi na mafao ya wakleri na watawa nchini Afrika ya Kusini. Ulimwengu mamboleo umesheheni changamoto nyingi, kumbe, kuna haja ya kuwa na uhakika wa usalama wa watumishi wa Kanisa, kama njia ya kuwasaidia kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu.

Sikiliza mwenyewe kwa raha zako!

 

07 August 2018, 14:39