Askofu mstaafu Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba ameaga dunia!
Sr. Angela Rwezula - Vatican
Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Mhashamu Nestori Timanywa alifariki dunia tarehe 28 Agosti 2018 , katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu. Misa ya mazishi itafanyika tarehe 31 Agosti 2018 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Bikira Maria Mama mwenye Huruma Jimboni Bukoba ikitanguliwa na masifu ya jioni.
Taarifa iliyotolewa na Mhashamu Baba Askofu Deusderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania imeeleza kuwa, Baba Askofu Mstaafu Nestori Timanywa amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani majira ya saa tano asubuhi ya tarehe 28 Agosti 2018.
Akitoa utaratibu wa mazishi ya Askofu Mstaafu Nestori Timanywa kupitia Radio MBIU, Askofu Rwoma amesema kuwa, maziko yatafanyika Ijumaa tarehe 31 Agosti kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria, Mama Mwenye Huruma Jimboni Bukoba, yakitanguliwa na Masifu ya Jioni.
Askofu Mstaafu Nestori Tumanywa alizaliwa tarehe 7 Mei 1937 katika Kijiji cha Kakungiri, Parokiani Mugana, baada ya majiundo yake akapewa daraja Takatifu la Upadre tarehe 11 Desemba 1966 na Mwadhama Lauren Kardinali Rugambwa. Kunako tarehe 26 Novemba 1973 akachaguliwa na Baba Mtakatifu wa wakati ule Papa Paulo wa VI, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba na kusimikwa rasmi kunako tarehe 24 Februari 1974.
Amestaafu tangu tarehe 15 Januari 2013, akiwa na umri wa miaka 75. Na tarehe 28 Agosti 2018 akiwa na umri wa miaka 81 ameitwa kwa Mungu Baba.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa, Jina lake libarikiwe leo na hata Milele!
Kwa maelezo zaidi: http://www.bukobadiocese.co.tz/bishopsofbukoba.php