Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu Jimboni Mbulu, Tanzania inahimizwa kumpokea, kumsikiliza na kushirikiana na Askofu wake mpya! Familia ya Mungu Jimboni Mbulu, Tanzania inahimizwa kumpokea, kumsikiliza na kushirikiana na Askofu wake mpya!  (AFP or licensors)

Familia ya Mungu Mbulu, mpokeeni, msikilizeni na kumuenzi Askofu wenu mpya!

Askofu Falian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini Jimbo Katoliki la Mbulu kumpokea kwa ukarimu na upendo Askofu wao mpya, kama sehemu ya mapenzi na mpango wa Mungu, ili kweli Mwenyezi Mungu aabudiwe na mwanadamu apate wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu anayo dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Lakini zaidi, anao wajibu wa kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu, kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu, ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Wakleri wanatambua kwamba, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ajili ya mastahili yao binafsi, kumbe, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, chemchemi ya amana za maisha ya kiroho!

Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika mahojiano maalum na Vatican News, wakati huu familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mbulu na Tanzania katika ujumla wake, inapojiandaa kwa ajili ya Askofu mteule Anthony Lagwen Gaspar, kuwekwa wakfu kama Askofu na kusimikwa rasmi kama kiongozi mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, anasema, Wito ni mwendelezo wa historia ya mapendo ambayo inapata chimbuko lake katika Daraja Takatifu. Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, analea na kupalilia miito ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani toba na wongofu wa ndani, kama sehemu ya mchakato wa utume, umisionari na uinjilishaji. Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu na kwamba, Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Askofu Kassala anawaalika waamini Jimbo Katoliki la Mbulu kumpokea kwa ukarimu na upendo Askofu wao mpya, kama sehemu ya mapenzi na mpango wa Mungu, ili kweli Mwenyezi Mungu aabudiwe na mwanadamu apate wokovu. Anawaalika waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kumsikiliza na kuandamana na Askofu wao katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji Jimbo Katoliki Mbulu. Wampatie nafasi Askofu Lagwen: kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza, daima akiwalinda dhidi ya adui wa imani, maadili na utu wema.

Askofu Kassala anapenda kuchukua nafasi hii, kumkaribisha Askofu mteule Anthony Lagwen Gaspar katika urika wa Maaskofu, awe tayari kutumika, daima akijitahidi kusoma alama za nyakati. Aendelee kujisadaka katika maisha yake, daima akimtegemea Mwenyezi Mungu! Kwa huruma, upendo na msamaha awahudumie pia Mbwamwitu watakaojitokeza mbele ya safari, daima akionesha sifa za Kristo Mchungaji mwema!

Askofu mteule Anthony Lagwen Gaspar, aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Mei 2018 kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mbulu, nchini Tanzania. Nembo yake ya Kiaskofu inaongozwa na maneno: Kwa upendo na umoja tutumikie! Askofu mteule Anthony Lagwen alizaliwa tarehe 5 Julai 1967 huko Tlawi, Jimboni Mbulu. Baada ya masomo yake ya msingi, alibahatika kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari Ndogo ya Sanu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Akapata masomo ya falsafa kutoka Seminari kuu ya Ntungamo, iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akahamia Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora ili kuendelea na masomo ya kitaalimungu. Tarehe 18 Oktoba 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki Mbulu.

Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake wa Kipadre kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2000, alikuwa Paroko-usu wa Parokia ya Bashay. Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2004 akepelekwa na Jimbo kujiendeleza zaidi katika masuala ya biashara kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino Tanzania, SAUT, Mwanza. Kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2009 akateuliwa kuwa Mchumi wa Jimbo Katoliki la Mbulu. Kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011 akatumwa tena na Jimbo kujiendeleza zaidi katika masuala ya biashara kwenye Taasisi ya “East and Southern Africa Management Institute” iliyoko Jijini, Arusha. Kuanzia mwaka 2012 hadi kuteuliwa kwake, amekuwa ni mchumi mwaminifu wa mali ya Kanisa, Jimbo Katoliki la Mbulu!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

10 August 2018, 16:56