Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVI ya Mwaka B wa Kanisa. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVI ya Mwaka B wa Kanisa.  (ANSA)

Uongozi wa Kanisa ni huduma ya Neno, Upendo na Sakramenti za Kanisa!

Maandiko Matakatifu Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa yanawaangazia wale wanaochukua dhamana ya uongozi na kuwaalika kujishughulisha kwa ajili ya ustawi wa watu wanaowaongoza; kutenda kwa hekima, kutenda kwa haki, kulinda na kuleta umoja, kustawisha amani.

Padre William Bahitwa. - Vatican.

UTANGULIZI: Kristo ndiye amani yetu. Amani ya duniani ni tunda la amani ya Kristo, mkuu wa amani ya kimasiha. Kwa damu ya msalaba wake, ameharibu ndani yake uadui amewapatanisha watu na Mungu na amelifanya Kanisa lake kuwa Sakramenti ya umoja wa ubinadamu na ya umoja wake na Mungu. (Rej KKK. 2305). Katika dominika hii ya 16 ya mwaka B wa Kanisa, Maandiko Matakatifu yanatualika tutafakari juu ya tunu zinazojenga ubinadamu: umoja, haki, amani na manufaa ya wote.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Yer 23:1-6) Mungu anatoa maonyo kwa wachungaji - viongozi na watawala- wasiotekeleza majukumu yao kwa kundi walilokabidhiwa. Na wao badala ya kushughulikia ustawi wa kundi, kwa kutokujali kwao wanaliweka kundi katika hatari na wanalitawanya. Kwa kinywa cha Nabii Yeremia, Mungu anawaonya kuwa atawapatiliza kwa uovu huo wanaolitendea kundi walilokabidhiwa. Kisha anatoa unabii kuwa atainua kiongozi atakayechipusha haki na atakayetenda kwa hekima katika kulichunga kundi hilo la Bwana.

Katika somo hili tunaona madhara au hasara inayoikumba jamii pale ambapo jamii hiyo inakuwa na kiongozi asiyejali mahitaji ya watu wake. Jamii inaingia katika mahangaiko, inakosa umoja na inakosa amani. Badala yake, pale jamii inapokuwa na kiongozi anayeijali, anayezingatia haki na kutenda kwa hekima jamii hiyo huneemeka. Na haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa watu wake.

Somo la pili (Ef. 2:13-18) linasisitiza nafasi ya Kristo katika kujenga umoja na kuleta amani kwa watu wake. Mtume Paulo kwa kuangalia hali ilivyokuwa kati ya jamii ya wayahudi na ile ya watu walioitwa wa mataifa, kabla na baada ya Kristo, anakiri kuwa Kristo ndiye amani yetu. Mtume Paulo anakiri hilo kwa sababu anaona kwa kukiri imani kwa Kristo watu hao wamekuwa wamoja na wamepatana. Ule utofauti wa kiibada, wa kisheria na wa kijamii uliokuwapo hapo awali sasa haupo. Lakini amani hii Kristo ameifanikisha kwa kujisadaka Msalabani.  Somo linakazia juu ya nafasi ya Kristo katika kujenga jumuiya na jamii bora, si tu katika upande wa imani, bali hata zaidi ya hapo na kugusa nyanja nyingine za maisha.

Injili (Mk. 6: 30-34) mitume wanarudi kutoka kule Yesu alikowatuma waende wawili wawili kutangaza Habari Njema. Somo hili linalenga kuonesha moyo wa Yesu wa kujali mahitaji ya watu wake. Yeye kama kiongozi wa mitume alitambua uchovu waliokuwa nao baada ya kutoka utumeni, alitambua mahitaji yao ya kupumzika kidogo kupata nguvu ili utume uendelee. Akawaambia “njooni mahali pa faragha mkapumzike kidogo”. Hapo hapo anaona kundi linalomfuata, kundi lililokuwa na mahitaji ya kusikia Neno lake na kupata mafundisho yake. Aliwahurumia kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Hili lilikuwa kweli ni kundi kama kondoo wasio na mchungaji kwa sababu wale waliokuwa wamekabidhiwa kulihudumia, makuhani na wakuu wa makuhani, hawakuwa wakijishugulisha tena na mahitaji ya kondoo wao. Akaanza kuwafundisha mambo mengi.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kiongozi ni alama ya umoja katika jamii. Anayechukua nafasi hii anabeba dhamana kubwa. Anapoitimiza vema anajipatia wingi wa baraka toka kwa Mungu, muumba na kiongozi halisi wa watu wake. Kinyume chake anakuwa chukizo kwanza kwa Mungu mwenyewe, anakaribisha hasira ya Mungu na anawaletea hatari watu anaowaongoza.

Maandiko Matakatifu siku ya leo yanawaangazia wale wanaochukua dhamana ya uongozi na kuwaalika kujishughulisha kwa ajili ya ustawi wa watu wanaowaongoza; kutenda kwa hekima, kutenda kwa haki, kulinda na kuleta umoja, kustawisha amani. Maandiko yanamuweka Kristo kama mfano ambao viongozi wote watajifunza namna ya kuyatimiza hayo. Yeye alishughulikia mahitaji halisi ya watu wake, aliwajali, aliunganisha makundi yasiyopatana na akajitoa sadaka msalabani ili kuwaletea ukombozi toka utumwa wa dhambi na mauti. Ni kweli mfalme wa amani na ndiye amani yetu. Na uongozi unaomtambua Kristo na unaotambua tunu za kijamii zilizojengwa katika Kristo utapata amani kama matunda yake.

Sisi ambao kwa mapenzi ya Mungu tumepata neema ya kuwa wakristo tulitegemewa kuwa mstari wa mbele katika kulinda tunu za kijamii zilizojengwa katika Kristo pale tupatapo nafasi ya uongozi katika jamii, hasa jamii inayoundwa na watu wa imani tofauti tofauti. Hii bila kumaanisha kuwafanya wote wafuate imani ya kikristo, bali misingi yake na tunu za kiinjili zinazostawisha ubinadamu mzima. Kinyume chake baadhi ya viongozi wakristo ndio wamekuwa mstari wa mbele kupinga na hata kuongoza mikakati ya kupiga vita tunu za kikristo katika jamii, si katika jumuiya za kimataifa, si katika jumuiya za kitaifa na hata katika jamii zilizo chini ya jumuiya hizo.

Ni masikitiko makubwa kwa mfano kuona viongozi wakristo wakiongoza kampeni za upitishaji wa sheria zinazoruhusu utoaji wa mimba. Ni masikitiko kwa mfano kuona viongozi wakristo wakiongoza kampeni za kuondoa misalaba katika shule za Kanisa ili kutokuwakwaza wanafunzi wasio wakristo wanaosoma hapo. Na ni masikitiko makubwa kuona viongozi wakristo wakiongoza kampeni za kulichafua kanisa na kulivunjia uaminifu katika jamii kwa sababu linakuwa tishio kwao katika misimamo ya mafundisho yanayojengwa juu ya Kristo.

Ni jambo la kumshukuru Mungu na tena ni bahati kubwa kwamba sisi tunaishi katika nchi iliyo na sifa ya kuwa kisiwa cha amani. Sifa hii pia inatuwajibisha kuendelea kuliombea taifa letu na jumuiya zote zilizo ndani yake ziendele kudumu katika amani. Ni muhimu kukumbuka pia kuwa amani ni mojawapo ya tunu zilizowekwa na waasisi wa taifa letu. Pamoja nayo ipo hekima na umoja. Ndivyo tunavyosali na kuimba katika wimbo wetu wa Taifa, Hekima, umoja na Amani ni ngao zetu. Kumbe, amani hii tunavyoifurahia, waasisi hao waliangaziwa kuona kuwa ni zao la utendaji wa hekima na ni zao la utunzaji wa umoja wa kitaifa.

Na kwa jinsi hiyo, haitoshi tu kutamani kuendelea kuwa na amani yetu kama tunaanza kulegalega katika mawili yanayotangulia amani. Kila tunapoililia amani turudi nyuma na kujipima namna gani tumeongoza kwa hekima na namna gani tumelinda umoja; namna gani tumetafuta hekima na namna gani tumekusudia kujenga umoja, naye Kristo aliye hekima ya kimungu na anayekusudia wote wawe na umoja atatujia katika amani yake.

Sikiliza

 

21 July 2018, 06:52