Tafuta

Vatican News
Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu inafumbatwa katika huruma, upendo na msamaha! Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu inafumbatwa katika huruma, upendo na msamaha! 

Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu inafumbata upendo kwa wote!

Tasaufi ya Kikristo inajengwa katika misingi ya Neno la Mungu, Mapokeo ya Kanisa, Mang’amuzi na mafundisho ya watakatifu mbalimbali katika historia ya Kanisa, Liturjia na hasa Ekaristi Takatifu. Kumbe, tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu inatusaidia kuishi katika imani thabiti ya Kikristo na inatujenga katika mitazamo sahihi ya Kikristo kadiri ya mafundisho ya Yesu mwenyewe.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu msikilizaji napenda kukaribisha katika tafakari ya tasaufi ya Damu Takatifu. Tuko katika mwezi Julai, mwezi ambao Mama Kanisa ameutenga maalumu kwa ajili ya kutafakari na kuitukuza kwa namna ya pekee Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Damu ya ukombozi na upatanisho. Katika tafakari iliyopita tulisema kuwa tasaufi ni ujumla wa mambo yanayohuisha na kuongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu; ni mambo yahusuyo imani, mitazamo na matendo maalumu. Katika mazingira ya Kikristo tunaweza kusema kwamba tasaufi ni mtindo wa maisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu.

Ndani ya Kanisa kuna tasaufi mbalimbali ambazo ni zawadi zitokazo kwa Roho Mtakatifu. Ikumbukwe daima kuwa kiini cha tasaufi yeyote ya Kikristo ni Yesu mwenyewe: yaani mafundisho na mfano halisi wa maisha yake. Kila tasaufi hujaribu kuyaishi mafundisho ya Yesu katika matendo na maisha ya kila siku. Tasaufi huongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu katika mahusiano na Mungu, mahusiano na watu wengine, na ulimwengu kwa jumla. Tasaufi yeyote haiwezi kuwa tasaufi ya kweli kama haina uhusiano na maisha halisi. Ikijengwa katika misingi ya Neno la Mungu, Mapokeo ya Kanisa, Mang’amuzi na mafundisho ya watakatifu mbalimbali katika historia ya Kanisa, Liturjia na hasa Ekaristi Takatifu, tasaufi ya Damu Takatifu inatusaidia kuishi katika imani thabiti ya Kikristo na inatujenga katika mitazamo sahihi ya Kikristu kadiri ya mafundisho ya Yesu mwenyewe.

Fadhila ya pili inayotokana na tafakari ya mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote ni fadhila ya upendo usiobagua: Katika maisha yetu ya kila siku mara kadhaa tumeshindwa kuwapenda na kuwatendea watu kwa usawa. Mara nyingi tunatenda kwa upendeleo au kwa kuwabagua watu kwa kutumia vigezo mbalimbali. Tumezoea kuwapendelea watu wa familiya yetu na ndugu wa karibu, marafiki zetu, watu wa kabila letu, watu wa dini yetu, watu wa jinsia fulani, watu wenye umri fulani, wenye kipato fulani, cheo au hadhi fulani katika jamii, n.k. Kinyume chake, kwa Mungu hakuna upendeleo wala ubaguzi wowote. Mungu hataki upendeleo kwa kuwa anataka watu wote wapate kuokoka bila kumpoteza hata mmoja.

Katika kudhihirisha upendo wa Mungu usio na ubaguzi Yesu alimwaga Damu yake Msalabani kwa ajili wokovu wa wote. Katika Kitabu cha Ufunuo Sura ya Tano aya ya Tisa tunakutana na wimbo wa kumsifu Yesu kwa zawadi na kazi yake ya ukombozi. Wimbo huu unasema, “Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua mihuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa Damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa”.

Kutokana na ukweli huu tasaufi ya Damu Takatifu inapinga ubaguzi wa aina yeyote katika jumuiya, jamii na dunia kwa jumla. Miaka ya hivi karibuni yamefanyika marekebisho katika baadhi ya maneno yatumikayo wakati wa mageuzo ya divai kuwa Damu ya Yesu kwa kutamka maneno, itakayomwagika kwa ajili ya WENGI badala ya kwa ajili ya WOTE.

Baba Mtakatifu mstaafu  Benedikto wa XVI kunako mwaka 2012 alipenda Kanisa zima litamke maneno yaleyale ya Yesu aliyoyatamka katika Karamu ya mwisho kama jinsi yalivyoandikwa katika Biblia kwa lugha ya Kilatini ( “Hic est enim calix Sanguinis mei[…]qui pro vobis et pro multis effundetur.”). Katika lugha yatu ya Kiswahili, kuna utofauti mkubwa wa maana kati ya WOTE na WENGI. Wote ni neno mjumuisho, linawaingiza wote katika wigo bila kumwacha yeyote. Kinyume chake, “wengi” si neno mjumuisho, linawaacha wengine nje ya wigo. Swali la msingi linakuja, endapo Yesu alitamka neno “wengi” badala ya “wote” basi Damu yake haikumwagika kwa ajili ya wote bali kwa ajili ya baadhi tu. Maelezo halisi ya suala hili ni kwamba, Yesu alimwaga Damu yake kwa ajili ya watu wote na si kwa ajili ya baadhi tu. Ukweli huu unabaki hivyo na unabaki kuwa ni nguzo muhimu ya tasaufi ya Damu Takatifu.

Ni kweli kabisa kwamba, maneno aliyotamka Yesu siku ya Karamu ya mwisho kama jinsi yalivyoandikwa katika Biblia ya Kilatini yanatamka “pro multis” yaani kwa tafsiri ya Kiswahili ni “kwa ajili ya wengi”. Hata hivyo kila lugha ina tamaduni na mazingira yake kiasi kwamba tafsiri ya moja kwa moja inaweza isitoe maana halisi iliyodhamiriwa katika lugha tajwa. Wachambuzi wa lugha ya Kilatini wanatudhihirishia kwamba, neno “pro multis” hubeba pia maana ya “kwa ajili ya wote”.

Namna nyingine ya kuelezea kwanini Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliagiza itamkwe “kwa ajili ya wengi” badala ya wote ni kutaka kuonyesha hali halisi itakavyokuwa siku ya mwisho kwamba pamoja na kwamba Yesu alimwaga Damu yake kwa ajili ya wokovu wa watu wote, si watu wote watakaookolewa. Hii ni kwa sababu zawadi ya wokovu imetolewa kwa wote lakini si wote watakaoipokea zawadi hiyo kwa kutumia vibaya uhuru wao. Kwa maana hiyo wengi wataokolewa lakini si wote.

Kwa maana zote hizo mbili, ukweli unabaki palepale kwamba Yesu alimwaga Damu yake kwa ajili ya wote bila ubaguzi. Mitume wa Yesu ambao kwa asili walikuwa Wayahudi walianza kutambua juu ya msimamo wa Mungu wa kutokuwa na upendeleo walipotumwa kwenda Ulimwenguni kote kuwahubiria watu habari njema. Ipo mifano mbalimbali. Petro alipokuwa katika mji wa Kaisaria, alipata maono yaliyomdhihirishia kuwa Mungu anawapokea watu wote pamoja na tamaduni zao. Ndiyo maana anapokutana na akida Cornelio anakubali kumpokea katika imani. Kwa maneno yake mwenyewe Petro alipaza sauti na kusema, “Hakika natambua kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa naye.” (Mat 10, 34-35). Naye Mtume Paulo anasisitizia jambo hili anapowaambia ukweli Wagalatia kwamba katika Kristu Yesu tofauti na ubaguzi wa aina yeyote kati ya watu hukoma kabisa. (Rejea Gal 3, 28).

Umuhimu wa upendo usiobagua unadhihirishwa pia na moja ya tabia za damu katika mwili wa binadamu. Tabia hii ni ile ya kufika katika kila kiungo cha mwili bila kujali ukubwa au udogo wa kiungo husika, bila kujali umbali au ukaribu wake na moyo. Anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu anapaswa kutokuwa mbaguzi wala mwenye upendeleo. Lazima awatendee wote kwa usawa na haki bila kuwabagua. Baba Mtakatifu Fransisko alipokutana na Familia ya Damu Takatifu siku ya tarehe 30 Juni 2018 aliwakumbusha na kuwasisitizia wanafamilia ya Damu kwamba katika huduma kwa jamii na kazi zao za kimisionari wanapaswa kuwajali na kuwafikia watu wote na hasa wale walioko mbali. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuishi fadhila zitokanazo na tasaufi hii ili iwe njia kwetu ya kushuhudia imani yetu kwa maneno na matendo.

Sikiliza

 

 

25 July 2018, 08:31