Misa ya Ufunguzi wa Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM. Misa ya Ufunguzi wa Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM. 

SECAM: Kanisa Barani Afrika liwe makini na vishawishi mamboleo!

Changamoto mamboleo Barani Afrika ni pamoja na: mihimili ya Injili kumezwa sna na malimwengu kiasi cha kushindwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko; rushwa na ufisadi wa mali ya umma; Ukosefu wa haki, amani na utulivu na kwamba, kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, ili Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako” ni fursa makini ya kuzima kiu ya baa la njaa Barani Afrika, kwa kujikita katika: ukarimu, upendo na mshikamano kama njia makini ya kupambana pia na changamoto zinazoendelea kujitokeza Barani Afrika.

Changamoto mamboleo ni pamoja na mihimili ya Injili kumezwa sana na malimwengu kiasi cha kushindwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko; rushwa na ufisadi wa mali ya umma; Ukosefu wa haki, amani na utulivu na kwamba, kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, ili Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa Jumapili tarehe 29 Julai 2018 na Askofu Sithembele Sipuka wa Jimbo Katoliki Mthatha, Afrika ya Kusini, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa SECAM, wakati wa kuzindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu SECAM ilipoanzishwa.

Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Lubaga, Jimbo kuu la Kampala, Uganda na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. Amesema, kama ilivyokuwa kwa watu wa Agano la Kale, hata leo hii, Bara la Afrika bado linakabaliwa na matatizo na changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga. Moja ya changamoto hizi ni baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa chakula Barani Afrika. Jambo la msingi si kukata tamaa, bali kushirikiana na Kristo Yesu, ili kwa njia ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati, watu wengi Barani Afrika waweze kupata mahitaji yao msingi.

Dhana ya baa la njaa inapaswa kuchukuliwa katika mwelekeo mpana zaidi Barani Afrika: Njaa kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ni kurejea tena katika nchi na makazi yao; njaa ya haki, amani na maridhiano ili kutoa fursa kwa familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani. Kimsingi, waamini wanapaswa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kwa kuondokana na ubinafsi, choyo, uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanaendelea kuleta athari kubwa kwa watu wengi Barani Afrika.

Rushwa na ufisadi wa mali ya umma, vimepelekea kushamiri kwa: baa la njaa, umaskini na magonjwa. Kashfa ya rushwa, ufisadi na kutaka kumezwa na malimwengu ni kati ya changamoto zinazoiandama hata mihimili ya uinjilishaji kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”. Wakleri na watawa wanatafuta kwa udi na uvumba uhuru binafsi, raha na starehe; mambo ambayo yanayodhohisha mchakato mzima wa uinjilishaji. Kanisa Barani Afrika halina budi kuwa makini katika kuchagua na kulea mihimili ya uinjilishaji, itakayojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ndani na nje ya Afrika.

Wakristo wote watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu. Vijana wa kizazi kipya wafundwe kumwilisha tunu msingi za maisha, daima wakijitahidi kujenga uhusiano wao wa dhati na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti na Sala zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kanisa liunganishe nguvu na wadau mbali mbali ili kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima yake bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Haki, uchumi shirikishi, sera na siasa zenye mfumo fungamanishi pamoja na masuala ya kijamii ni mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga na waamini kama sehemu ya ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake. Ukwapuaji mkubwa wa ardhi hasa kutoka kwa wakulima vijijini ni hatari kubwa kwa siku za usoni, kwani huu ni mtaji na rasilimali ya wakulima wengi vijijini. Kanisa liendelee kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu kwa kusoma alama za nyakati ili kujibu kilio na matamanio ya halali, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa msisitizo wa pekee. Kila mtu ashiriki kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!
31 July 2018, 15:38