Vatican News
Mkutano wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia Mkutano wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia  (ANSA)

Nchi za AMECEA zinapaswa kuwekeza zaidi katika haki, amani na maridhiano kati ya watu

Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania, anasema licha ya tofauti kubwa za kikabila, kidini, kitamaduni na mapokeo, lakini bado familia ya Mungu Barani Afrika inatakiwa kutumia tofauti hizi katika kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano: Kanisa liendelee kuwekeza katika uinjilishaji wa mpya kwa kutoa kipaumbele kwa vijana na wanasiasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Awamu ya Pili ya Maaskofu wa Afrika wanasema upatanisho na haki ni msingi wa amani ya kweli na kwamba, huu ni utume na dhamana endeelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa. Hakuna amani ya kweli pasi na haki, ukweli, upendo na uhuru kamili unaozingatia na kuheshimu haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, ili kujenga familia ya binadamu na jumuiya inayosimikwa katika misingi ya amani. Upatanisho husinda matatizo, hurejesha heshima na utu wa binadamu, hufungua njia ya maendeleo endelevu na fungamani kati ya watu na hivyo kukoleza amani ambalo ndilo jina jipya la maendeleo kama anavyokaza kusema, Mwenyeheri Paulo VI. Upendo katika ukweli ni chemchemi ya amani ya kudumu!

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki la Kigoma anagusia kuhusu amani na utulivu nchini Tanzania licha ya tofauti kubwa za kikabila, kidini na kiitikadi zilizomo nchini humo, sanjari na umuhimu wa kujikita katika uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kuwahusisha vijana na wanasiasa ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu Barani Afrika.

Kwa miaka mingi, Tanzania inajivunia kuwa ni kisiwa cha amani na mahali ambapo watu wengi kutoka Afrika Mashariki wamepata hifadhi na usalama kama wakimbizi na wahamiaji. Amani na utulivu wa Tanzania ni zawadi ambayo watanzania hawana budi kumshukuru Mungu na kuendelea kuiwajibikia kwa hali na amani, kama chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watanzania wapalilie amani kwa kwa kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kulinda uhuru wa kuabudu; kwa kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Mlola anasema, tofauti msingi zinazojitokeza nchini Tanzania kutokana na makabila, dini na itikadi za watanzania katika masuala mbali mbali ziwe ni chemchemi ya ujenzi wa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii, mambo msingi ambayo yalivaliwa njuga kwa namna ya pekee kabisa na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mtumishi wa Mungu! Baadaye, dhamana hii ikaendelezwa na viongozi wa awamu mbali mbali zilizofuatia.

Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kujaliana kama binadamu hata katika tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kati ya watu na kwamba, tofauti hizi zisiwe ni sababu ya choko choko, mipasuko na migawanyiko ya kijamii. Nchini Tanzania kuna mwingiliano na mafungamano makubwa ya kijamii, kitamaduni na kidini, kwani watanzania wanaunganishwa na utanzania wao na wala si ukabila, dini au itikadi zao, kwani haya ni mambo mpito! Tofauti hizi ziendelee kujenga na kuimarisha uhuru wa kuabudu, haki msingi za binadamu, ukweli na upendo mambo msingi yanayoimarisha Injili ya haki na amani duniani. Jambo la msingi ni watu kufahamu kwamba, wao ni ndugu wamoja, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Joseph Roman Mlola anasema, mambo haya yakizingatiwa na familia ya Mungu Barani Afrika, haki, amani, upendo na mshikamano vitaweza kutawala tena. Bara la Afrika linaangaliwa kuwa ni chachu ya matumaini ya dunia, lakini kwa bahati mbaya, limegeuka kuwa kichaka cha vita, kinzani na migogoro. Tofauti za kikabila, kidini na kiitikadi zijenge na kuimarisha umoja, haki, amani, utu na heshima ya binadamu ili kuweza kujikita zaidi na zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Pili, Mababa wa AMECEA wamekazia uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kwamba, nguvu za ziada zielekezwe katika utume kwa vijana wa kizazi kipya na wanasiasa ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii unahitaji kwa namna ya pekee kabisa kusoma alama za nyakati, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia njia hizi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Vijana wa kizazi kipya ni matumaini na jeuri ya Kanisa la leo na kesho; hawa ndio wadau watakaoweza kushika hatamu za uongozi ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, kumbe wanapaswa kufundwa vyema katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linaitwa na kutumwa kuwainjilisha vijana wa kizazi kipya; kuwapatia elimu na malezi makini yatakayoweza kuwasaidia kupambana na hali pamoja na mazingira yao katika mwanga na kweli za Kiinjili. Vijana waandaliwe ili waweze kuwa ni wamisionari kati pamoja na vijana wenzao, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kanisa lijenge sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuambatana nao, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana na Siku ya XXXIV ya Vijana Kimataifa huko Panama, ni fursa makini kwa Mababa wa AMECEA kujikita katika mchakato wa utume wa vijana, ili kuwajengea matumaini, ari na bidii ya kimisionari katika ujana wao. Vijana wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Kumbe, vijana wakithaminiwa na kuwezeshwa kikamilifu, wanaweza kutenda maajabu hadi watu wakashika tama kwa mshangao mkubwa!

Lakini, vijana nao, wanapaswa kuishi kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, Amri za Mungu, Kanuni maadili na utu wema, vinginevyo, watakuwa wanauchezea ujana wao kwa mambo ya ovyo ovyo na kusahau kwamba, ujana ni mali, lakini fainali ni uzeeni! Kanisa liendelee kuwekeza katika malezi, makuzi na majiundo makini ya watoto wadogo kwa kukazia “utoto mtakatifu” chombo cha uinjilishaji miongoni mwa watoto wenzao. Watoto wajengewe mazingira ya usalama, amani na utulivu, ili waweze kuwa na ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kwani watoto hawa wakifundwa tangu awali watakuwa na moyo wa kujali, kutambua na kuthamini dhamana na nyajibu zao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Wongofu wa kweli, haki, toba na upatanisho, umoja na mshikamano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki msingi, utu na heshima ya binadamu ni kati ya mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika kuwainjilisha wanasiasa Barani Afrika, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho kati ya watu! Wanasiasa wawe mstari wa mbele kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuheshimu, kuthamini na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kudumisha uongozi bora unaojikita katika utawala wa sheria daima kwa kujikita katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa njia hii, hata wanasiasa wanaweza kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa anasema, Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Vatican News kutoka Addis, Ababa nchini Ethiopia!

Sikiliza

 

23 July 2018, 07:13