Tafuta

Vatican News
Mwenyeheri NUNZIO SULPRIZIO kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 14 Oktoba 2018 Mwenyeheri NUNZIO SULPRIZIO kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 14 Oktoba 2018 

Mwenyeheri Nunzio Sulprizio kutangazwa kuwa Mtakatifu 14 Oktoba 2018

Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwenyeheri Nunzio Sulprizio aliyezaliwa mwaka 1817, akatangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu na Papa Pio IX na hatimaye, akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Baba Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1963, tarehe 14 Oktoba 2018 atatangazwa kuwa Mtakatifu pamoja na Mwenyeheri Paulo VI na Askofu mkuu Oscar Romero na wengine pia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 19 Julai 2018 ameongoza Ibada ya Sala ya Kanisa ambayo imehudhuriwa na Baraza la Makardinali na kutangaza kwamba: Mwenyeheri Nunzio Sulprizio, kijana mlei na mfanyakazi mahiri atangazwe kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Siku hiyo pia Mwenyeheri Paulo VI, Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez; Francesco Spinelli, Muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Sakramenti Kuu; Mwenyeheri Vincenzo Romano, Padre wa Jimbo, Mwenyeheri Maria Caterina Kasper; Bikira na mwanzilishi wa Shirika la Wahudumu Maskini wa Kristo Yesu pamoja na Mwenyeheri Nazaria Ignazia wa Mtakatifu Theresa wa Yesu watangazwe kuwa watakatifu siku hiyo hiyo!

Mwenyeheri Nunzio Sulprizio alizaliwa mnamo tarehe 13 Aprili 1817 Pescosansonesco, Abruzzo, nchini Italia na alifariki huko Napoli mnamo tarehe 5 Mei 1836, akiwa na umri wa miaka 18. Alipata kilema alipokuwa akifanya kazi katika kiwanda cha mjomba wake, na Baraza la maaskofu nchini Italia linamuenzi kuwa ni msimamizi na mwombezi wa Chama cha Wafanyakazi Vilema na Viwete.

Mwaka 1859, miaka 23 baada ya kifo cha Mwenyeheri  Nunzio Sulprizio, Papa Pius IX alimtambua kuwa mtumishi wa Mungu na kuanzisha mchakato wa kumtangaza mwenyeheri. Mnamo mwaka 1891, Baba Mtakatifu Leo XIII alizitambua fadhili za kijana huyu kuwa ni za kishujaa na akamfananisha na mtakatifu Aloysius Gonzaga. Mtakatifu Gonzaga alizaliwa mnamo tarehe 9 Machi 1568, maeneo ya Brescia nchini Italia. Alikuwa mtoto wa mfalme ambaye hakuona mali, utajiri, madaraka na heshima ya kifalme kana kwamba ni vitu vya kung’ang’ana navyo. Hivyo aliviachilia mbali, akajiunga na maisha ya kitawa na ufukara kupitia Shirika la Wayesuiti. Angali bado mwanafunzi chuoni Roma, tarehe 21 Juni 1591, alifariki akiwa na umri wa miaka 23 kufuatia kuathirika na ugonjwa alipokuwa akihudumia mgonjwa wa magonjwa ya mlipuko.

Vijana hawa wawili, wanaonesha fadhili za kishujaa katika utakatifu wa maisha kwenye umri mdogo sana. Hata hivyo wana historia tofauti sana katika jamii. Wakati Aloysius Gonzaga alizaliwa katika familia ya kifalme na kuamua kuishi ufukara na huduma kwa watu, Nunzio Sulprizio alizaliwa katika familia maskini, akabaki yatima katika umri mdogo na kujikuta akilazimika kujishughulisha na kazi katika umri mdogo. Hata hivyo, wote wawili wanatoa mfano bora sana kwa vijana, wafanyakazi, wenye mali na madaraka, juu ya utakatifu wa maisha, kujikatalia, kuchapa kazi, kuvumilia mateso, kukabiliana na changamoto za maisha na kujisadaka kuwahudumia wahitaji.

Tarehe 1 Disemba 1963, katika Misa Takatifu ya kumtangaza Nunzio Sulprizio kuwa mwenyeheri, wakati wa mahuburi, Baba Mtakatifu Paulo VI aliwaalika waamini na wote wenye mapenzi mema kuwatazama watakatifu kuwa ni vioo kwa ajili ya kujitambua na kujifahamu vema kadiri ya saikolojia ya kisasa kufuatana na historia na tamaduni ya mwanadamu. Kusoma na kuchambua maisha ya watakatifu ni kioo kwa maana ya kuona kile kinachowezekana ndani ya mwanadamu, na hivyo kutupilia mbali visingizio ili kujirekebisha na kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kama anavyofundisha mtakatifu Agustino: Si isti et istae, cur non ego? Yaani “Iwapo wao wameweza, kwa nini mimi nisiweze, iwapo wao wamekuwa, kwa nini mimi nisiwe?

Kanisa kutangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu halina lengo la kuwatafutia ujiko, kwanza tayari wanagonga mvinyo kwa raha zao. Bali lengo la kuwa na wenyeheri na watakatifu, ni kusoma na kujifunza maisha yao, ikiwa ni neema ya pamoja inayoyaelekeza maisha ya waamini walioko bado hai ili kumfuasa Kristo, aliye mfano kamili kwa wote, kama asemavyo mtume Paulo: wapate kufanana na mwana, yaani Kristo, ili mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi (Rej., Warumi 8:29). Kwa upande mwingine, ni kujitambua na kujithamini kwa kila mmoja kadiri alivyoumbwa na kuitwa kuishi kwa mapenzi ya Mungu kama ilivyo historia ya watakatifu wanavyotofautiana kila mmoja kwa historia na namna yake ya maisha huru na asilia. Hivyo maisha ya waamini yasiwe ya kuoneana husuda, bali kila mmoja kwa namna yake, kadiri anavyofundisha mtume Paulo: uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota, hata nyota nazo hutofautiana kwa uzuri (Rej., IWakorintho 15:41).

Baba Mtakatifu Paulo VI anasisitiza kwamba Mwenyeheri Nunzio Sulprizio anawaalika vijana watambue maisha yao ya ujana kuwa ni upendeleo na neema ya pekee; ujana sio umri wa kujiachia kwa tamaa huria na mivuto inayowapiga mweleka; ujana sio umri wa kusingizia kwamba lazima kuanguka na kufanya makosa fulani fulani kama baadhi wanavyodanganyana; ujana sio umri wa changamoto na mahangaiko yasiyoweza kushindwa kama wanavyojiendekeza baadhi ya vijana; ujana sio umri wa uchoyo, ulevi, uzinifu, rushwa, dhuluma, uvivu, utegemezi na mambo ya kujibofusha kwa starehe na anasa.

Ujana ni umri wa kutenda mema, ni neema ya kuwa na nguvu na muda wa kuboresha maisha bora kwa kijana binafsi na kwa wengine. Kama ilivyo kwa sakramenti ya Ubatizo, ujana ni hazina ya kulinda, kuenzi, kuelimisha, kukuza na kuendeleza kwa ajili ya matunda bora na yanayodumu. Huu ni mwaliko kwa vijana kubadili jamii ya leo, ili iweze kuwa jamii yenye matumaini kwa vizazi vijavyo, na sio kuwa kizazi cha upotevu.

Kwa upande wa wafanyakazi, Mwenyeheri Nunzio Sulprizio ni kioo katika kujitafutia kipato halali kwa haki na usawa bila kujitafutia faida kubwa inayonyonya wengine na kupelekea maumivu katika jamii. Kijana huyu aliyekuwa maskini, mlemavu na mwenye mateso makali katika maisha yake ya muda mfupi, anaonesha umuhimu wa kujali mazingira mazuri kwa wafanyakazi na kulinda utu na heshima ya binadamu. Juhudi, uchovu na mahangaiko yao yawe ni nguzo katika kutetea haki zao msingi na kushuhudia maisha ya maadili katika jamii.

Mwenyeheri Paulo VI anasema kazi na shughuli za kila siku haziwezi kutenganishwa na imani ya mtu, kwani imani ndiyo inayotoa mwanga na kuvuvia utendaji wa haki na usawa kwa ajili ya maendelo ya binadamu kwa mafao ya wote. Imani ndiyo inayotakatifuza shughuli za kila siku, imani ndiyo inayofuta jasho na kumfariji mwanadamu kwa kuonesha maana na lengo halisi la kazi, uchumi, jamii na shughuli zote kwa kuzingatia utu na heshima ya mwanadamu.

Mwenyeheri Nunzio Sulprizio ni kioo kinachoakisi jinsi gani itakuwa uvunjwaji mkubwa wa haki kutompatia nafasi mfanyakazi kuwa na uhuru wa kuabudu na nafasi za mahusiano kati yake na Muumba wake; jinsi gani ilivyo sumu kwa roho za wafanyakazi na kwa familia zao iwapo watathubutu kujitenga na Kristo; ni jinsi gani ilivyo hatari kujifanya adui wa Kristo au kuishi kwa kutojali uwepo wa Mungu na kufuata mapenzi yake. Iwapo mwanadamu katika shughuli zake za kila siku za kujikimu ataweka kipaumbele kwa maisha yake ya kiroho, atajipalilia wokovu wake na kuwa mfano wa haki na uaminifu kwa wote wanaomzunguka kwa ajili ya wokovu wao.

Sikiliza

 

19 July 2018, 16:42