Tafuta

Vatican News
Viongozi wapya wa Masista wa CDNK Kanda ya Kaskazini Magharibi wanapaswa kuwa ni mwanga na chumvi ya dunia Viongozi wapya wa Masista wa CDNK Kanda ya Kaskazini Magharibi wanapaswa kuwa ni mwanga na chumvi ya dunia. 

Masista wa Huruma, CDNK, Tanzania wazindua Kanda na Viongozi wapya!

Masista wafuatao wameteuliwa kuwa viongozi wakuu wa kwanza wa Kanda mpya nao ni: Sr. Benjamina Buya, CDNK ambaye atakuwa Mkuu wa Kanda. Sr. Maria Magdalena Mmanda, CDNK ambaye atakuwa ni Makamu mkuu wa Kanda; Sr. Emmanuela Mallya, CDNK, Mshauri; Sr. Anastazia Sala, CDNK, Mshauri. Viongozi wapya watasimikwa rasmi tarehe 15 Agosti 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusiana na Maisha ya Kitawa: “Perfectae Caritatis”, yaani “Upendo mkamilifu”, wanawataka watawa kupyaisha maisha yao, kwa kutoa nafasi ya kwanza katika maisha ya kiroho, mashauri ya kiinjili, maisha ya kijumuiya pamoja na malezi makini, kwa wale wote wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto na mwaliko wa kufanya mageuzi ya kina, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kushuhudia ile furaha na unabii unaofumbatwa katika nadhiri, umoja na udugu katika maisha ya kijumuiya, ushuhuda wenye mvuto!

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anawataka watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa watu wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, katika maisha na utume wao, ili kweli Yesu aweze kuwa kati pamoja na watu wake, na hatimaye, kuwakirimia matumaini na furaha tele katika maisha! Anasema, uaminifu kwa wito, maisha ya kitawa na kwa karama ya shirika ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili watawa katika maisha na utume wao katika ulimwengu mamboleo.

Mheshimiwa Sr. Theresia Seraphin Buretta, CDNK, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, anayo furaha kubwa, kuitangazia familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania kwamba, tarehe 31 Julai 2018, Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro kwa mara ya kwanza katika historia yake, tangu kuanzishwa kunako mwaka 1931, linazindua Kanda ya Kaskazini Magharibi; Jimbo kuu la Mwanza. Kanda hii itawahusisha Masista wote wa CDNK wanaofanya utume wao kwenye Kanda ya Ziwa Victoria.

Masista wafuatao wameteuliwa kuwa viongozi wakuu wa kwanza wa Kanda hii nao ni: Sr. Benjamina Buya, CDNK ambaye atakuwa Mkuu wa Kanda. Sr. Maria Magdalena Mmanda, CDNK ambaye atakuwa ni Makamu mkuu wa Kanda; Sr. Emmanuela Mallya, CDNK, Mshauri; Sr. Anastazia Sala, CDNK, Mshauri. Viongozi wapya watasimikwa rasmi tarehe 15 Agosti 2018 kwenye Makao ya asili, Huruma mkuu Rombo. Baada ya kusimikwa rasmi, tarehe 22 Agosti watapokelewa rasmi kwenye Kanda mpya, tayari kuanza utume wao.

Mama Mkuu wa Shirika, Sr. Theresia Buretta anasema, mchakato wa maboresho ya uongozi ndani ya Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, ulianza kunako mwaka 2001, baada ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kusoma taarifa ya mkutano mkuu wa Shirika, kupembua historia ya Shirika na maendeleo yake, likaagiza kufanyike mambo makuu matatu: kuligawa Shirika katika Kanda za uongozi; kuratibu malezi na majiundo ya masista na kuanza kuingia katika mchakato wa Shirika kuwa na haki ya mashirika ya kipapa. Kumbe, tamko hili ni sehemu ya utekelezaji wa ushauri uliotolewa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha na utume wa Shirika.

Uongozi  mpya wa Kanda uwe ni ushuhuda wa huduma na sauti ya kinabii, kwa wale wasiokuwa na sauti kutokana na sababu mbali mbali katika maisha yao! Viongozi watambue kwamba, wao ni alama ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waoneshe kwamba, inawezekana kuishi kwa amani, upendo, umoja na mshikamano wa kidugu, licha ya tofauti za makabila, mahali anapotoka mtu, uwezo wa kielimu na hata pengine kiuchumi! Yote haya ni kwa ajili ya sifa, utukufu na heshima ya Mwenyezi Mungu, asili ya miito yote ndani ya Kanisa.

Kanda mpya ya Shirika la CDNK iwe ni jumuiya na shule ya umoja, ili kuliwezesha Kanisa mahalia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Watawa wa CDNK wawe ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa watu wanaowahudumia na wale wanaowazunguka na kwamba, Kanisa halipendi kuwaona Watawa wasiokuwa na furaha, kwani furaha, amani na utulivu wa ndani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uzuri wa Injili na ufuasi kwa Kristo Yesu.

Daima watawa wawe na mwono wa kukazia mambo msingi katika maisha, wanapoendelea kutoa huduma kwa Kristo na Kanisa lake katika sekta ya elimu, afya, katekesi, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya watu wa Mungu. Watawa wa CDNK wawe ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu, kwa njia ya matendo, tayari kuwa ni vyombo vya umoja na mshikamano wa dhati, mashuhuda wa furaha na upendo wa Kristo unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa ndani na nje ya Tanzania.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

31 July 2018, 07:09