SECAM imezindua maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kilele ni Julai, 2019. SECAM imezindua maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kilele ni Julai, 2019. 

Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM, kilele ni Julai 2019

Tarehe 29 Julai 2018, SECAM imezindua mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1969. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Kilele chake kitakuwa ni mwezi Julai 2019

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashahidi wa Uganda waliotangazwa kuwa Wenyeheri na Papa Benedikto XV kunako tarehe 6 Juni 1920 na hatimaye, kutangazwa kuwa Watakatifu na Mwenyeheri Paulo VI tarehe 8 Oktoba 1964 ni utambulisho wa ushuhuda wa imani ya watu wa Mungu nchini Uganda. Leo hii Madhabahu ya Namgongo, yamekuwa ni kivutio kikuu cha imani kutoka kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Uganda. Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda anasema, hii ni alama ya shukrani kwa kazi na utume mkubwa uliofanywa na wamisionari waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo ambayo, leo hii imeenea sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, lakini, bado inapaswa kupyaishwa, kumwilishwa na kushuhudiwa, kama kielelezo cha imani tendaji.

Uganda inakumbukwa sana kuwa ni mahali palipozaliwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. Hiki kikawa ni chombo kinachoyaunganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. Kanisa Barani Afrika limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu, hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii. Kanisa pia limeendelea kuwa ni kikolezo cha mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, awamu ya pili, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, likibidishwa na imani na upendo unaomwilishwa katika matendo, liweze kuzaa matunda ya upendo, upatanisho, haki na amani kama utume wake endelevu na fungamani kwa ajili ya watu wa Mungu. Tarehe 29 Julai 2018, SECAM imezindua mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1969. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Kilele chake kitakuwa ni mwezi Julai 2019.

Hii ni nafasi kwa Kanisa Barani Afrika kuimarisha SECAM, ili kiweze kuwa ni chombo anasema Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM, cha sauti ya watu wa Mungu Barani Afrika. Hii ni fursa makini ya kurejea tena katika mambo msingi ya maisha ya Kikristo yanayofumbatwa katika: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Sala na Matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji. Maadhimisho ya Jubilei, ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, ili kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 tangu SECAM ilipoanzishwa.

Familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kumshukuru na Mungu na kuomba tena neema na baraka ya kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo, ili kweli Kanisa Barani Afrika liweze kuwa ni shuhuda na chombo cha haki, amani na upatanisho, unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Maadhimisho haya, licha ya kupambwa na kwa sala na tafakari, lakini iwe ni fursa ya ushuhuda wa Jumuiya za Kikristo, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo, lililojitambulisha kwa kwa kusali, kutafakari na kuumega mkate.

SECAM inapenda kuwahamasisha wakleri, watawa na waamini walei katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM, kama kielelezo na ushuhuda wa kukua na kukomaa kwa Kanisa Barani Afrika, ili kuweza kujikita zaidi katika mchakato wa kujitegemea na kulitegemeza Kanisa, changamoto pevu kwa wakati huu, ili kuondokana na aibu ya kuomba omba kila wakati, kwani kwa sasa watu wengi wamechoka na kwamba, ombi la msaada ni wimbo usiokuwa na kiitikio kwa wakati huu.

Umoja, upendo na mshikamano unaoshuhudiwa katika urika wa Maaskofu ni muhimu sana. Huu ni wakati mwingine tena kwa “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Kanisa Barani Afrika anasema Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga linawakumbuka na kuwaenzi makatekista na waalimu waliojitosa kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika hali na mazingira magumu, leo hii, familia ya Mungu inafurahia matunda ya uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa limekuwa mdau mkubwa wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ushuhuda unaojionesha kwa Kanisa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii katika ujumla wake. Ni wakati wa kufurahia mchango wa Kanisa katika maendeleo fungamani ya binadamu; kuomba msamaha pale ambapo Kanisa limeelemewa na udhaifu na mapungufu ya watoto wake, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wadhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu, ili siku moja, waweze kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

30 July 2018, 11:45