Tafuta

Genfest, Manila nchini Ufilippini 2018 imekuwa ni fursa ya vijana kukutana, kusali na kutafakari kuhusu changamoto za maisha. Genfest, Manila nchini Ufilippini 2018 imekuwa ni fursa ya vijana kukutana, kusali na kutafakari kuhusu changamoto za maisha. 

Genfest Manila: Vijana wa kizazi kipya watimua vumbi la imani, matumaini na mapendo

Genfest, Manila 2018 imekuwa nifursa ya kusikiliza: umuhimu wa mshikamano, maridhiano katika kuleta na kujenga misingi ya haki, amani pamoja na kuunga mkono utamaduni wa msamaha dhidi ya utamaduni wa kisasi na chuki zisizo na mashiko wala mvuto! Na zaidi sana kusisitiza kuwa, binadamu wote ni sawa na ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi.

Na Frt. Karoli Joseph Amani, Jimbo kuu Katoliki Tabora, - Vatican.

Hivi karibuni vijana wa Chama cha Kitume cha Wanafokolari walikutana jijini Manila, nchini Ufilippini katika kumbi za World Trade Centre, kwa ajili ya Kongamano la Vijana maarufu kama “Gen Fest”. Kongamano hilo huandaliwa na kuratibiwa na wana vuguvugu la Wafokolari na lilianzishwa mnamo mwaka 1973 na Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich mwanzilishi wa Wafokolari.

Maadhimisho ya “Gen Fest” hufanyika kila baada ya miaka sita. Hili toleo la 11 la  maadhimisho haya tangu yalipoanzishwa na limehudhuriwa na takribani na vijana 6000 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Pamoja na wawakilishi wengine kutoka Barani Afrika walikuwepo wawakilishi kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Mali, Benin, Jamhuri ya kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, Burkinafaso na Cameroon. Kauli mbiu ilikuwa ni vuka mipaka yote (beyond all boarders). Lengo kuu la maadhimisho haya ya vijana ni kuwakutanisha pamoja vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani; kukusanya nguvu, kuelimishana na kubadilishana uzoefu na mang’amuzi yao juu ya namna ya kufaa zaidi kujenga ulimwengu wenye mshikamano na umoja (Rej. Yoh. 17,21) baina ya watu wote na kukuza amani duniani.

Kama ilivyo desturi, walipo vijana, hazikosekani: nyimbo, furaha na shangwe, vijana walipata fursa ya kufaidi maonesho mbalimbali ya sanaa na tamaduni hususan katika Bara la Asia. Kwa mara ya kwanza kabisa maadhimisho haya yanafanyika nje ya Bara la Ulaya. Vilevile, washiriki walisikia shuhuda kutoka kwa vijana wenzao, shuhuda ambazo zilielezea umuhimu wa mshikamano, maridhiano katika kuleta na kujenga misingi ya haki, amani pamoja na kuunga mkono utamaduni wa msamaha dhidi ya utamaduni wa kisasi na chuki zisizo na mashiko wala mvuto! Na zaidi sana kusisitiza kuwa, binadamu wote ni sawa na ndugu wamoja licha ya tofauti zao za kinasaba, utaifa, rangi, makabila na anakotoka mtu! Hii inatokana na ukweli kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wana asili na haki sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Semina za kina zilitolewa na zikijikita katika masuala mbalimbali yakiwemo:  wajibu wa kila mmoja kutoa mchango katika kukuza amani duniani, utunzaji bora wa mazingira, ujenzi wa uchumi shirikishi, wajibu katika jamii, uhamiaji, uraia wa kimataifa, sanaa na utamaduni; majadiliano na mahusiano na waamini wa dini mbali mbali. Suala la majadiliano ya kidini na kiekumene lilionekana kuwa lina umuhimu wa kipekee katika kusaidia kufahamiana vizuri na kuunganisha nguvu katika kujenga ulimwengu wenye amani, furaha, ukweli na utu kwa wote bila kumuacha mtu awaye yote akichechemea nyuma!

Maadhimisho haya yalihudhuriwa pia na Maaskofu Katoliki kutoka nchini Ufilippini, miongoni mwao alikuwa ni Kardinali Luis Antonio Chito Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila ambaye aliongoza adhimisho la Ekaristi Takatifu siku ya kuhitimisha maadhimisho haya hapo tarehe 8 Julai 2018. Katika mahubiri yake, Kardinali Tagle aliwahimiza vijana kuruhusu upendo ufungue macho na mioyo yao, ili neema ya Mungu iweze kuondoa ule upofu wa ndani, unaosababishwa na ujuaji kupita kiasi na ubinafsi wa wanadamu kiasi hata cha kutaka kujenga na kudumisha kuta za utengano wa kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kardinali Tagle akitumia mfano wa wito wa Nabii Ezekieli (Ezekieli 2:2-5), aliwasihi vijana kuwa jasiri, kuchangamkia na kupokea miito ambayo Mwenyezi Mungu anawaitia hata kama inaonekana kuwa na changamoto nyingi. Kuamini sana katika nguvu binafsi kunaweza kusababisha mtu kukata tamaa na hatimaye, kubwaga manyanga! Kardinali Tagle aliwasihi vijana kugundua chanzo cha nguvu na mafanikio yao katika neema na huruma ya Mungu kwao na wala si ujanja, umashuhuri na umahiri wa kijana katika kufanikisha mambo.

Katika kuhitimisha mahubiri yake, Kardinali Tagle aliwaomba vijana msamaha kwa niaba ya watu wazima na wazee wote, kwani wanawakabidhi vijana ulimwengu uliogubikwa na chuki, uzandiki, malalamiko, mipasuko katika jamii, vita na kinzani; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote unaoendelea kusababisha majanga na maafa makubwa sehemu mbali mbali za dunia. Wanawake, vijana na watoto kutekwa na kuuzwa kama bidhaa katika soko la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo na habari mbaya na za udaku kusambaa kwa kasi kubwa zaidi kuliko habari njema.

Pamoja na kasheshe patashika nguo kuchanika, Kardinali Tagle alikiri na kuonesha imani yake kwa vijana, akisisitiza kwamba, anafahamu na kutambua: uwezo, nia njema na ujasiri wa kubadilisha hali halisi ya mambo. “Nendeni mkaendelee kuvuka mipaka ya chuki, mateso na vita kwa sababu nyuma ya mipaka hiyo Yesu anawasubiri” Kardinali Tagle alihitimisha wosia wake wa kibaba, huku akiwaacha vijana wengi, wakiwa wameshika tama kutokana na umahiri wake wa kuchambua: changamoto, matatizo na matumaini ya vijana wa kizazi kipya.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa nchini Ufilippini linaadhimisha Mwaka wa wakleri na maisha ya wakfu uliozinduliwa mwaka 2017 na utakamilishwa mwaka 2018. Sanjari na hili, Kardinali Tagle alitumia vizuri fursa ya “Gen Fest” kwa kuwahamasisha vijana kujiunga na miito mitakatifu ya upadre na utawa, ndoa na familia akiwahakikishia vijana kwamba, katika miito hiyo Yesu hataondoa uzuri na ulimbwende wao, bali ataufanya kuwa maradufu zaidi katika huduma ndani ya Kanisa lake, moja, takatifu, katoliki na la mitume. Anasema, kuna raha ya kujisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Yaani, we acha tu!

Kwa upande wake, Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha Kitume cha Wafokolari aliinyaka nafasi hii ya kukutana na vijana kwa kuwatia moyo na kuwahamasisha kusonga mbele katika mkakati wa kuufanya ulimwengu na mataifa yote kuwa kitu kimoja; kwa kukuza sanaa na utamaduni wa urafiki. Yeye mwenyewe “Emmaus” kama anavyojulikana kwa wanafokolari, alishuhudia kwamba, daima katika safari zake sehemu mbalimbali ulimwenguni, ameguswa sana na vijana kwa uhai na uchangamfu wao; ubunifu na ujasiri; katika juhudi zao za kuhekimishana na kuhamasishana juu ya: haki, amani na umoja kwa watu wote duniani. Alisisitiza kwamba, lengo kuu la “Gen Fest” ni kulifikia lile tamanio thabiti la Yesu Kristo “ili wote wawe na umoja” (Yoh 17:21).

Mama Maria Voce aliwaambia vijana kwamba, ipo siri ya kutimiza wajibu huo wa kuleta: haki, amani na umoja ulimwenguni, nayo imejificha katika maneno matatu msingi; kupenda, kuanza upya na kushirikishana. Kwa kupendana kama ndugu, kuanza upya tena baada ya misukosuko na kushirikishana vipaji, uzoefu an changamoto vijana wanaweza kupiga hatua kubwa. Zaidi sana Mama Maria Voce aliwahimiza vijana kutumia nafasi na ubunifu wao wote kujenga mtandao wa familia Mungu duniani inayofumbatwa katika: umoja, upendo na mshikamano wa dhati, wakijitahidi wao wenyewe kuwa: vyombo na mashuhuda wa umoja na wenye uwezo wa kuthamini utamaduni wa watu wengine.

Ni wazi kwamba vijana hawa zaidi ya elfu sita kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wataisambaza roho ya “Gen Fest” katika vijiji, miji na mataifa yao mbalimbali. Wakiungwa mkono na kusaidiwa, ulimwengu utakuwa bora kuliko ilivyokuwa jana.

Hii ni taarifa iliyotumwa na Frt. Karoli Joseph Amani, wa Jimbo kuu Katoliki Tabora, Tanzania kutoka Ufilippini, lakini kwa sasa anaendelea kufundwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana – Roma. Itakumbukwa kwamba, Frt. Karoli alikuwa mhariri wa Jukwaa la Vijana wa Afrika wakati wa maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa, mwezi Oktoba, 2018. Vijana wanasema, wamemkubali sana! Big up, Jandokasisi Karoli Joseph Amani.

 

26 July 2018, 09:10