Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limetoa tamko kuhusu wakimbizi na wahamiaji, ili kuwapokea na kuondokana na hofu zisizo na msingi. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limetoa tamko kuhusu wakimbizi na wahamiaji, ili kuwapokea na kuondokana na hofu zisizo na msingi.  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, latoa tamko kuhusu wakimbizi na wahamiaji.

Baraza la Maaskofu katoliki Italia limeitaka Serikali pamoja na wadau mbali mbali nchini Italia kuondokana na hofu zisizo na msingi kuhusu wakimbizi na wahamiaji na kuanza mchakato wa kuwapokea na kuwakirimia, kwani hawa ni watu ambao wameathirika kutokana na vita, kinzani, nyanyaso, umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, kuna haja kwa Serikali pamoja na wadau mbali mbali kuondokana na hofu zisizokuwa na msingi kuhusu wakimbizi na wahamiaji na kuanza kujikita katika mchakato wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi katika maisha ya familia ya Mungu nchini Italia. Hawa ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ni watu ambao wameathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi, umaskini na magonjwa na kwa sasa wanatafuta: usalama, hifadhi na maendeleo. Si wakati muafaka wa kujenga kuta za utengano na badala yake, Serikali mbali mbali zielekeze zaidi katika kuimarisha utamaduni wa mshikamano na uwajibikaji kama njia sahihi ya kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, ili hatimaye, kujenga na kudumisha haki na amani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasikitika sana kwa lugha inayotumiwa dhidi ya wakimbizi na wahamiaji kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, kiasi cha kuwajengea wananchi wa Italia, hofu na mashaka yasiyokuwa na mvuto wala mashiko na matokeo yake, wananchi wanajenga hofu, kiasi hata cha kushindwa kuwakaribisha na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji. Maaskofu wanawapongeza wananchi wote wa Italia ambao wameonesha ujasiri, ari na moyo wa huruma na mapendo kwa kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, kama kielelezo cha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linawataka wadau mbali mbali kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Wakati huo huo, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaunga mkono tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuhusu umuhimu wa kuwapokea wakimbizi na wahamiaji kwa kuondona na hofu zisizokuwa na mashiko na kuanza ujenzi wa madaraja ya upendo na mshikamano, ili kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kukumbusha kwamba, maskini hawa ni amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Huu ni wakati wa ujenzi wa utamaduni shirikishi na unaolinda na kuwatetea wanyonge.

Mama Kanisa anapenda kuwaonesha upendo wake wa dhati, wakimbizi na wahamiaji, katika hatua mbali mbali za safari yao, tangu wanapoondoka, wanapofika na hatimaye, kurejea tena makwao hali inaporuhusu. Waamini wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kuyavalia njuga matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji kwa kuwaonesha moyo wa ukarimu, hekima na busara kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake. Lakini, wote kwa pamoja wanaweza kujibu changamoto hizi kwa kujikita katika mchakato unaofumbatwa katika mambo makuu yafuatayo: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji”.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kuingia katika nchi husika kwa njia salama zinazozingatia sheria za nchi; kwa kutoa hati za kusafiria na kuwapatia wakimbizi na wahamiaji nafasi ya kuweza kukutana na kujiunga tena na familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya na Mashirika mbali mbali yatasaidia kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali tete zaidi.

Watu wanaokimbia vita, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu, waangaliwe kwa jicho la huruma kwa kupewa hati za muda na huduma makini kadiri ya utu na heshima yao kama binadamu, ili kutoa nafasi kwa watu hawa kukutana na wenyeji wao, ili hatimaye, kuboresha huduma, daima usalama na utu wa mtu, ukipewa kipaumbele cha kwanza kabla hata ya kuangalia usalama wa taifa, sanjari na kuvifunda vyema vikosi vya ulinzi na usalama kwenye mipaka ya nchi. Wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, hawana budi kuhakikishiwa usalama na huduma msingi, kwa kuheshimu utu wao kama binadamu na kuondokana kabisa na mtindo wa kuwaweka kizuizini wakimbizi na wahamiaji wasiokuwa na nyaraka za kusafiria.

Sikiliza

 

20 July 2018, 17:27