Tafuta

Vatican News
Mkutano wa 19 wa AMECEA Mkutano wa 19 wa AMECEA 

Askofu Mfumbusa asema, watu wajenge utamaduni wa haki, amani na mshikamano

Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa nchini Tanzania wakati wa maadhimisho ya mkutano 19 wa AMECEA amesema, kuna tofauti kubwa sana katika nchi za AMECEA, tofauti ambazo zinajikita katika: lugha, tamaduni, mila na desturi, changamoto kubwa ni kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kukamilishana katika tofauti zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Familia ya Mungu Afrika Mashariki ya Kati haina budi kujielekeza zaidi katika kujenga mazingira yatakayowawezesha watu mbali mbali kupata haki zao msingi; kwa njia ya kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi; mambo ambayo yanafumbatwa kimsingi katika hadi na utu wa ndani kabisa wa binadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, usawa wa watu ni sehemu ya hadhi yao kama binadamu na kwamba kuna haki zinazotokana na hadhi hii. Tofauti za kibinadamu ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu anayetaka watu wake kushirikiana, kushikamana, kutajirishana na kukamilishana.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa katika mahojiano maalum na Vatican News mjini Addis Ababa anasikitika kusema kwamba, tofauti za kidini, kikabila, kisiasa na kitamaduni zimekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa baadhi ya nchi za AMECEA, changamoto ambayo kwa sasa inavaliwa njuga, ili kushughulikiwa kikamilifu na Mabaraza ya Maaskofu katika nchi zao husika.

Askofu Mfumbusa anaendelea kufafanua kwamba, kuna tofauti kubwa ya lugha, tamaduni, mila na desturi miongoni mwa familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati na wakati mwingine, tofauti hizi zinajitokeza hata kati ya nchi yenyewe au mkoa hadi mkoa. Kuna tofauti za mtindo wa maisha: kuna jamii za wakulima, wavuvi na wafugaji, ndiyo maana kuna haja ya kudumisha amani na utulivu kwani mara nyingi jumuiya za wakulima zimesigana sana na jumuiya za wafugaji na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kwa kugombania maeneo ya malisho au mashamba kwa ajili ya kilimo.

Inasikitisha sana kuona kwamba, baadhi ya wanasiasa wanatumia kinzani, chuki na migogoro kati ya wananchi wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa ajili ya kujiimarisha kisiasa, kwa kutafuta nafasi za madaraka na hatimaye kujipatia fedha, mali na heshima. Baadhi ya wanasiasa wamediriki hata kutumia migogoro ya kidini na kikabila kwa ajili ya mafao yao binafsi, huku watu wengi wakiteseka kutokana na machafuko, vita na magomvi.

Ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni raia wa kawaida. Ndiyo maana Mababa wa AMECEA wanakazia umuhimu wa kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuendelezwa na wala kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Umoja na mshikamano, haki na amani vinawezekana kabisa ikiwa kama watu wataonesha utashi unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene.

Asilimia 90% ya wakazi wa Jimbo Katoliki la Kondoa, nchini Tanzania ni waamini wa dini ya Kiislam. Waamini hawa wamekuwepo Kondoa kwa miaka mingi, kiasi kwamba, kwa wema na ukarimu wao, waliweza kuwakaribisha wamisionari walipofika eneo la Kondoa na kuwapatia hata sehemu ya ardhi kwa ajili ya kujenga Makanisa. Kinzani na mipasuko kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo ilianza baada ya uhuru wa Tanganyika, lakini tofauti hizi kwa sasa zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi na viongozi wa kidini, lengo likiwa ni kujenga na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano wa watanzania kama utambulisho wao makini na wala si kutokana na dini, makabila wala mahali wanakotoka.

Ikumbukwe kwamba, misimamo mikali ya kidini ni hatari sana kwa umoja wa kitaifa na mafungamano ya kijamii. Mababa wa AMECEA wanakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa familia ya Mungu kupata elimu ya mawasiliano ili waweze kutumia vyema vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kwa kufikiri na kuwajibika; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwani majuto ni mjuu na baada ya kisa ni mkasa!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliona umuhimu elimu ya mawasiliano ya jamii kwa majandokasisi, lakini kwa bahati mbaya kabisa, Kanisa limechelewa kutekeleza dhamana hii, lakini, anasema Askofu Mfumbusa huu ndio wakati wake, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linawaandaa Mapadre wake wa baadaye katika tasnia ya habari na mawasiliano kama sehemu ya mbinu mkakati wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kisasa.

Sikiliza

 

18 July 2018, 17:30