Cerca

Vatican News
AMECEA imekamilisha mkutano wake mkuu wa 19 kwa kumchagua Askofu Charles kasonde kuwa Mwenyekiti na Padre Anthony Makunde kuwa Katibu mkuu wa AMECEA AMECEA imekamilisha mkutano wake wa 19 kwa kumchagua Askofu Charles Kasonde kuwa Mwenyekiti na Padre Anthony Makunde kuwa Katibu mkuu wa AMECEA. 

Askofu Charles Kasonde na Padre Anthony Makunde, wachaguliwa kuongoza AMECEA

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa kipindi cha miaka minne, tarehe 21 Julai 2018 amemtangaza Askofu Charles Kasonde, kuwa Mwenyekiti mpya wa AMECEA kwa kipindi cha miaka minne kuanzia sasa na Padre Anthony Makunde kutoka Mbeya, Tanzania ameteuliwa kuwa Katibu mkuu wa AMECEA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, lililokuwa linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”, umemalizika kwa kuchagua viongozi watakaongoza jahazi kwa muda wa miaka minne kuanzia sasa.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa kipindi cha miaka minne, tarehe 21 Julai 2018 amemtangaza Askofu Charles Kasonde, kuwa Mwenyekiti mpya wa AMECEA kwa kipindi cha miaka minne kuanzia sasa. Askofu Kasonde alizaliwa tarehe 14 Desemba 1968, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 4 Agosti 2001 Jimboni Ndola, Zambia. Tarehe 23 Machi 2010 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Solwezi na kuwekwa wakfu tarehe 29 Mei 2010.

Mababa wa AMECEA wamemteua Mheshimiwa Padre Anthony Makunde kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania kuwa Katibu mkuu mpya wa AMECEA na hivyo kuchukua nafasi ya Padre Ferdinand Lugonzo aliyemaliza muda wake. Wakati huo huo, AMECEA imemteua Mheshimiwa Padre Stephen Mbugua, kutoka Jimbo Katoliki la Nakuru, kuwa Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashari na Kati, CUEA. Padre Mbugua anachakua nafasi ya Padre Justus Mbae ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.

Askofu Charles Kasonde katika mahojiano maalum na Vatican News amegusia mambo msingi ambayo yamejadiliwa na Mababa wa AMECEA na utekelezaji wake unapaswa kuanza mara moja kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi husika: Kukuza na kudumisha tofauti msingi miongoni mwa familia ya Mungu kama utajiri, ili kusimama kidete kulinda utu, haki msingi za binadamu, umoja, haki na amani. Mababa wa AMECEA wameonesha pia mshikamano wao wa dhati na shukrani kwa Ethiopia na Eritrea ambazo kwa sasa zinaanza mchakato wa kujenga umoja na amani.

AMECEA inaitaka Sudan ya Kusini kujibidisha zaidi, ili kumaliza mgogoro wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. AMECEA imekazia tunu msingi za ndoa na familia, utume miongoni mwa vijana, matumizi sahihi ya njia za mawasiliano ya jamii katika ulimwengu wa digitali, ekolojia fungamani, ushirikiano; usalama na hifadhi za kijamii kwa wakleri na watawa, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; dhamana na nafasi za vyuo vikuuu na taasisi za elimu ya juu; uwajibikaji katika kuendesha taasisi za Kanisa; misimamo mikali ya kidini na kiimani; rushwa na ufisadi; dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Ulinzi na usalama kwa watoto wadogo pamoja na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Sikiliza

 

23 July 2018, 08:57