Tafuta

Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia. 

Kanisa halina budi kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho ndani na nje ya AMECEA.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, awamu ya pili, walilitaka Kanisa kujizatiti zaidi katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu kama kikolezo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi amewataka Mababa wa AMECEA kudumisha juhudi hizi hata nje ya AMECEA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. -Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika walijikita kwa namna ya pekee katika mchakato wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika na kwamba, Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa haki, amani na upatanisho ndani na nje ya Bara la Afrika kama njia ya kuonesha mshikamano na watu wa Mungu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mkutano wa AMECEA, amewataka Mababa wa AMECEA kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya haki, amani, umoja na upatanisho kati ya watu wa Mungu ndani na nje ya Ukanda wa nchi za AMECEA. Kuna watu wanaoteseka na kunyanyasika kutoka na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii huko nchini DRC, Cameroon pamoja na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati. Hawa wanateseka kwa sababu ya chuki na uhasama; ukabila na udini, umaskini na hali ngumu ya maisha bila kusahau kwamba, kuna baadhi ya Serikali zimeshindwa kutekeleza dhamana ya ulinzi na usalama kwa raia wake.

Maaskofu wanapaswa kuwa ni sauti ya kinabii dhidi ya nyanyaso na dhuluma zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mfano, leo hii, kuna watu wanaofariki dunia kila kukicha kutokana na vita, umaskini, njaa na maradhi huko Yemen; mipasuko ya kisiasa inaendelea kusababisha maafa makubwa huko Palestina, kiasi kwamba, matukio yote haya yanaandika kurasa chungu za maisha ya watu wa Mungu katika maeneo haya. Tema mbali mbali ambazo zimechambuliwa na Mababa wa AMECEA, zifanyiwe tafakari ya kina na kwa maongozi ya Roho Mtakatifu zitolewe maamuzi yatakayofanyiwa kazi na Mababa wa AMECEA, ili, Kanisa kweli liendelee kuwa ni sauti ya kinabii si tu kwa maneno bali kwa njia ya matendo thabiti!

Kwa upande wake, Askofu Joseph Antony Zziwa, Mwenyekiti wa Idara ya Haki, Amani na Upendo ya AMECEA amepembua kwa kina na mapana kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Amesema, nchi nyingi za AMECEA kwa sasa zinakabiliwa na machafuko ya kisiasa, kijamii na kitamaduni kutokana na watu kuathiriwa na utandawazi usiojali wa la kuguswa na mahangaiko ya wengine katika masuala ya kisiasa, kijamii, kidini na kitamaduni. Hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Mababa wa AMECEA ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu katika mwanga wa Injili. Chokochoko na mipasuko ya kijamii na kisiasa inafumbatwa katika: udini, ukabila na umajimbo.

Tofauti mtetemo: Nchi za AMECEA zinatofautiana sana kutokana na wingi wa makabila, tamaduni, mila na desturi; lugha na mitindo ya maisha pamoja na dini; mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kuwa ni utajiri na amana kubwa, inayopaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Utofauti ni alama ya nguvu katika nchi za AMECEA na kamwe tofauti hizi hazipaswi kuwagawa na kuwasambaratisha watu wa AMECEA. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile kwani binadamu wote wameumbwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wanayo hadhi sawa!

Umoja wa amani: Amani ya kweli ni tunda la haki na mapendo; ukweli na uhuru kamili. Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha mwanadamu! Kushindwa kwa amani kutawala katika akili na nyoyo za watu, matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na hata pengine mauaji ya kimbari. Tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu wa AMECEA ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa binadamu, ili kuheshimiana, kuthaminiana na kukamilishana. Kamwe tofauti hizi zisiwe ni chanzo cha vita na mipasuko ya kijamii.

Ndani ya Mwenyezi Mungu: Mababa wa AMECEA wametaka kwamba, tofauti mtetemo, hadhi sawa, umoja na amani viwaambate na kuwashikamanisha watu wa Mungu ndani na nje ya Ukanda wa AMECEA, kama kieleleo cha Ukatoliki wao unaofumbatwa pia katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wamekombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.

Askofu Joseph Antony Zziwa anasema, familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati, inapaswa kushikamana na kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya uchumi unaobagua na kuwatenga watu; vita na ukosefu wa haki, amani na demokrasia ya kweli. Familia ya Mungu katika Ukanda wa AMECEA inapaswa kujikita katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya, vipigo vya wanawake na “hata wakati mwingine wanaume” majumbani; ukabila na udini usiokuwa na mvuto wala mashiko. Matokeo yake ni watu kuendelea kutumbukizwa katika umaskini, ujinga na maradhi; maadui wakubwa wanaokwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Mababa wa AMECEA wanaitaka familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu tunu msingi za Kiinjili na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amekazia umuhimu wa kudumisha utu wa binadamu kama njia ya kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii ndani na nje ya Afrika Mashariki na Kati. Watu wapate mahitaji na haki zao msingi bila ya kubaguliwa kutokana na sababu yoyote ile! Watu wasipuuzwe, kutengwa wala kudhalilishwa kiasi hata cha kukosa ulinzi na usalama katika maisha yao, kwani wote wana haki na utu sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa liwe ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni. Maendeleo endelevu na fungamani yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu.

Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Nchi za AMECEA, ACWECA, lililoanzishwa kunako mwaka 1974 na kwa sasa linawajumuisha Watawa wa kike zaidi ya 20, 000. ACWECA pamoja na mambo mengine, linapania kukuza na kuendeleza majiundo makini ya watawa; kuwajengea uwezo watawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani pamoja na kujitegemea.

Ni Shirikisho linalotoa msaada wa kiufundi kwa Mashirika ya Kitawa, ili kweli watawa waweze kuwa ni Mashahidi wa Kristo kati ya watu wanaowahudumia katika sekta mbali mbali za maisha. Sr. Cecilia Njeri, LSOSF, Rais wa Shirikisho hili amewataka Mababa wa AMECEA kuwaangalia watawa kama sehemu muhimu sana ya mihimili ya uinjilishaji na wala si wapinzani wao. Watambue na kuthamini mchango na huduma inayotolewa na watawa katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi, maendeleo na katekesi shuleni na parokiani.

Mshikamano wa dhati ni chachu muhimu sana ya uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hapa kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha watawa katika kuamua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji katika Ukanda wa AMECEA.

Sr. Cecilia Njeri, Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Nchi za AMECEA, anasema, ACWECA inajivunia mafanikio iliyokwisha kuyapata katika kipindi cha miaka 44 cha uwepo na utume wake. Mpango Mkakati wa Maendeleo kati ya Mwaka 2017- 2022 unakazia pamoja na mambo mengine: Majiundo na utume; familia na vijana; haki na amani; uumbaji fungamani na kwamba, wanataka kuzitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, Afrika Mashari na Kati.

Sikiliza

 

20 July 2018, 17:16